Old/New Testament
Baadhi ya Watu Wawa na Mashaka na Mamlaka ya Yesu
(Mt 12:38-42; Mk 8:12)
29 Baada ya kundi la watu kuongezeka na kumzunguka, Yesu alisema, “Ninyi watu mnaoishi sasa ni waovu. Mnaomba muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu. Lakini hakuna muujiza utakaofanyika ili kuwathibitishia jambo lolote. Ishara pekee mtakayopata ni kile kilichompata Yona.[a] 30 Yona alikuwa ishara kwa watu walioishi katika mji wa Ninawi. Ni sawasawa na Mwana wa Adamu atakavyokuwa ishara kwa watu wa wakati huu.
31 Siku ya hukumu, ninyi watu mnaoishi sasa, mtalinganishwa na Malkia wa Kusini,[b] naye pia, atakuwa shahidi atakayeonyesha namna mlivyo waovu. Kwa nini ninasema haya? Kwa sababu alisafiri kutoka mbali, mbali sana ili ayasikilize mafundisho yenye hekima ya Suleimani. Na ninawaambia mkuu[c] kuliko Suleimani yupo hapa, lakini hamnisikilizi!
32 Siku ya hukumu, ninyi watu mnaoishi sasa mtafananishwa pia na watu wa Ninawi, nao watakuwa mashahidi watakaoonyesha makosa yenu. Ninasema hivi kwa sababu Yona alipowahubiri, walibadili mioyo na maisha yao. Na sasa mnamsikia mtu aliye mkuu kuliko Yona, Lakini hamtaki kubadilika!
Iweni Mwanga kwa Ajili ya Ulimwengu
(Mt 5:15; 6:22-23)
33 Hakuna mtu anayechukua taa na kuiweka mahali palipofichika au kuifunika. Badala yake huiweka mahali palipo wazi, ili wanaoingia ndani waweze kuiona nuru yake. 34 Namna unavyowatazama watu inaonesha kwa hakika jinsi ulivyo. Unapowatazama watu katika hali isiyo ya ubinafsi, inaonesha wazi kuwa umejaa nuru. Lakini unapowatazama watu katika namna ya uchoyo, ni wazi kuwa umejaa giza.[d] 35 Hivyo iweni waangalifu ili nuru iliyo ndani yenu usiwe giza! 36 Ikiwa umejaa nuru na hakuna sehemu yenye giza ndani yako, basi utang'aa, kama nuru ya kwenye taa.”
Yesu Awakosoa Viongozi wa Kidini
(Mt 23:1-36; Mk 12:38-40; Lk 20:45-47)
37 Baada ya Yesu kumaliza kuzungumza, Farisayo mmoja alimwalika Yesu kula pamoja naye. Hivyo Yesu alikwenda na kuketi sehemu ya kulia chakula. 38 Lakini Farisayo alishangaa alipoona Yesu hakunawa[e] mikono yake kwanza kabla ya kuanza kula. 39 Bwana akamwambia, “Usafi mnaoufanya ninyi Mafarisayo ni kama kusafisha kikombe au sahani kwa nje tu. Lakini ndani yenu mna nini? Mnataka kuwadanganya na kuwaumiza watu tu. 40 Ninyi ni wajinga! Aliyeumba kilicho nje ndiye aliumba kilicho ndani. 41 Hivyo, jalini vilivyo ndani. Wapeni vitu wenye uhitaji. Ndipo mtakuwa wasafi kikamilifu.
42 Lakini, ole wenu ninyi Mafarisayo! Mnampa Mungu sehemu ya kumi ya vyakula mnavyopata, hata mnanaa, na hata kila mmea mdogo katika bustani[f] zenu. Lakini mnapuuzia kuwatendea haki wengine na kumpenda Mungu. Haya ni mambo mnayotakiwa kufanya. Na endeleeni kufanya mambo hayo mengine.
43 Ole wenu ninyi Mafarisayo, kwa sababu mnapenda kupata viti vya heshima katika masinagogi. Na mnapenda kusalimiwa na watu kwa kuheshimiwa sehemu za masoko. 44 Ole wenu, kwa kuwa mnafanana na makaburi ya zamani yasiyoonekana, ambayo watu hupita juu yake na kuyakanyaga bila kuyatambua.”
45 Mmoja wa wanasheria akamwambia Yesu, “Mwalimu, unaposema mambo haya kuhusu Mafarisayo unatukosoa hata sisi pia.”
46 Yesu akamjibu, “Ole wenu, enyi wanasheria! Mnatunga sheria kali ambazo ni vigumu watu kuzitii.[g] Mnawalazimisha wengine kuzitii sheria zenu. Lakini ninyi wenyewe hamthubutu hata kujaribu kufuata mojawapo ya sheria hizo. 47 Ole wenu kwa kuwa mnajenga makaburi ya manabii. Lakini hawa ni manabii wale wale ambao mababu zenu waliwaua. 48 Na sasa mnawaonesha watu wote kwamba mnakubaliana na mambo ambayo baba zenu walifanya. Waliwaua manabii, nanyi mnasherehekea mauaji hayo kwa kujenga makaburi ya manabii! 49 Hii ndiyo sababu ambayo kwa Hekima yake Mungu alisema, ‘Nitawatuma manabii na mitume[h] kwao. Baadhi ya manabii na mitume wangu watauawa na watu waovu. Wengine watateswa sana.’
50 Hivyo ninyi watu mnaoishi sasa mtaadhibiwa kwa sababu ya vifo vya manabii wote waliouawa tangu mwanzo wa ulimwengu. 51 Mtachukuliwa wenye hatia kutokana na vifo hivyo vyote, tangu kuuawa kwa Habili mpaka kuuawa kwa nabii Zakaria,[i] aliyeuawa kati ya madhabahu na Hekalu. Ndiyo ninawaambia, kizazi hiki kitaadhibiwa kwa sababu yao wote.
52 Ole wenu, ninyi wanasheria, mmechukua ufunguo wa kujifunza kuhusu Mungu. Ninyi wenyewe hamtaki kujifunza na mmewazuia wengine wasijifunze pia.”
53 Yesu alipotoka humo, walimu wa sheria na Mafarisayo walianza kumpinga sana. Walianza kumjaribu ili awajibu maswali kuhusu mambo mengi, 54 ili Yesu akisema jambo isivyo sahihi waweze kupata sababu ya kumkosoa.
© 2017 Bible League International