Add parallel Print Page Options

Yesu Awakosoa Viongozi wa Kidini

(Mk 12:38-40; Lk 11:37-52; 20:45-47)

23 Kisha Yesu akazungumza na watu pamoja na wafuasi wake, akasema, “Walimu wa sheria na Mafarisayo wana mamlaka ya kuwaambia Sheria ya Musa inasema nini. Hivyo mnapaswa kuwatii. Fanyeni kila wanachowaambia. Lakini maisha yao sio mfano mzuri wa kuufuata. Hawatendi wale wanayofundisha. Hutengeneza orodha ndefu ya kanuni na kujaribu kuwalazimisha watu kuzifuata. Lakini sheria hizi ni kama mizigo mizito ambayo watu hawawezi kuibeba, na viongozi hawa hawatazirahisisha kupunguza mzigo kwa watu.

Wao wanatenda mambo mema tu ili waonwe na watu wengine. Hufanya visanduku vidogo vya Maandiko[a] wanavyovaa kuwa vikubwa zaidi. Hufanya mashada ya urembo[b] kwenye mavazi yao ya nje kuwa marefu zaidi ili waonwe na watu. Watu hawa wanapenda kukaa sehemu za heshima kwenye sherehe na kwenye viti muhimu zaidi katika masinagogi. Wanapenda kuitwa ‘Mwalimu’ Na kusalimiwa kwa heshima na watu kwenye masoko.

Ninyi nyote ni ndugu, dada na kaka kwa sababu mnaye mwalimu mmoja tu. Hivyo msikubali kuitwa ‘Mwalimu’. Nanyi msimwite mtu yeyote duniani ‘Baba’, maana mnaye Baba mmoja tu, naye yuko mbinguni. 10 Msikubali kuitwa ‘Mwalimu’, kwa sababu mnaye Mwalimu mmoja tu, naye ni Masihi. 11 Kila atakayetumika kama mtumishi ndiyo mkuu zaidi kati yenu. 12 Wanaojifanya kuwa bora kuliko wengine watanyenyekezwa kwa lazima. Lakini watu wanaojinyenyekeza wenyewe watafanywa kuwa wakuu.

13 Ole wenu[c] walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnawafungia watu njia ya kuingia katika ufalme wa Mungu, kwa kuwa ninyi wenyewe hamwingii na mnawazuia wale wanaojaribu kuingia. 14 [d]

15 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki. Mnasafiri kuvuka bahari na nchi nyingine ili kumtafuta mtu mmoja atakayefuata njia zenu. Mnapompata mtu huyo, mnamfanya astahili maradufu kwenda Jehanamu kama ninyi mlivyo!

16 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Mnawaongoza watu lakini ninyi wenyewe ni wasiyeona. Mnasema, ‘Mtu yeyote akiweka kiapo au nadhiri kwa jina la Hekalu, haimaanishi kitu. Lakini yeyote atakayeweka kiapo kwa kutumia dhahabu iliyo Hekaluni lazima atimize nadhiri au kiapo hicho.’ 17 Ninyi ni wasiyeona mlio wajinga! Hamwoni kuwa Hekalu ni kuu kuliko dhahabu iliyo ndani yake? Hekalu ndilo huifanya dhahabu kuwa takatifu!

18 Na mnasema, ‘Mtu yeyote akitumia madhabahu kuweka nadhiri au kiapo, haina maana yeyote. Lakini kila anayetumia sadaka iliyo kwenye madhabahu na kuapa au kuweka nadhiri, lazima atimize nadhiri au kiapo hicho.’ 19 Ninyi ni wasiyeona! Hamwoni kuwa madhabahu ni kuu kuliko sadaka yo yote iliyo juu yake? Madhabahu ndiyo inaifanya sadaka kuwa takatifu! 20 Kila anayeitumia madhabahu kuapa au kuweka nadhiri ni dhahiri anatumia madhabahu na kila kitu kilicho juu yake. 21 Na kila anayetumia Hekalu kuapa au kuweka nadhiri kwa hakika analitumia Hekalu na Mungu, anayeishi ndani humo. 22 Kila anayetumia mbingu kuapa au kuweka nadhiri anakitumia kiti cha enzi cha Mungu na yule aketiye juu yake.

23 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnampa Mungu sehemu ya kumi ya chakula mnachopata,[e] hata mnanaa, binzari na jira.[f] Lakini hamtii mambo ya muhimu katika mafundisho ya sheria; kuishi kwa haki, kuwa wenye huruma, na kuwa waaminifu. Haya ndiyo mambo mnayopaswa kufanya. Na mwendelee pia kufanya mambo hayo mengine. 24 Mnawaongoza watu lakini ninyi wenyewe ni wasiyeona![g] Ninyi ni kama mtu anayemtoa nzi katika kinywa chake na kisha anammeza ngamia!

