M’Cheyne Bible Reading Plan
Yesu Aonya Kuhusu Wakati Ujao
(Mk 13:1-31; Lk 21:5-33)
24 Yesu alipokuwa anaondoka eneo la Hekalu, wanafunzi wake walimwendea na kumwonyesha majengo ya Hekalu. 2 Akawauliza, “Mnayaona majengo haya? Ukweli ni kuwa, yataharibiwa. Kila jiwe litadondoshwa chini, hakuna jiwe litakaloachwa juu ya jiwe jingine.”
3 Baadaye, Yesu alipokuwa ameketi mahali fulani katika Mlima wa Mizeituni, Wafuasi wake walimwendea faraghani. Wakasema, “Twambie mambo haya yatatokea lini. Na nini kitatokea ili kutuandaa kwa ajili ya ujio wako na mwisho wa nyakati?”
4 Yesu akajibu, “Mjihadhari! Msimruhusu mtu yeyote awadanganye. 5 Watu wengi watakuja na watatumia jina langu. Watasema, ‘Mimi ndiye Masihi.’ Na watawadanganya watu wengi. 6 Mtasikia kuhusu vita vinanavyopiganwa na pia matetesi ya kuwapo vita vingine. Lakini msiogope. Mambo haya lazima yatokee na mwisho wenyewe hautafuata palepale. 7 Mataifa yatapigana na mataifa mengine. Falme zitapigana na falme zingine. Utakuwepo wakati wa njaa ambapo watu watakosa chakula. Na kutakuwa matetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali. 8 Mambo haya ni mwanzo wa matatizo, kama uchungu wa kwanza mwanamke anapozaa.
9 Kisha mtakamatwa na kupelekwa kwa wenye mamlaka ili mhukumiwe na kuuawa. Watu wote katika ulimwengu watawachukia kwa sababu mnaniamini mimi. 10 Nyakati hizo watu wengi wataacha kuwa wafuasi wangu. Watasalitiana na kuchukiana. 11 Manabii wengi watatokea na kusababisha watu wengi kuamini mambo yasiyo ya kweli. 12 Kutakuwepo na uovu mwingi sana duniani kiasi kwamba upendo wa waaminio wengi utapoa. 13 Lakini yeyote yule atakayekuwa mwaminifu mpaka mwisho ataokolewa. 14 Na Habari Njema niliyoihubiri kuhusu Ufalme wa Mungu itahubiriwa ulimwenguni kote. Itatawanywa katika kila taifa. Kisha mwisho utakuja.
15 Nabii Danieli alizungumza kuhusu ‘jambo la kutisha litakalosababisha uharibifu.’[a] Mtakapoliona jambo hili la kutisha limesimama patakatifu.” (Asomaye hili anapaswa kuelewa jambo hili linamaanisha nini.) 16 “Watu walio Uyahudi wakimbilie milimani. 17 Wakimbie pasipo kupoteza muda ili kuchukua kitu chochote. Wakiwa darini wasiteremke ili kuchukua kitu na kukitoa nje ya nyumba. 18 Wakiwa shambani wasirudi nyumbani kuchukua koti.
19 Itakuwa hali ngumu kwa wanawake wenye mimba na wenye watoto wachanga! 20 Ombeni isiwe majira ya baridi au isiwe siku ya Sabato mambo haya yatakapotokea na mkalazimika kukimbia, 21 kwa sababu utakuwa wakati wa dhiki kuu. Kutakuwepo na usumbufu mwingi sana kuliko ule uliowahi kutokea tangu mwanzo wa ulimwengu. Na hakuna jambo baya kama hilo litakalotokea tena.
22 Lakini Mungu amekwisha amua kuufupisha wakati huo. Ikiwa usingefupishwa, hakuna ambaye angeendelea kuishi. Lakini Mungu ataufupisha ili kuwasaidia watu aliowachagua.
23 Wakati huo watu wataweza kuwaambia, ‘Tazama, Masihi yuko kule!’ Au wakasema, ‘Ni yule!’ Msiwaamini. 24 Manabii wa uongo na masihi wa uongo watatokea na kufanya miujiza na maajabu[b] makuu, ili ikiwezekana wawadanganye wateule. 25 Na sasa nimewatahadharisha kuhusu hili kabla halijatokea.
Yesu Atakaporudi Tena
(Mk 13:24-31; Lk 17:23-24,37; 21:25-32)
26 Inawezekana mtaambiwa, ‘Masihi yuko jangwani!’ Msiende jangwani kumtafuta. Mtu mwingine anaweza akasema, ‘Masihi yuko katika chumba kile!’ Msiamini. 27 Mwana wa Adamu atakapokuja, kila mtu atamwona. Itakuwa kama radi inavyowaka angani na kuonekana kila mahali. 28 Ni kama kutafuta mzoga: Mzoga hupatikana mahali ambapo tai wengi wamekusanyika.
