Old/New Testament
23 Mtu mmoja akamwuliza, “Bwana, watu wangapi wataokolewa? Ni wachache?”
Yesu akajibu, 24 “Mlango wa kuingia katika ufalme wa Mungu ni mwembamba. Jitahidini kuingia kupitia mlango huo. Watu wengi watataka kuingia huko, lakini hawataweza. 25 Mtu anapoufunga mlango wa nyumba yake, unaweza ukasimama nje na kubisha mlangoni, lakini hataufungua. Mnaweza kusema, ‘Mkuu tufungulie mlango!’ Lakini yeye akawajibu, ‘Siwajui ninyi na mnakotoka sikujui.’ 26 Ndipo mtaanza kusema, ‘Tulikula na kunywa pamoja nawe. Ulifundisha katika mitaa ya mji wetu.’ 27 Kisha atawaambia, ‘Siwajui na sijui mlikotoka! Ondokeni kwangu! Ninyi nyote ni watu mnaotenda maovu!’
28 Mtamwona Ibrahimu, Isaka, Yakobo na manabii wote wakiwa katika ufalme wa Mungu. Lakini ninyi wenyewe mtatupwa nje. Hapo mtalia na kusaga meno yenu kwa uchungu. 29 Watu watakuja kutoka mashariki, magharibi, kaskazini na kusini. Watakaa kuizunguka meza ya chakula katika ufalme wa Mungu. 30 Zingatieni kwamba wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.”
Yesu Atakufa Yerusalemu
(Mt 23:37-39)
31 Wakati huo huo baadhi ya Mafarisayo wakaja kwa Yesu, na wakamwambia, “Ondoka hapa, nenda ukajifiche. Kwa sababu Herode anataka kukuua!”
32 Lakini Yesu akawaambia, “Nendeni, mkamwambie yule mbweha,[a] ‘Leo na kesho ninatoa pepo wachafu na kuponya watu, na kesho kazi itakwisha.’ 33 Baada ya hilo, ni lazima niende, kwa sababu manabii wote wanapaswa kufia Yerusalemu.
34 Yerusalemu! Yerusalemu! Uwauaye manabii. Unawapiga kwa mawe watu waliotumwa na Mungu kwako. Mara ngapi nimetaka kuwasaidia watu wako! Nilitaka kuwakusanya kama kuku anavyovikusanya vifaranga vyake chini ya mbawa zake. Lakini hukuniruhusu. 35 Mungu atakuacha ukiwa. Ninawaambia, hamtaniona tena mpaka wakati ule mtakaposema, ‘Karibu! Mungu ambariki yeye ajaye katika jina la Bwana.’”(A)
© 2017 Bible League International