Old/New Testament
Yesu Akiwa Galilaya
8 Siku iliyofuata, Yesu alisafiri kupitia katika baadhi ya miji na vijiji. Yesu aliwahubiri watu Habari Njema kuhusu ufalme wa Mungu. Mitume kumi na wawili walikuwa pamoja naye. 2 Walikuwepo pia baadhi ya wanawake ambao Yesu aliwaponya magonjwa na pepo wabaya. Mmoja wao alikuwa Mariamu aitwaye Magdalena ambaye alitokwa na pepo saba; 3 Pia pamoja na wanawake hawa alikuwepo Yoana mke wa Kuza (msimamizi wa mali za Herode), Susana, na wanawake wengine wengi. Wanawake hawa walitumia fedha zao kuwahudumia Yesu na mitume wake.
Simulizi Kuhusu Mkulima Aliyepanda Mbegu
(Mt 13:1-17; Mk 4:1-12)
4 Kundi kubwa la watu lilikusanyika. Watu walimjia Yesu kutoka katika kila mji, naye Yesu akawaambia fumbo hili:
5 “Mkulima alikwenda kupanda mbegu. Alipokuwa akizitawanya, baadhi zilianguka kandokando ya njia. Watu wakazikanyaga, na ndege wa angani wakazila. 6 Zingine zikaanguka kwenye udongo wenye mawe. Zilipoanza kukua zikafa kwa sababu ya kukosa maji. 7 Mbegu zingine ziliangukia kwenye miiba. Miiba ikakua pamoja nazo, miiba ikazisongasonga na hazikukua. 8 Zilizosalia ziliangukia kwenye udongo mzuri wenye rutuba. Mbegu hizi zikaota na kuzaa kila moja mia.”
Yesu akamalizia fumbo. Kisha akapaza sauti, akasema, “Ninyi watu mnaonisikia, sikilizeni!”
9 Wafuasi wake wakamwuliza, “Fumbo hili linamaanisha nini?”
10 Akasema, “Mmechaguliwa kujua kweli za siri kuhusu ufalme wa Mungu. Lakini ninatumia mafumbo kuzungungumza na watu wengine. Ninafanya hivi ili,
‘Watazame,
lakini wasiweze kuona.
Wasikia,
lakini wasielewe.’(A)
Yesu Afafanua Simulizi Kuhusu Mbegu
(Mt 13:18-23; Mk 4:13-20)
11 Hii ndiyo maana ya fumbo hili: Mbegu ni Neno la Mungu. 12 Watu wengine ni kama mbegu zilizoanguka njiani. Husikia mafundisho ya Mungu, lakini Shetani huja na kuwafanya waache kuyatafakari. Hii huwafanya kutoamini na kuokoka. 13 Wengine wanafanana na mbegu zilizoanguka kwenye udongo wenye mawe. Ni watu ambao huyasikia mafundisho ya Mungu na kuyapokea kwa furaha, lakini kwa kuwa hawana mizizi yenye kina, huamini kwa muda mfupi. Majaribu yanapokuja, humwacha Mungu.
14 Zilizoanguka katika miiba, zinafanana na watu wanaoyasikia Mafundisho ya Mungu, lakini wanaruhusu wasiwasi, mali na anasa za maisha haya kuwasimamisha na hawaendelei kukua. Hivyo mafundisho hayazalishi matokeo mazuri katika maisha yao.[a] 15 Na zile zilizoangukia katika udongo mzuri, ni wale ambao huyasikia mafundisho ya Mungu kwa moyo safi na mnyoofu. Huyatii na kwa uvumilivu wao huzaa mazao mazuri.
Zingatieni Nuru
(Mk 4:21-25)
16 Hakuna mtu anayewasha taa na kuifunika kwa bakuli au kuificha uvunguni mwa kitanda. Badala yake huiweka kwenye kinara cha taa mahali palipo wazi, ili wanaoingia ndani wapate nuru ya kuwawezesha kuona. 17 Kila jambo lililofichwa litawekwa wazi na kila siri itajulikana na kila mtu ataiona. 18 Hivyo yatafakarini kwa umakini yale mnayosikia. Watu wenye uelewa kiasi watapokea zaidi. Lakini wale wasio na uelewa watapoteza hata ule wanaodhani kuwa wanao.”
Wafuasi wa Yesu ni Familia Yake Halisi
(Mt 12:46-50; Mk 3:31-35)
19 Mama yake Yesu na wadogo zake wakaenda kumwona, lakini walishindwa kumfikia kwa sababu walikuwepo watu wengi sana. 20 Mtu mmoja akamwambia Yesu, “Mama yako na wadogo zako wamesimama nje. Wanataka kukuona.”
21 Yesu akawajibu “Mama yangu na wadogo zangu ni wale wanaolisikia na kulitii Neno la Mungu.”
Yesu Atuliza Dhoruba
(Mt 8:23-27; Mk 4:35-41)
22 Siku moja Yesu na wafuasi wake walipanda mashua. Akawaambia, “Tuvuke mpaka upande mwingine wa ziwa.” Wakaanza safari kuvuka ziwa. 23 Walipokuwa wanasafiri, Yesu alisinzia. Tufani kubwa ikalikumba ziwa na mashua ikaanza kujaa maji, wakawa katika hatari. 24 Wafuasi wakamwendea, wakamwamsha, wakasema, “Mkuu, mkuu, tutazama!”
Yesu akasimama, akaukemea upepo na mawimbi ya maji. Upepo ukakoma na ziwa likatulia. 25 Ndipo Yesu akawaambia wafuasi wake, “Imani yenu iko wapi?”
Lakini wao waliogopa na kustaajabu, wakanong'onezana, “Huyu ni mtu wa namna gani? Anaamuru upepo na maji, na vinamtii?”
© 2017 Bible League International