Old/New Testament
Baadhi ya Masadukayo Wajaribu Kumtega Yesu
(Mt 22:23-33; Mk 12:18-27)
27 Baadhi ya Masadukayo walimwendea Yesu. (Masadukayo wanaamini watu hawatafufuka kutoka kwa wafu.) Wakamwuliza, 28 “Mwalimu, Musa aliandika kwamba mtu aliyeoa akifa na hakuwa na watoto, kaka au mdogo wake amwoe mjane wake, ili wawe na watoto kwa ajili ya yule aliyekufa.[a] 29 Walikuwepo ndugu saba. Wa kwanza alioa mke lakini akafa bila ya kuwa na watoto. 30 Wa pili akamuoa yule mwanamke kisha akafa. 31 Na wa tatu akamwoa mwanamke na akafa. Kitu kile kile kikawatokea ndugu wote saba. Walikufa bila ya kuwa na watoto. 32 Mwanamke akawa wa mwisho kufa. 33 Lakini ndugu wote saba walimwoa. Sasa, watu watakapofufuka kutoka kwa wafu, atakuwa mke wa yupi?”
34 Yesu akawaambia Masadukayo, “Watu huoana katika ulimwengu huu. 35 Baadhi ya watu watastahili kufufuliwa kutoka kwa wafu na kuishi tena katika ulimwengu ujao. Katika maisha yale hawataoa kamwe. 36 Katika maisha hayo, watu watakuwa kama malaika na hawatakufa. Ni watoto wa Mungu, kwa sababu wamefufuliwa kutoka kwa wafu. 37 Musa alionesha dhahiri kwamba watu hufufuliwa kutoka kwa wafu. Alipoandika kuhusu kichaka kilichokuwa kinaungua,[b] alisema kwamba Bwana ni ‘Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo.’(A) 38 Ni Mungu wa wanaoishi tu. Hivyo watu hawa kwa hakika hawakuwa wamekufa. Ndiyo, kwa Mungu watu wote bado wako hai.”
39 Baadhi ya walimu wa sheria wakasema, “Mwalimu, jibu lako ni zuri.” 40 Hakuna hata mmoja aliyekuwa na ujasiri wa kumwuliza swali jingine.
Je, Masihi ni Mwana wa Daudi?
(Mt 22:41-46; Mk 12:35-37)
41 Kisha Yesu akasema, “Kwa nini watu husema kwamba Masihi ni Mwana wa Daudi? 42 Katika kitabu cha Zaburi, Daudi mwenyewe anasema,
‘Bwana Mungu alimwambia Bwana wangu:
Keti karibu nami upande wangu wa kulia,
43 na nitawaweka adui zako chini ya mamlaka yako.’[c](B)
44 Hivyo ikiwa Daudi anamwita Masihi, ‘Bwana’. Inawezekanaje Masihi awe mwana wa Daudi?”
Tahadhali Juu ya Walimu wa Sheria
(Mt 23:1-36; Mk 12:38-40; Lk 11:37-54)
45 Watu wote walipokuwa wanamsikiliza Yesu, akawaambia wafuasi wake, 46 “Iweni waangalifu dhidi ya walimu wa sheria. Wanapenda kutembea wakiwa wamevaa mavazi yanayoonekana ya heshima. Na wanapenda pale watu wanapowasalimu kwa heshima maeneo ya masoko. Wanapenda kukaa sehemu za heshima katika masinagogi na sehemu za watu maarufu katika sherehe. 47 Lakini huwalaghai wajane na kuchukua nyumba zao. Kisha kujionesha kuwa waongofu wa mioyo kuomba sala ndefu. Mungu atawaadhibu kwa hukumu kuu.”
© 2017 Bible League International