Old/New Testament
Msitumainie Fedha
32 Msiogope, enyi kundi dogo. Kwa kuwa imempendeza Baba yenu kuwapa ninyi ufalme wake. 33 Uzeni vitu mlivyo navyo, wapeni fedha wale wanaohitaji. Hii ni njia pekee mnayoweza kufanya utajiri wenu usipotee. Mtakuwa mnaweka hazina isiyoisha mbinguni, mahali ambapo wezi hawawezi kuiba na hakuna wadudu wa kuharibu. 34 Kwa kuwa mahali ilipo hazina yako, ndipo roho yako itakapokuwa.
Iweni Tayari Daima
(Mt 24:42-44)
35 Iweni tayari! Vaeni kikamilifu na taa zenu zikiwaka. 36 Iweni tayari kama watumishi wanaomngojea bwana wao anayerudi kutoka kwenye sherehe ya harusi. Bwana wao anaporudi na kubisha mlangoni, watumishi huweza kumfungulia mlango haraka. 37 Bwana wao atakapoona kuwa wako tayari na wanamsubiri, itakuwa siku ya furaha kwa watumishi hao. Ninawaambia bila mashaka, bwana wao atavaa nguo, atawakaribisha kwenye chakula kisha atawahudumia. 38 Watumishi hao wanaweza kumsubiri bwana wao mpaka usiku wa manane. Lakini watafurahi sana kwa sababu aliporudi aliwakuta bado wanamsubiri.
39 Mwenye nyumba angefanya nini ikiwa angejua ni lini mwizi atakuja? Mnajua kuwa asingeruhusu mwizi akavunja na kuingia ndani. 40 Hivyo, iweni tayari ninyi nanyi, kwa kuwa Mwana wa Adamu atakuja wakati msiotarajia!”
Mtumwa Mwaminifu ni Yupi?
(Mt 24:45-51)
41 Petro akasema, “Bwana, mfano ule ulikuwa kwa ajili yetu au kwa ajili ya watu wote?”
42 Bwana akamjibu, “Fikiria kuhusu mtumishi mwenye hekima na mwaminifu, ambaye bwana wake anamwamini na kumweka kuwa msimamizi wa kuwapa watumishi wengine chakula kwa wakati uliokubalika? Mtumishi huyo ataoneshaje kuwa yeye ni msimamizi makini na anayeweza kujisimamia? 43 Mkuu[a] wake atakaporudi na kumkuta akifanya kazi aliyompa, siku hiyo itakuwa siku ya furaha sana kwa mtumishi huyo. 44 Ninawaambia ukweli bila mashaka yo yote, mkuu wake atamweka kuwa msimamizi wa vitu vyake vyote anavyomiliki.
45 Lakini itakuwaje ikiwa mtumishi huyo ni mwovu na akadhani bwana wake hatarudi mapema? Ataanza kuwapiga watumishi wengine, wanaume na wanawake. Atakula na kunywa mpaka atalewa. 46 Ndipo bwana wa mtumishi huyo atakuja wakati usiotarajiwa, wakati ambapo mtumishi hajajiandaa. Ataadhibiwa bila huruma[b] na bwana wake na kumpeleka anakostahili, mahali waliko watumishi wengine wasiotii.
47 Mtumishi huyo alijua kitu ambacho bwana wake alimtaka afanye. Lakini hakuwa tayari kufanya au kujaribu kufanya kile bwana wake alichotaka. Hivyo mtumishi huyo ataadhibiwa sana! 48 Lakini vipi kuhusu mtumishi asiyejua kile ambacho bwana wake anataka? Yeye pia anafanya mambo yanayostahili adhabu, lakini ataadhibiwa kidogo kuliko mtumishi aliyejua alichotakiwa kufanya. Yeyote aliyepewa vingi atawajibika kwa vingi. Hivyo vingi vitategemewa kutoka kwa yule aliyepewa vingi zaidi.”
Kumfuata Yesu Kunaleta Matatizo
(Mt 10:34-36)
49 Yesu aliendelea kusema: “Nimekuja kuleta moto ulimwenguni. Ninatamani ungekuwa unawaka tayari! 50 Kuna aina ya ubatizo[c] ambao ni lazima niupitie na niteseke. Ninajisikia kusumbuka mpaka pale utakapotimizwa. 51 Mnadhani nilikuja kuleta amani ulimwenguni? Hapana, nilikuja kuugawa ulimwengu! 52 Kuanzia sasa, familia ya watu watano itagawanyika, watatu watakuwa kinyume cha wawili, na wawili kinyume cha watatu.
53 Kina baba watakuwa kinyume cha wana wao:
na wana nao watakuwa kinyume cha baba zao.
Kina mama watakuwa kinyume cha binti zao:
na binti nao watakuwa kinyume cha mama zao.
Mama wakwe watakuwa kinyume cha wake za wana wao,
na wake za wana wao watakuwa kinyume cha mama wakwe zao.”[d]
Kuzielewa Nyakati
(Mt 16:2-3)
54 Ndipo Yesu akawaambia watu, “Mnapoona wingu likikua upande wa magharibi, mnasema, ‘Mvua inakuja,’ na muda si mrefu huanza kunyesha. 55 Mnapoona upepo unaanza kuvuma kutoka kusini mnasema, ‘Kutakuwa joto,’ na huwa hivyo. 56 Enyi wanafiki! Mnaweza kuiona nchi na anga na mkajua hali ya hewa itakavyokuwa. Kwa nini hamwelewi kinachotokea sasa?
Malizeni Matatizo Yenu
(Mt 5:25-26)
57 Kwa nini ninyi wenyewe hamwezi kujiamulia ninyi wenyewe kilicho haki? 58 Ikiwa mtu anakushtaki na ninyi nyote mnaongozana kwenda mahakamani. Jitahidi kadri inavyowezekana kupatana naye mkiwa njiani. Usipopatana naye, atakupeleka kwa hakimu. Na hakimu atakutia hatiani na maofisa wa mahakama watakutupa gerezani. 59 Ninawaambieni, hautatoka humo, mpaka ulipe kila senti unayodaiwa.”
© 2017 Bible League International