Old/New Testament
Mungu Atawajibu Watu Wake
18 Kisha Yesu akawafundisha wafuasi wake kwamba wanapaswa kuomba daima bila kupoteza tumaini. Akatumia simulizi hii kuwafundisha. 2 Akasema, “Kulikuwa na mwamuzi katika mji fulani. Hakumcha Mungu wala hakujali watu walikuwa wanamfikiriaje. 3 Na katika mji huo huo alikuwepo mwanamke mjane. Huyu alimjia mwamuzi huyu mara nyingi akimwambia, ‘Kuna mtu anayenitendea mambo mabaya. Nipe haki yangu!’ 4 Mwanzoni mwamuzi hakutaka kumsaidia yule mwanamke. Lakini baada ya muda kupita, akawaza moyoni mwake yeye mwenyewe, ‘Simchi Mungu. Na sijali watu wananifikiriaje. 5 Lakini mwanamke huyu ananisumbua. Nikimpa haki yake ataacha kunisumbua. Nisipomsaidia, ataendelea kunijia na anaweza kunishambulia.’”
6 Bwana akasema, “Sikilizeni, maneno aliyosema mwamuzi mbaya yana mafundisho kwa ajili yenu. 7 Daima Mungu atawapa mahitaji yao wateule wanaomwomba usiku na mchana. Hatachelewa kuwajibu. 8 Ninawaambia, Mungu atawapa haki yao watu wake haraka. Lakini Mwana wa Adamu atakaporudi, atawakuta duniani watu ambao bado wanamwamini?”
Farisayo na Mtoza Ushuru
9 Walikuwepo baadhi ya watu waliojiona kuwa wenye haki na waliwadharau wengine. Yesu alitumia simulizi hii kuwafundisha: 10 “Siku moja Farisayo na mtoza ushuru walikwenda Hekaluni kuomba. 11 Farisayo alisimama peke yake mbali na mtoza ushuru. Farisayo aliomba akisema, ‘Ee Mungu, ninakushukuru kwa kuwa mimi si mwovu kama watu wengine. Mimi siyo kama wezi, waongo au wazinzi. Ninakushukuru kwa kuwa mimi ni bora kuliko huyu mtoza ushuru. 12 Ninafunga mara mbili kwa wiki na kutoa sehemu ya kumi ya vyote ninavyopata!’
13 Mtoza ushuru alisimama peke yake pia. Lakini alipoanza kuomba, hakuthubutu hata kutazama juu mbinguni. Alijipigapiga kifua chake akijinyenyekeza mbele za Mungu. Akasema, ‘Ee Mungu, unihurumie, mimi ni mwenye dhambi.’ 14 Ninawaambia, mtu huyu alipomaliza kuomba na kwenda nyumbani, alikuwa amepatana na Mungu. Lakini Farisayo, aliyejisikia kuwa bora kuliko wengine, hakuwa amepatana na Mungu. Watu wanaojikweza watashushwa. Lakini wale wanaojishusha watakwezwa.”
Yesu Awakaribisha Watoto
(Mt 19:13-15; Mk 10:13-16)
15 Baadhi ya watu waliwaleta hata watoto wao wadogo kwa Yesu ili awawekee mikono kuwabariki. Lakini wafuasi walipoona hili, waliwakataza. 16 Lakini Yesu aliwaalika watoto kwake na kuwaambia wafuasi wake, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu. Msiwazuie, kwa kuwa ufalme wa Mungu ni wa watu walio kama watoto wadogo hawa. 17 Ukweli ni kwamba, ni lazima uupokee ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo anavyopokea vitu, la si hivyo hautauingia.”
Mtu Tajiri Akataa Kumfuata Yesu
(Mt 19:16-30; Mk 10:17-31)
18 Kiongozi wa dini akamuuliza Yesu, “Mwalimu Mwema, ni lazima nifanye nini ili niweze kuupata uzima wa milele?”
19 Yesu akamwambia, “Kwa nini unaniita mwema? Mungu peke yake ndiye mwema. 20 Na unazijua amri zake: ‘Usizini, usiue, usiibe, usiseme uongo, na ni lazima uwaheshimu baba na mama yako.’”(A)
21 Lakini yule kiongozi akasema, “Nimezitii amri zote hizi tangu nilipokuwa mdogo.”
22 Yesu aliposikia hili, akamwambia, “Lakini kuna jambo moja unatakiwa kufanya. Uza kila kitu ulichonacho na uwape maskini pesa. Utakuwa na utajiri mbinguni. Kisha, njoo unifuate.” 23 Lakini yule mtu aliposikia Yesu anamwambia kutoa pesa zake, alihuzunika. Hakutaka kufanya hivi kwa sababu alikuwa tajiri sana.
© 2017 Bible League International