29 Mara baada ya mateso ya siku hizo, mambo haya yatatokea:
‘Jua litakuwa jeusi,
na mwezi hautatoa mwanga.
Nyota zitaanguka kutoka angani,
na kila kitu kilicho angani
kitatikiswa kutoka mahali pake.’[c]
30 Kisha kutatokea ishara angani kuwa Mwana wa Adamu anakuja. Watu wote wa ulimwengu watajipiga kifuani wakiomboleza. Kila mtu atamwona Mwana wa Adamu akija katika mawingu ya angani akiwa na nguvu na utukufu mkuu. 31 Naye atatumia parapanda kuu kuwatuma malaika zake kila mahali duniani. Nao watawakusanya wateule wake kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwingine.
32 Jifunze kwa mtini: Matawi yake yanapokuwa ya kijani na laini na kuanza kutoa majani mapya, ndipo mnatambua kuwa majira ya joto yamekaribia. 33 Katika namna hiyo hiyo, mtakapoona mambo haya yote yakitokea, mtajua kuwa wakati[d] umekaribia wa kile kitakachotokea. 34 Ninawahakikishia kuwa mambo haya yote yatatokea wakati ambao baadhi ya watu wa nyakati hizi wakiwa bado hai. 35 Ulimwengu wote, dunia na anga vitaangamizwa, lakini maneno yangu yatadumu milele.
Mungu Peke Yake Ndiye Ajuaye Siku ya Kurudi kwa Mwana wa Adamu
(Mk 13:32,35; Lk 17:26-30,34-36)
36 Hakuna anayeijua siku wala wakati. Malaika wa mbinguni hawaijui hata Mwana hajui itakuwa lini. Baba peke yake ndiye anayejua.
37 Mwana wa Adamu atakapokuja, itakuwa kama ilivyokuwa nyakati za Nuhu. 38 Siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuwatoa binti zao kuolewa mpaka siku ambayo Nuhu aliingia kwenye safina. 39 Hawakujua juu ya kilichokuwa kinaendelea mpaka mafuriko yalipowajia na kuwaangamiza wote.
Ndiyo itakavyokuwa Mwana wa Adamu atakapokuja. 40 Wanaume wawili watakuwa wakifanya kazi shambani, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. 41 Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.
42 Hivyo iweni tayari daima. Hamjui siku ambayo Bwana wenu atarudi. 43 Mwenye nyumba angefanya nini ikiwa angejua wakati ambao mwizi atakuja? Mnajua angelikesha ili mwizi asivunje na kuingia. 44 Hivyo, ninyi nanyi iweni tayari. Mwana wa Adamu atakuja katika wakati msiomtarajia.
Watumishi Wema na Wabaya
(Mk 13:33-37; Lk 12:41-48)
45 Fikiria mtumishi aliyewekwa na bwana wake kuwapa chakula watumishi wake wengine katika muda uliopangwa. Ni kwa namna gani mtumishi huyo atajionyesha kuwa ni mwangalifu na mwaminifu? 46 Bwana wake atakaporudi na kumkuta anafanya kazi aliyompa, siku hiyo itakuwa siku ya furaha kwa mtumishi huyo. 47 Ninawaambia bila mashaka yoyote kuwa, bwana wake atamchagua mtumishi huyo awe msimamizi wa kila kitu anachomiliki yule Bwana.
48 Lakini nini kitatokea ikiwa mtumishi huyo ni mbaya na akadhani kuwa bwana wake hatarudi karibuni? 49 Ataanza kuwapiga watumishi wengine na kuanza kunywa na kula na walevi. 50 Ndipo bwana wake atakuja wakati asioutarajia, ambapo mtumishi hakujiandaa. 51 Bwana atamwadhibu mtumishi huyo na kumpeleka anakostahili kuwapo pamoja na watumishi wengine waliojifanya kuwa wema. Huko watalia na kusaga meno kwa maumivu.
Baadhi ya Wayahudi Wamshitaki Paulo
24 Siku tano baadaye Anania, kuhani mkuu, alikwenda mjini Kaisaria. Aliwachukua pamoja naye baadhi ya viongozi wa wazee wa Kiyahudi na mwanasheria aitwaye Tertulo. Walikwenda Kaisaria kutoa ushahidi dhidi ya Paulo mbele ya gavana. 2-3 Paulo aliitwa kwenye mkutano, na Tertulo akaanza kueleza mashitaka.
