Old/New Testament
Dhambi na Msamaha
(Mt 18:6-7,21-22; Mk 9:42)
17 Yesu akawaambia wafuasi wake, “Mambo yanayosababisha watu kutenda dhambi yatatokea hakika. Lakini ole wake mtu anayesababisha hili litokee. 2 Ingekuwa vizuri kwa mtu huyo kama jiwe la kusagia lingefungwa shingoni mwake, na akatupwa baharini, kuliko kusababisha mmojawapo wa wanyenyekevu hawa kutenda dhambi. 3 Hivyo iweni waangalifu!
Ikiwa ndugu au dada yako katika familia ya Mungu akikukosea, umwonye. Akitubu, msamehe. 4 Hata kama akikukosea mara saba katika siku moja, lakini akakuomba msamaha kila anapokukosea, msamehe.”
Imani Yako Ni Kubwa Kiasi Gani?
5 Kisha mitume wakamwambia Bwana, “Tuongezee imani.”
6 Bwana akasema, “Imani yenu ingekuwa kubwa kama mbegu ya haradali, mngeuambia mforosadi huu, ‘Ng'oka, ukajipandikize baharini,’ nao ungewatii.
Iweni Watumishi Wema
7 Chukulia mmoja wenu ana mtumishi ambaye amekuwa shambani akilima au akichunga kondoo shambani. Akirudi kutoka shambani au machungani, utamwambia nini? Je, utamwambia, ‘Njoo ndani, keti, ule chakula’? 8 Hapana! Utamwambia mtumishi wako, ‘Nitayarishie chakula nile. Jitayarishe na unihudumie. Nitakapomaliza kula na kunywa, ndipo utakula.’ 9 Mtumishi asipewe shukrani maalumu kwa kufanya kazi yake. Anafanya kile alichoagizwa na mkuu wake. 10 Vivyo hivyo nanyi. Mkimaliza kufanya yote mliyoamriwa kufanya, mseme, ‘Sisi ni watumwa, hatustahili shukrani yoyote maalumu. Tumefanya kazi tunayotakiwa kufanya.’”
Yesu Awaponya Baadhi ya Wayahudi na Msamaria
11 Yesu alikuwa anasafiri kwenda Yerusalemu. Alipotoka Galilaya alisafiri akipita kando ya mpaka wa Samaria. 12 Aliingia katika mji mdogo, na wanaume kumi walimwendea. Hawakumkaribia, kwa sababu wote walikuwa na ugonjwa mbaya sana wa ngozi. 13 Lakini watu wale wakaita kwa kupaza sauti wakisema, “Yesu! Mkuu! Tafadhali utusaidie!”
14 Yesu alipowaona, akasema, “Nendeni mkajioneshe kwa makuhani.”[a]
Wale watu kumi walipokuwa wanakwenda kujionesha kwa makuhani, waliponywa. 15 Mmoja wao alipoona kuwa amepona, alirudi kwa Yesu huku akimsifu Mungu kwa kupaza sauti. 16 Akaanguka kifudifudi miguuni pa Yesu, akamshukuru. (Alikuwa Msamaria.) 17 Yesu akasema, “Watu kumi wameponywa, wengine tisa wako wapi? 18 Mtu huyu wala si mmoja wa watu wetu. Ni yeye peke yake aliyerudi kumsifu Mungu?” 19 Ndipo Yesu akamwambia, “Inuka! Unaweza kwenda. Umeponywa kwa sababu uliamini.”
© 2017 Bible League International