Old/New Testament
Simulizi Kuhusu Msamaria Mwema
25 Kisha mwanasheria mmoja alisimama ili amjaribu Yesu. Akasema, “Mwalimu, ninatakiwa nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”
26 Yesu akamwambia, “Imeandikwa nini katika torati? Unaielewaje?”
27 Yule mwana sheria akajibu, “‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote.’(A) Pia ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe.’”(B)
28 Yesu akasema, “Jibu lako ni sahihi. Fanya hivi nawe utaupata uzima wa milele.”
29 Lakini mwanasheria alitaka kuonesha kuwa alikuwa mwenye haki na aliishi kwa usahihi. Hivyo akamwuliza Yesu, “Lakini si kila mtu aliye jirani yangu, au unasemaje?”
30 Katika kujibu swali hili, Yesu akasema, “Mtu mmoja alikuwa anasafiri kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko. Akiwa njiani alivamiwa na majambazi, wakamchania nguo na kumpiga. Kisha wakamwacha amelala chini akiwa katika hali ya kufa.
31 Ikatokea kuwa kuhani mmoja alikuwa anasafiri kupitia njia hiyo hiyo. Alipomwona, hakusimama ili amsaidie, alikwenda zake. 32 Kisha Mlawi[a] alipokaribia na kumwona yule mtu, alipita upande mwingine. Hakusimama ili amsaidie, Alikwenda zake.
33 Ndipo Msamaria[b] mmoja aliyekuwa anasafiri kupitia njia ile ile, alipofika mahali ambapo mtu aliyejeruhiwa alikuwa amelala, alipomwona alimhurumia. 34 Alimkaribia ili amsaidie, akamsafisha majeraha kwa mafuta ya zeituni na divai,[c] kisha akayafunga majeraha yake. Msamaria alikuwa na punda. Akampandisha juu ya punda wake na kumpeleka mpaka kwenye nyumba ya wageni. Akamhudumia huko. 35 Siku iliyofuata, Msamaria alitoa sarafu mbili za fedha na kumpa mtunza nyumba ya wageni, akamwambia, ‘Mtunze mtu huyu aliyejeruhiwa. Ukitumia pesa nyingi zaidi kwa kumhudumia, nitakulipa nitakapokuja tena.’”
36 Kisha Yesu akasema, “Ni yupi kati ya hawa watu watatu unadhani hakika alikuwa jirani wa yule mtu aliyepigwa na majambazi?”
37 Mwanasheria akajibu, “Ni yule aliyemsaidia.”
Yesu akasema, “Basi nenda ukafanye kama alivyofanya.”
Maria na Martha
38 Yesu na wafuasi wake walipokuwa wanasafiri, walifika katika kijiji kimoja. Mwanamke aitwaye Martha alimkaribisha nyumbani kwake. 39 Alikuwa na mdogo wake aliyeitwa Mariamu. Mariamu alikuwa amekaa karibu na Yesu akimsikiliza anavyofundisha. 40 Lakini Martha dada yake Mariamu alikuwa anashughulisha na shughuli mbalimbali zilizotakiwa kufanywa. Martha aliingia ndani na akasema, “Bwana, hujali kuona mdogo wangu ameniacha nifanye kazi zote peke yangu? Mwambie aje kunisaidia.”
41 Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, unasumbuka na kuhangaika kwa shughuli nyingi. 42 Lakini kitu kimoja tu ndicho cha lazima. Mariamu amefanya uchaguzi sahihi na kamwe hautachukuliwa kutoka kwake.”
© 2017 Bible League International