Tertulo alisema, “Mheshimiwa Feliki, kwa muda mrefu watu wetu wamefurahia amani kwa sababu yako, na mambo mengi mabaya katika nchi yetu yanarekebishwa kutokana na msaada wako wa hekima. Kwa hili sisi sote tunaendelea kushukuru. 4 Lakini sitaki kuchukua muda wako mwingi. Hivyo nitasema maneno machache. Tafadhali uwe mvumilivu. 5 Mtu huyu ni mkorofi. Anasababisha vurugu kwa Wayahudi kila mahali ulimwenguni. Ni kiongozi wa kundi la Wanazorayo. 6-8 Pia, alikuwa anajaribu kulinajisi Hekalu, lakini tulimsimamisha.[a] Unaweza kuamua ikiwa haya yote ni kweli. Mwulize maswali wewe mwenyewe.” 9 Wayahudi wengine wakakubali na kusema ndivyo ilivyo.
Paulo Ajitetea Mbele ya Feliki
10 Gavana alifanya ishara ili Paulo aanze kuzungumza. Hivyo Paulo alijibu, “Gavana Feliki, ninafahamu kuwa umekuwa jaji wa nchi hii kwa muda mrefu. Hivyo ninafurahi kujitetea mimi mwenyewe mbele yako. 11 Nilikwenda kuabudu Yerusalemu siku kumi na mbili tu zilizopita. Unaweza kutambua wewe mwenyewe kuwa hii ni kweli. 12 Wayahudi hawa wanaonishitaki, hawakuniona nikibishana na mtu yeyote wala kukusanya kundi la watu Hekaluni. Na sikuwa nabishana au kufanya vurugu kwenye masinagogi au mahali popote katika mji. 13 Watu hawa hawawezi kuthibitisha mambo wanayoyasema dhidi yangu sasa.
14 Lakini nitakuambia hili: Ninamuabudu Mungu, Mungu yule yule aliyeabudiwa na baba zetu, na kama mfuasi wa Njia, ambayo wayahudi hawa wanasema si njia sahihi. Na ninaamini kila kitu kinachofundishwa katika Sheria ya Musa na yote yaliyoandikwa katika vitabu vya manabii. 15 Nina tumaini katika Mungu kama walilonalo Wayahudi hawa, kwamba watu wote, wema na wabaya, watafufuliwa kutoka kwa wafu. 16 Hii ndiyo sababu daima nimejaribu kufanya kile ninachoamini kuwa sahihi mbele za Mungu na kila mtu.
17-18 Nimekuwa mbali na Yerusalemu kwa miaka mingi. Nilikwenda kule nikiwa na fedha za kuwasaidia watu wangu. Pia nilikuwa na sadaka za kutoa Hekaluni. Nilipokuwa nafanya hivyo, baadhi ya Wayahudi waliponiona pale. Nilikuwa nimemaliza ibada ya utakaso.[b] Sikufanya vurugu yoyote, na hakuna watu waliokuwa wamekusanyika kunizunguka. 19 Lakini baadhi ya Wayahudi kutoka Asia walikuwa pale. Walipaswa kuwa hapa mbele yako wakinishtaki ikiwa wana ushahidi kuwa nilifanya kitu chochote kibaya. 20 Waulize watu hawa ikiwa waliona kosa lolote kwangu niliposimama mbele ya mkutano wa baraza kuu mjini Yerusalemu. 21 Jibu pekee watakaloweza kukujibu ni hili: Kwamba nilipokuwa mbele zao nilipaza sauti na kusema, ‘Mnanishitaki leo kwa sababu ninaamini watu watafufuka kutoka kwa wafu!’”
22 Feliki tayari alikuwa anaelewa mengi kuhusu Njia. Akasimamisha kesi na kusema, “Kamanda Lisiasi atakapokuja hapa, nitaamua nini cha kufanya.” 23 Feliki alimwambia ofisa wa jeshi kumlinda Paulo lakini wampe uhuru kiasi na wawaruhusu rafiki zake wamletee chochote atakachohitaji.
Paulo Azungumza na Feliki na Mkewe
24 Baada ya siku chache, Feliki alikuja na mke wake Drusila, aliyekuwa Myahudi. Feliki akaagiza Paulo apelekwe kwake. Alimsikiliza Paulo akiongea kuhusu kumwamini Yesu Kristo. 25 Lakini Feliki aliogopa Paulo alipoongelea kuhusu vitu kama kutenda haki, kuwa na kiasi, na hukumu itakayokuja baadaye. Akasema, “Unaweza kwenda sasa. Nitakapokuwa na muda mwingi, nitakuita.” 26 Lakini Feliki alikuwa na sababu nyingine ya kuzungumza na Paulo. Alitegemea Paulo angempa rushwa, hivyo alimwita Paulo mara nyingi na kuzungumza naye.
27 Lakini baada ya miaka miwili, Porkio Festo akawa gavana. Hivyo Feliki hakuwa gavana tena. Lakini alimwacha Paulo gerezani ili kuwaridhisha Wayahudi.
© 2017 Bible League International