25 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnaosha vikombe na sahani zenu kwa nje. Lakini ndani yake vimejaa vitu mlivyopata kwa kuwadang'anya wengine na kujifurahisha ninyi wenyewe. 26 Mafarisayo, ninyi ni wasiyeona! Safisheni kwanza vikombe kwa ndani ili viwe safi. Ndipo vikombe hivyo vitakuwa safi hata kwa nje.

27 Ole wenu walimu wa sheria na ninyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Ninyi ni kama makaburi yaliyopakwa rangi nyeupe, lakini ndani yake yamejaa mifupa ya wafu na kila aina ya uchafu. 28 Ndivyo ilivyo hata kwenu. Watu wanawatazama na kudhani kuwa ninyi ni wenye haki, lakini mmejaa unafiki na uovu ndani yenu.

29 Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii, na kuyaheshimu makaburi ya wenye haki waliouawa. 30 Na mnasema, ‘Ikiwa tungeishi nyakati za mababu zetu, tusingewasaidia kuwaua manabii hawa.’ 31 Hivyo mnathibitisha kuwa ninyi ni uzao wa wale waliowaua manabii. 32 Na mtaimalizia dhambi waliyoianza mababu zenu!

33 Enyi nyoka! Ninyi mlio wa uzao wa nyoka wenye sumu kali! Hamtaikwepa adhabu. Mtahukumiwa na kutupwa Jehanamu! 34 Hivyo ninawaambia: Ninawatuma manabii na walimu wenye hekima na wanaojua Maandiko. Lakini mtawaua, mtawatundika baadhi yao kwenye misalaba na kuwapiga wengine katika masinagogi yenu. Mtawafukuza kutoka katika mji mmoja hadi mwingine.

35 Hivyo mtakuwa na hatia kutokana vifo vyote vya watu wema wote waliouawa duniani. Mtakuwa na hatia kwa kumwua mtu wa haki Habili, na mtakuwa na hatia kwa kuuawa kwa Zakaria[h] mwana wa Barakia mliyemwua kati ya Hekalu na madhabahu. Mtakuwa na hatia ya kuwaua watu wote wema walioishi kati ya wakati wa Habili mpaka wakati wa Zakaria. 36 Niaminini ninapowaambia kuwa mambo haya yote yatawapata ninyi watu mnaoishi sasa.

Read full chapter

Footnotes

  1. 23:5 visanduku vidogo vya Maandiko Visanduku vidogo vya ngozi vyenye Maandiko manne muhimu. Baadhi ya Wayahudi walivifunga visanduku hivi kwenye vipaji vya nyuso zao na mkono wa kushoto kuonesha kumpenda au uaminifu wao kwa Mungu na Neno lake. Mafarisayo wengi walitengeneza visanduku hivi vikubwa kuliko vya wengine kuonesha kuwa wao ni watu wa dini kuliko watu wengine.
  2. 23:5 mashada ya urembo Urembo uliotengenezwa kwa nyuzi za sufu au manyoya ya kondoo zinazotambaa mpaka chini kutoka pembe nne za vazi la kusalia au vazi la maombi lililovaliwa na Wayahudi. Urembo huu ulipaswa kuwa ukumbusho wa amri za Mungu (tazama Hes 15:38-41).
  3. 23:13 Ole wenu Ama Itakuwa vibaya kwenu enyi walimu wa sheria na Mafarisayo.
  4. 23:14 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza mstari wa 14: “Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo. Ninyi ni wanafiki. Mnawadanganya wajane na kuchukua nyumba zao. Kisha mnafanya maombi marefu ili watu wawaone. Mtapata adhabu mbaya zaidi.” Tazama Mk 12:40; Lk 20:47.
  5. 23:23 Mnampa Mungu … mnachopata Sheria ya Musa iliwataka Waisraeli kumtolea Mungu sehemu ya kumi ya mazao yao (tazama Law 27:30-32; Kum 26:12).
  6. 23:23 mnanaa, binzari na jira Haya ni mazao yaliyotolewa malipo ya fungu la kumi. Lakini sheria ya Musa halikujumuisha mazao madogo kama haya yaliyotajwa hapa. Bali Mafarisayo walikuwa wanatoa zaidi ili kuwa na uhakika kuwa hawavunji Sheria.
  7. 23:24 lakini ninyi wenyewe ni wasiyeona Hii ina maana kuwa “Mnajishughulisha kwa mambo madogo sana lakini mnatenda dhambi kubwa.”
  8. 23:35 Habili, Zakaria Katika Agano la Kale la Kiebrania, hawa ni watu wa kwanza na wa mwisho kuuawa. Tazama Mwa 4:8-11 na 2 Nya 24:20-25.