Old/New Testament
Mjane Aonesha Jinsi Ulivyo Utoaji wa Kweli
(Mk 12:41-44)
21 Yesu alitazama na kuwaona matajiri wakimtolea Mungu sadaka zao katika sanduku la sadaka ndani ya Hekalu. 2 Kisha akamwona mjane maskini akiweka sarafu mbili za shaba kwenye sanduku. 3 Akasema, “Mjane huyu maskini ametoa sarafu mbili tu. Lakini ukweli ni kuwa, ametoa zaidi ya hao matajiri wote. 4 Wale wanavyo vingi, na wametoa vile ambavyo hawavihitaji. Lakini mwanamke huyu ni maskini sana, lakini ametoa vyote alivyokuwa akitegemea ili aishi.”
Yesu Aonya Kuhusu Wakati Ujao
(Mt 24:1-14; Mk 13:1-13)
5 Baadhi ya watu walikuwa wanazungumza kuhusu uzuri wa Hekalu lililojengwa kwa mawe safi na kupambwa kutokana na matoleo mbalimbali ambayo watu humtolea Mungu ili kutimiza nadhili zao.
6 Lakini Yesu akasema, “Wakati utafika ambao yote mnayoyaona hapa yatateketezwa. Kila jiwe katika majengo haya litatupwa chini. Hakuna jiwe litakaloachwa juu ya jingine.”
7 Baadhi ya watu wakamwuliza Yesu, “Mwalimu, mambo hayo yatakuwa lini? Dalili ipi itatuonyesha kwamba ni wakati wa mambo haya kutokea?”
8 Yesu akasema, “Iweni waangalifu, msije mkarubuniwa. Watu wengi watakuja wakitumia jina langu, watasema, ‘Mimi ndiye Masihi,’[a] na ‘Wakati sahihi umefika!’ Lakini msiwafuate. 9 Mtakaposikia kuhusu vita na machafuko, msiogope. Mambo haya lazima yatokee kwanza. Lakini mwisho hautakuja haraka.”
10 Kisha Yesu akawaambia, “Mataifa yatapigana na mataifa mengine. Falme zitapigana na falme zingine. 11 Kutakuwa matetemeko makubwa, kutakuwa njaa na magonjwa ya kutisha sehemu nyingi. Mambo ya kutisha yatatokea, na mambo ya kushangaza yatatokea kutoka mbinguni ili kuwaonya watu.
12 Lakini kabla ya mambo haya yote kutokea, watu watawakamata ninyi na kuwatesa. Watawahukumu katika masinagogi yao na kuwafunga gerezani. Mtalazimishwa kusimama mbele ya wafalme na magavana. Watawatendea mambo haya yote kwa sababu ninyi ni wafuasi wangu. 13 Lakini hili litawapa ninyi fursa ya kuhubiri juu yangu. 14 Msihofu namna mtakavyojitetea, 15 Nitawapa hekima kusema mambo ambayo adui zenu watashindwa kuyajibu. 16 Hata wazazi wenu, ndugu zenu, jamaa, na marafiki watawageuka. Watawaua baadhi yenu. 17 Kila mtu atawachukia kwa sababu mnanifuata mimi. 18 Lakini hakuna hata unywele mmoja wa vichwa vyenu utakaopotea. 19 Mtayaokoa maisha yenu ikiwa mtaendelea kuwa imara katika imani mnapopita katika mambo haya yote.
© 2017 Bible League International