Old/New Testament
Yesu Amweka Huru Mvulana Kutoka Pepo Mchafu
(Mt 17:14-18; Mk 9:14-27)
37 Siku iliyofuata, Yesu, Petro, Yohana na Yakobo walitelemka kutoka mlimani. Kundi kubwa la watu likaenda kukutana naye. 38 Mtu mmoja katika umati huo alimwita Yesu akisema, “Mwalimu, tafadhali njoo umwonee mwanangu. Ni mtoto pekee niliye naye. 39 Pepo mchafu humvaa na hupiga kelele, humtia kifafa na kumtoa povu mdomoni. Huendelea kumwumiza na hamwachi kirahisi. 40 Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe pepo huyu mchafu lakini wameshindwa.”
41 Yesu akajibu, “Enyi watu msio na imani. Maisha yenu ni mabaya. Nitakaa na kuchukuliana nanyi mpaka lini?” Ndipo Yesu akamwambia yule mtu, “Mlete kijana wako hapa.”
42 Kijana alipokuwa anakwenda kwa Yesu, pepo mchafu akamwangusha chini na kumtia kifafa. Lakini Yesu akamwamuru atoke. Kijana akaponywa, na Yesu akampeleka kwa baba yake. 43 Watu wote wakaushangaa ukuu wa nguvu ya Mungu.
Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake
(Mt 17:22-23; Mk 9:30-32)
Watu walipokuwa bado wanayashangaa mambo yote aliyofanya Yesu. Akawaambia wanafunzi wake, 44 “Msiyasahau nitakayowaambia sasa: Mwana wa Adamu yu karibu kukamatwa na kuwekwa katika mikono ya watu wengine.” 45 Lakini wanafunzi hawakuelewa alichomaanisha. Maana ilifichwa kwao ili wasitambue. Lakini waliogopa kumwuliza Yesu kuhusiana na alilosema.
Nani ni Mkuu Zaidi?
(Mt 18:1-5; Mk 9:33-37)
46 Wafuasi wa Yesu walianza kubishana wakiulizana nani ni mkuu kuliko wote miongoni mwao. 47 Yesu alijua walichokuwa wanafikiri, hivyo akamchukua mtoto mdogo na kumsimamisha karibu yake. 48 Kisha akawaambia, “Yeyote anayemkaribisha mtoto mdogo kama huyu kwa jina langu ananikaribisha mimi. Na yeyote anayenikaribisha mimi anamkaribisha yule aliyenituma. Aliye mnyenyekevu zaidi miongoni mwenu, ndiye mkuu.”
Asiye Kinyume Nanyi ni Mmoja Wenu
(Mk 9:38-40)
49 Yohana akajibu; “Bwana mkubwa, tuliona mtu anatoa pepo kutoka kwa watu akitumia jina lako. Tulimwambia aache kwa sababu hayuko katika kundi letu.”
50 Yesu akamwambia, “Msimkataze. Asiye kinyume nanyi yu pamoja nanyi.”
Katika Mji wa Samaria
51 Wakati ulikuwa unakaribia ambapo Yesu alikuwa aondoke na kurudi mbinguni. Hivyo aliamua kwenda Yerusalemu. 52 Alituma baadhi ya watu kumtangulia. Waliondoka na kwenda katika mji mmoja wa Samaria, ili kumwandalia mahali pa kufikia. 53 Lakini watu katika mji huo hawakumkaribisha Yesu kwa sababu alikuwa anakwenda Yerusalemu. 54 Wafuasi wake; Yakobo na Yohana walipoona hayo, wakasema, “Bwana, unataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni na kuwateketeza watu hawa?”[a]
55 Lakini Yesu aligeuka na akawakemea baada ya wao kusema hivi.[b] 56 Kisha Yesu na wanafunzi wake wakaondoka wakaenda katika mji mwingine.
Kumfuata Yesu
(Mt 8:19-22)
57 Walipokuwa wakisafiri pamoja njiani, mtu mmoja akamwambia Yesu, “Nitakufuata kokote utakakokwenda.”
58 Yesu akamwambia, “Mbweha wana mapango na ndege wa angani wana viota. Lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”
59 Yesu akamwambia mtu mwingine, “Nifuate!”
Lakini mtu yule akamwambia, “Bwana, niache nikamzike baba yangu kwanza.”
60 Lakini Yesu akamwambia, “Waache waliokufa wawazike wafu wao. Ni lazima uende kuhubiri kuhusu Ufalme wa Mungu.”
61 Mtu mwingine pia akamwambia, “Nitakufuata Bwana, lakini niruhusu kwanza nikaiage familia yangu.”
62 Yesu akamwambia, “Mtu yeyote anayeanza kulima, kisha akaangalia nyuma hajajiandaa kwa ajili ya Ufalme wa Mungu.”
© 2017 Bible League International