M’Cheyne Bible Reading Plan
Yesu Amefufuka Kutoka Mauti
(Mk 16:1-8; Lk 24:1-12; Yh 20:1-10)
28 Alfajiri mapema siku iliyofuata baada ya siku ya Sabato, yaani siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalena na mwanamke mwingine aliyeitwa Mariamu alikwenda kuliangalia kaburi.
2 Ghafla malaika wa Bwana akaja kutoka mbinguni, na tetemeko kubwa likatokea. Malaika alikwenda kaburini na kulivingirisha jiwe kutoka kwenye mlango wa kaburi. Kisha akaketi juu ya jiwe. 3 Malaika alikuwa anang'aa kama miali ya radi. Mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. 4 Askari waliokuwa wanalinda kaburi walimwogopa sana malaika, walitetemeka kwa woga na wakawa kama watu waliokufa.
5 Malaika akawaambia wale wanawake, “Msiogope. Ninajua mnamtafuta Yesu, aliyeuawa msalabani. 6 Lakini hayupo hapa. Amefufuka kutoka kwa wafu, kama alivyosema. Njooni mwone mahali ulipokuwa mwili wake. 7 Nendeni haraka mkawaambie wafuasi wake, ‘Yesu amefufuka kutoka kwa wafu. Amekwenda Galilaya na atafika huko kabla yenu. Na mtamwona huko.’” Kisha malaika akasema, “Sasa nimewaambia.”
8 Hivyo wanawake wakaondoka haraka kaburini. Waliogopa sana, lakini walijawa na furaha. Walipokuwa wanakimbia kwenda kuwaambia wafuasi wake kilichotokea, 9 ghafla Yesu alisimama mbele yao. Akasema, “Salamu!” Wanawake wakamwendea wakamshika miguu na wakamwabudu. 10 Kisha Yesu akawaambia, “Msiogope. Nendeni mkawaambie wafuasi wangu[a] waende Galilaya, wataniona huko.”
Taarifa ya Kufufuka Yesu Yawafikia Viongozi wa Kiyahudi
11 Wanawake wakaenda kuwaambia wafuasi. Na wakati huo huo baadhi ya askari waliokuwa wanalinda kaburi waliingia mjini. Walikwenda kuwaambia viongozi wa makuhani kila kitu kilichotokea. 12 Ndipo makuhani wakakutana na viongozi wazee wa Kiyahudi na kufanya mpango. Wakawalipa wale askari pesa nyingi 13 na kuwaambia, “Waambieni watu kuwa wafuasi wake walikuja usiku na kuuiba mwili mlipokuwa mmesinzia. 14 Gavana atakaposikia juu ya hili, tutazungumza naye ili msiadhibiwe.” 15 Hivyo wale askari wakachukua pesa na kuwatii makuhani. Na jambo hili[b] bado linasambaa miongoni mwa Wayahudi hata hivi leo.
Yesu Azungumza na Wafuasi Wake
(Mk 16:14-18; Lk 24:36-49; Yh 20:19-23; Mdo 1:6-8)
16 Wale wafuasi kumi na mmoja walikwenda Galilaya, kwenye mlima ambao Yesu aliwaambia waende. 17 Wakiwa mlimani, wafuasi wale walimwona Yesu na wakamwabudu. Lakini baadhi ya wafuasi hawakuwa na uhakika kama alikuwa Yesu. 18 Kisha Yesu akawajia na akasema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 Hivyo nendeni ulimwenguni kote mkawafanye watu kuwa wafuasi wangu. Mkiwabatiza katika jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. 20 Wafundisheni kutii kila kitu nilichowaambia. Na tambueni hili: Niko pamoja nanyi daima. Na nitaendelea kuwa pamoja nanyi hata mwisho wa wakati.”
Paulo Katika Kisiwa cha Malta
28 Tulipokuwa salama nchi kavu, tukatambua kuwa kisiwa kile kinaitwa Malta. 2 Watu walioishi pale walikuwa wema sana kwetu. Mvua ilikuwa inanyesha na kulikuwa baridi sana, hivyo walitengeneza moto na kutukaribisha sote. 3 Paulo alikusanya kuni nyingi kwa ajili ya moto. Alipokuwa akiweka kuni kwenye moto, nyoka mwenye sumu kali akajitokeza kwa sababu ya joto na kumuuma kwenye mkono. 4 Wenyeji wa kisiwa kile walipomwona nyoka ananing'inia kwenye mkono wa Paulo, walisema, “Mtu huyu lazima ni mwuaji! Hakufa baharini, lakini Haki[a] hataki aishi.”
5 Lakini Paulo alimku'ngutia nyoka kwenye moto na hakudhurika. 6 Watu wakadhani atavimba au ataanguka na kufa. Walisubiri na kumwangalia kwa muda mrefu, lakini hakuna kibaya kilichomtokea. Hivyo wakabadili mawazo yao. Wakasema, “Paulo ni mungu!”
