Old/New Testament
Yesu Aingia Yerusalemu Kama Mfalme
(Mt 21:1-11; Mk 11:1-11; Yh 12:12-19)
28 Baada ya Yesu kusema mambo haya, aliendelea kusafiri kuelekea Yerusalemu. 29 Akakaribia Bethfage na Bethania, miji iliyo karibu na kilima kinachoitwa Mlima wa Mizeituni. Kisha akawatuma wawili miongoni mwa wafuasi wake, 30 akawaambia, “Nendeni kwenye mji mnaoweza kuuona pale. Mtakapoingia mjini, mtamwona mwanapunda amefungwa ambaye bado mtu yeyote hajampanda. Mfungueni na mleteni hapa kwangu. 31 Kama mtu yeyote akiwauliza, ‘Kwa nini mnamfungua?’ Semeni, ‘Bwana anamhitaji.’”
32 Wafuasi wawili wakaenda kwenye mji ule. Wakamwona punda kama Yesu alivyowaambia. 33 Wakamfungua, lakini wamiliki wa punda wakatoka. Wakawauliza wafuasi wa Yesu, “Kwa nini mnamfungua punda wetu?”
34 Wafuasi wakajibu, “Bwana anamhitaji.” 35 Hivyo wafuasi wakampeleka punda kwa Yesu. Wakatandika baadhi ya nguo zao juu ya mwanapunda, kisha wakampandisha Yesu juu yake. 36 Yesu akaanza kwenda Yerusalemu. Wafuasi walikuwa wanatandaza nguo zao njiani mbele yake.
37 Yesu alipokaribia Yerusalemu. Alipokuwa katika njia inayotelemka kutoka kwenye Mlima wa Mizeituni, kundi lote la wafuasi wake wakaanza kumsifu Mungu kwa kupaza sauti. Walimsifu Mungu kwa furaha kwa sababu ya miujiza yote waliyoiona. 38 Walisema,
“Karibu! Mungu ambariki mfalme
ajaye kwa jina la Bwana!(A)
Amani iwe mbinguni,
na utukufu kwa Mungu!”
39 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika kundi wakamwambia Yesu, “Mwalimu, waambie wafuasi wako wasiseme mambo haya!”
40 Lakini Yesu akawajibu, “Ninawaambia ikiwa wafuasi wangu wasingesema, mawe haya yangesema kwa kupaza sauti!”
Yesu Aulilia Mji wa Yerusalemu
41 Yesu alipoukaribia mji wa Yerusalemu, akautazama kisha akaanza kuulilia, 42 akisema, “Laiti ungelijua leo kile kinachokuletea amani. Lakini kimefichwa kwako usikijue sasa. 43 Wakati unakuja, ambao adui zako watajenga ukuta kukuzunguka na kukuzingira pande zote. 44 Watakuteketeza wewe na watu wako wote. Hakuna jiwe hata moja katika majengo yako litaachwa juu ya jiwe jingine. Haya yote yatatokea kwa sababu hukujua wakati ambao Mungu alikuja kukuokoa.”
Yesu Asafisha Eneo la Hekalu
(Mt 21:12-17; Mk 11:15-19; Yh 2:13-22)
45 Yesu aliingia katika eneo la Hekalu. Akaanza kuwafukuza watu waliokuwa wanauza vitu humo. 46 Akasema, “Maandiko yanasema, ‘Hekalu langu litakuwa nyumba ya sala.’(B) Lakini mmeligeuza kuwa ‘maficho ya wezi.’”(C)
47 Yesu aliwafundisha watu kila siku katika eneo la Hekalu. Viongozi wa makuhani, walimu wa sheria na baadhi ya viongozi wa watu walikuwa wakitafuta namna ya kumwua. 48 Lakini hawakujua namna ambavyo wangefanya, kwa sababu alikuwa anazungukwa na watu kila wakati waliokuwa wakimsikiliza. Kila mtu alifurahia yale ambayo Yesu alikuwa anasema, hawakuacha kumsikiliza.
© 2017 Bible League International