Old/New Testament
Viongozi Wawa na Mashaka Kuhusu Mamlaka ya Yesu
(Mt 21:23-27; Mk 11:27-33)
20 Siku moja Yesu alikuwa anawafundisha watu katika eneo la Hekalu. Alikuwa anawahubiri Habari njema. Viongozi wa makuhani, walimu wa sheria, na viongozi wazee wa Kiyahudi walikwenda kuzungumza na Yesu. 2 Wakamwambia, “Tuambie, una mamlaka gani kutenda mambo haya! Ni nani aliyekupa mamlaka hii?”
3 Yesu akawajibu, “Nami nitawauliza swali pia. Niambieni: 4 Yohana alipobatiza watu, mamlaka yake ilitoka kwa Mungu au kwa watu fulani?”
5 Makuhani, walimu wa sheria na viongozi wa Kiyahudi wakajadiliana kwa pamoja kuhusu hili. Wakasema, “Kama tukijibu ‘Ubatizo wa Yohana ulitoka kwa Mungu,’ atasema, ‘Sasa kwa nini hamkumwamini Yohana?’ 6 Lakini kama tukisema ulitoka kwa watu fulani, watu hawa watatupiga kwa mawe mpaka tufe. Kwa sababu wote wanaamini Yohana alikuwa nabii.” 7 Hivyo wakajibu, “Hatujui.”
8 Ndipo Yesu akawaambia, “Hata mimi sitawaambia ni nani alinipa mamlaka kufanya mambo haya.”
Yesu Atoa Simulizi Kuhusu Shamba la Mzabibu
(Mt 21:33-46; Mk 12:1-12)
9 Yesu akawaambia watu kisa hiki; “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu. Kisha akalikodisha kwa wakulima, kisha akasafiri kwa muda mrefu. 10 Wakati wa kuvuna zabibu ulipofika, alimtuma mmoja wa watumishi wake kwa wakulima wale ili wampe sehemu yake ya zabibu. Lakini wakulima wale walimpiga yule mtumishi na wakamfukuza bila kumpa kitu. 11 Hivyo mtu yule akamtuma mtumishi mwingine. Wakulima walimpiga mtumishi huyu pia, wakamwaibisha na kumfukuza bila kumpa kitu. 12 Hivyo mtu yule akamtuma mtumishi wa tatu. Wakulima wakampiga sana mtumishi huyu na wakamtupa nje ya shamba la mizabibu.
13 Mmiliki wa shamba la mizabibu akasema, ‘Nitafanya nini? Nitamtuma mwanangu mpendwa. Yumkini watamheshimu.’ 14 Lakini wakulima walipomwona mwana wa mwenye shamba, wakajadiliana wakisema, ‘Huyu ni mwana wa mmiliki wa shamba. Shamba hili la mizabibu litakuwa lake. Tukimwua, litakuwa letu.’ 15 Hivyo wakulima wakamtupa mwana wa mmiliki wa shamba nje ya shamba la mizabibu na wakamwua.
Je, mmiliki wa shamba la mizabibu atafanya nini? 16 Atakuja na atawaua wale wakulima, kisha atalikodisha shamba kwa wakulima wengine.”
Watu waliposikia mfano huu, wakasema, “Hili lisije kutokea!” 17 Lakini Yesu akawakazia macho na akasema, “Hivyo basi, Maandiko haya yanamaanisha nini:
‘Jiwe lililokataliwa na wajenzi,
limekuwa jiwe kuu la pembeni?’[a]
18 Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjikavunjika na ikiwa jiwe hilo litaangukia, litakusaga!”
19 Walimu wa sheria na wakuu wa makuhani waliposikia kisa hiki, walijua unawahusu wao. Hivyo walitaka kumkamata Yesu wakati huo huo, lakini waliogopa watu wangewadhuru.
Yesu Ajibu Swali Lenye Mtego
(Mt 22:15-22; Mk 12:13-17)
20 Hivyo viongozi wa Kiyahudi walitafuta namna ya kumtega Yesu. Walituma watu waliojifanya kuwa wenye haki, ili waweze kumnasa ikiwa angesema jambo ambalo wangeweza kutumia kinyume naye. Ikiwa angesema jambo lolote baya, wangemkamata na kumpeleka kwa gavana wa Kirumi, mwenye mamlaka ya kumhukumu na kumwadhibu. 21 Hivyo wale watu wakamwambia Yesu, “Mwalimu, tunafahamu kwamba yale unayosema na kufundisha ni kweli. Haijalishi ni nani anasikiliza, unafundisha sawa kwa watu wote. Daima unafundisha ukweli kuhusu njia ya Mungu. 22 Tuambie, ni sahihi sisi kulipa kodi kwa Kaisari, au si sahihi?”
23 Lakini Yesu alitambua watu hawa walikuwa wanajaribu kumtega. Akawaambia, 24 “Nionesheni sarafu ya fedha,” Kisha akauliza, “Jina na picha katika sarafu hii ni ya nani?”
Wakamjibu, “Ya Kaisari.”
25 Akawaambia, “Basi mpeni Kaisari vilivyo vya Kaisari, na mpeni Mungu vilivyo vya Mungu.”
26 Watu wale wakashangaa jibu lake la hekima. Hawakusema kitu. Hawakuweza kumtega Yesu pale mbele za watu. Hakusema chochote kibaya ambacho wangekitumia ili kumnasa.
© 2017 Bible League International