7 Yalikuwepo mashamba kuzunguka eneo lile. Yaliyomilikiwa na ofisa wa juu sana wa Rumi katika kisiwa hicho aliyeitwa Pablio. Alitukaribisha nyumbani kwake na alikuwa mwema sana kwetu. Tulikaa nyumbani kwake kwa siku tatu. 8 Baba yake Pablio alikuwa mgonjwa sana. Alikuwa na homa na alikuwa anaharisha damu, lakini Paulo alikwenda kwake na kumuombea. Aliweka mikono juu yake naye akapona. 9 Baada ya hili kutokea, wagonjwa wengine wote kisiwani walikuja kwa Paulo, naye aliwaombea na wakaponywa pia.
10-11 Watu katika kisiwa hiki walituheshimu sana. Na baada ya kuwa pale kwa miezi mitatu, tukawa tayari kuondoka, walitupa kila kitu tulichohitaji kwa ajili ya safari yetu.
Paulo Aenda Rumi
Tulipanda meli iliyotoka Iskanderia iliyokaa katika kisiwa cha Malta wakati majira ya baridi. Mbele ya meli kulikuwa alama ya miungu pacha.[b] 12 Tulisimama katika mji wa Sirakuse. Tulikaa pale kwa siku tatu kisha tukaondoka. 13 Tulifika katika mji wa Regio. Siku iliyofuata upepo ulianza kuvuma kutokea Kusini-Magharibi, hivyo tuliweza kuondoka. Baada ya siku moja tukafika katika mji wa Puteoli. 14 Tuliwapata baadhi ya waamini pale, walituomba tukae nao kwa wiki moja. Mwishowe tulifika Rumi. 15 Ndugu na dada waliokaa Rumi walisikia habari zetu, walikuja kutupokea kwenye Soko la Apio[c] na kwenye Migahawa Mitatu.[d] Paulo alipowaona waamini hawa, alimshukuru Mungu na alifarijika.
Paulo Akiwa Rumi
16 Tulipofika Rumi, Paulo aliruhisiwa kuishi peke yake. Lakini askari alikaa pamoja naye kumlinda.
17 Siku tatu baadaye Paulo aliagiza baadhi ya Wayahudi muhimu waje kwake. Walipokusanyika, akasema, “Ndugu zangu, sijafanya lolote kinyume na watu wetu au kinyume na desturi za baba zetu. Lakini nilikamatwa Yerusalemu na kukabidhiwa kwa Warumi. 18 Waliniuliza maswali mengi, lakini hawakupata sababu yoyote kwa nini niuawe. Hivyo walitaka kuniachia huru. 19 Lakini Wayahudi kule hawakutaka hilo. Hivyo ilinibidi niombe kuja Rumi kuweka mashitaka yangu mbele ya Kaisari. Kwa kufanya hivi haimaanishi kuwa ninawashutumu watu wangu kwa kufanya chochote kibaya. 20 Ndiyo sababu nilitaka kuonana na kuzungumza nanyi. Nimefungwa kwa minyororo hii kwa sababu ninaamini katika tumaini la Israeli.”
21 Wayahudi walimjibu Paulo, “Hakuna barua tuliyoipokea kutoka Uyahudi kuhusu wewe. Hakuna ndugu yetu yeyote Myahudi aliyesafiri kutoka huko aliyeleta habari zako au kutwambia chochote kibaya juu yako. 22 Tunataka kusikia mawazo yako. Tunafahamu kuwa watu kila mahali wanapinga kundi hili jipya.”
23 Paulo na Wayahudi walichagua siku kwa ajili ya mkutano. Siku hiyo Wayahudi wengi walikutana na Paulo katika nyumba yake. Aliwaambia kwa siku nzima, akawafafanulia kuhusu ufalme wa Mungu. Alitumia Sheria ya Musa na maandishi ya manabii kuwashawishi kumwamini Yesu. 24 Baadhi ya Wayahudi waliamini alichosema, lakini wengine hawakuamini. 25 Walibishana wao wenyewe na wakaanza kuondoka. Lakini aliwaambia kitu kimoja zaidi: “Roho Mtakatifu aliwaambia ukweli baba zenu kupitia nabii Isaya, aliposema,
26 ‘Nenda kwa watu hawa na uwaambie:
Mtasikiliza na kusikiliza,
lakini hamtaelewa.
Mtatazama na kutazama,
lakini hakika hamtaona.
27 Watu hawa hawawezi kuelewa.
Masikio yao yamezibwa.
Na macho yao yamefumbwa.
Hivyo hawawezi kuona kwa macho yao,
au kusikia kwa masikio yao;
au kuelewa kwa akili zao;
au kuelewa kwa akili zao.
Ikiwa wangeelewa, wangeweza kunirudia,
na ningewaponya.’(A)
28 Ninataka ninyi Wayahudi mjue kuwa Mungu ameupeleka wokovu wake kwa watu wasio Wayahudi. Watasikia!” 29 [e]
30 Paulo alikaa katika nyumba yake mwenyewe aliyopanga kwa miaka miwili kamili. Aliwakaribisha watu wote waliokuja kumtembelea. 31 Aliwaambia kuhusu ufalme wa Mungu na kuwafundisha kuhusu Bwana Yesu Kristo. Alikuwa na ujasiri sana, na hakuna aliyejaribu kumzuia asizungumze.
© 2017 Bible League International