Old/New Testament
Simulizi Kuhusu Mwana Mpotevu
11 Kisha Yesu akasema, “Alikuwepo mtu mmoja aliyekuwa na wana wawili. 12 Mwana mdogo alimwambia baba yake, ‘Baba, nipe sehemu ya mali ninayotarajia kurithi baadaye.’ Hivyo baba yake akagawa utajiri wake kwa wanawe wawili.
13 Baada ya siku chache yule mdogo akauza mali zake, akachukua pesa zake na akaondoka. Akasafiri mbali katika nchi nyingine. Huko alipoteza pesa zake zote katika starehe na anasa. 14 Baada ya kutumia vyote alivyokuwa navyo, kukatokea njaa kali katika nchi ile yote. Akawa na njaa na mhitaji wa pesa. 15 Hivyo alikwenda kutafuta kazi kwa mwenyeji mmoja wa nchi ile, naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. 16 Alikuwa anasikia njaa kiasi kwamba alikuwa anatamani kula chakula walichokula nguruwe. Lakini hakuna mtu aliyempa chakula.
17 Alipotambua namna alivyokuwa mjinga, akafikiri moyoni mwake na kusema, ‘Wafanyakazi wote wa baba yangu wana chakula kingi. Lakini niko hapa kama niliyekufa kwa sababu sina chakula. 18 Nitaondoka na kurudi kwa baba yangu. Nitamwambia hivi: Baba, nimemtenda Mungu dhambi na nimekukosea wewe. 19 Sistahili kuitwa mwanao tena. Lakini niruhusu niwe kama mmoja wa wafanyakazi wako.’ 20 Hivyo akaondoka na kurudi kwa baba yake.
Alipokuwa mbali na nyumbani kwao, baba yake alimwona, akamwonea huruma. Akamkimbilia, akamkumbatia na kumbusu sana. 21 Mwanaye akasema, ‘Baba, nimemtenda Mungu dhambi na nimekukosea wewe; sistahili kuitwa mwanao tena.’
22 Lakini baba akawaambia watumishi wake, ‘Fanyeni haraka, leteni vazi maalumu, mvikeni. Pia, mvisheni viatu vizuri na pete kwenye kidole chake. 23 Na leteni ndama aliyenona, mchinjeni ili tule na kusherehekea. 24 Kwa sababu mwanangu alikuwa amekufa, lakini sasa yuko hai tena! Alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’ Wakaanza kusherehekea.
25 Mwanaye mkubwa alikuwa shambani. Alipoikaribia nyumba, alisikia sauti za muziki na kucheza. 26 Akaita mmoja wa watumishi na akamwuliza, ‘Kuna nini?’ 27 Mtumishi akasema, ‘Mdogo wako amerudi, na baba yako amechinja ndama aliyenona. Anafurahi kwa sababu amempata mwanaye akiwa salama na mzima.’
28 Mwana mkubwa alikasirika na hakutaka kwenda kwenye sherehe. Hivyo baba yake akatoka nje kumsihi. 29 Lakini alimwambia baba yake, ‘Tazama, miaka yote hii nimekutumikia kama mtumishi, kamwe sijaacha kukutii! Lakini hujawahi kunipa hata mbuzi mdogo ili nisherehekee pamoja na rafiki zangu. 30 Lakini alipokuja huyu mwanao aliyepoteza mali zako kwa makahaba, umemchinjia ndama aliyenona!’
31 Baba yake akamwambia, ‘Mwanangu, daima umekuwa pamoja nami, na vyote nilivyo navyo ni vyako. 32 Lakini tulipaswa kusherehekea. Mdogo wako alikuwa amekufa, lakini sasa ni hai tena. Alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’”
© 2017 Bible League International