M’Cheyne Bible Reading Plan
Yesu Afundisha Kuhusu Talaka
(Mk 10:1-12)
19 Yesu alipomaliza kuzungumza haya yote, aliondoka Galilaya. Alikwenda maeneo ya Yuda ng'ambo ya Mto Yordani. 2 Watu wengi walimfuata na akaponya wagonjwa wengi huko.
3 Baadhi ya Mafarisayo wakamjia Yesu. Walitaka aseme jambo fulani lisilo sahihi. Wakamwuliza, “Je, ni sahihi kwa mume kumtaliki mke wake kutokana na sababu yoyote ile kama anavyotaka?”
4 Yesu akajibu, “Hakika mmesoma hili katika Maandiko: Mungu alipoumba ulimwengu, ‘aliumba watu wa jinsi ya kiume na wa jinsi ya kike.’(A) 5 Na Mungu alisema, ‘Hii ndiyo sababu mwanaume atawaacha baba na mama yake na kuungana na mke wake. Na hao watu wawili watakuwa mmoja.’(B) 6 Hivyo wao si wawili tena, bali mmoja. Ni Mungu aliowaunganisha pamoja, hivyo mtu yeyote asiwatenganishe.”
7 Mafarisayo wakauliza, “Sasa kwa nini Musa alitoa amri ya kumruhusu mwanaume kumtaliki mke wake kwa kuandika hati ya talaka?”[a]
8 Yesu akajibu, “Musa aliwaruhusu kuwataliki wake zenu kwa sababu mlikataa kupokea mafundisho ya Mungu. Lakini talaka haikuruhusiwa hapo mwanzo. 9 Ninawaambia kuwa, kila anayemtaliki mke wake, isipokuwa kutokana na uzinzi, na akamwoa mwanamke mwingine, anazini.”
10 Wafuasi wakamwambia Yesu, “Ikiwa hiyo ndiyo sababu pekee ambayo mtu anaruhusiwa kumtaliki mke wake, ni bora kutooa.”
11 Akajibu, “Tamko hili ni la kweli kwa baadhi ya watu, lakini si kwa kila mtu. Bali ni kwa wale tu waliopewa karama hii. 12 Kuna sababu tofauti kwa nini baadhi ya wanaume hawaoi.[b] Wengine wamezaliwa wakiwa hawana uwezo wa kuzaa watoto, wengine walifanywa hivyo katika maisha yao ya baadaye. Na wengine walichagua kutokuoa kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Hili liko hivyo kwa kila anayeweza kulikubali.”
Yesu Awakaribisha Watoto
(Mk 10:13-16; Lk 18:15-17)
13 Ndipo watu wakawaleta watoto wao wadogo kwa Yesu ili awabariki na kuwaombea. Wafuasi wake walipoliona hili, waliwakataza watu wasiwalete watoto kwa Yesu. 14 Lakini Yesu akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wa watu walio kama watoto hawa wadogo.” 15 Baada ya Yesu kuwabariki watoto, aliondoka huko.
Mtu Tajiri Akataa Kumfuata Yesu
(Mk 10:17-31; Lk 18:18-30)
16 Mtu mmoja alimwendea Yesu na kumwuliza, “Mwalimu, nifanye jambo gani lililo jema ili niweze kuupata uzima wa milele?”
17 Yesu akajibu, “Kwa nini unaniuliza kuhusu jambo gani lililo jema? Mungu pekee yake ndiye mwema. Lakini ikiwa unataka kuupata uzima wa milele, zitii amri.”
18 Yule mtu akauliza, “Amri zipi?”
Yesu akajibu, “‘Usiue, usizini, usiibe, usiseme uongo, 19 mheshimu baba na mama yako,’(C) na ‘mpende jirani yako[c] kama unavyojipenda wewe mwenyewe.’”(D)
20 Yule kijana akasema, “Ninazitii amri hizi zote. Nifanye nini zaidi?”
21 Yesu akajibu, “Ikiwa unataka kuwa mkamilifu, nenda ukauze kila kitu unachomiliki. Uwape pesa maskini na utakuwa na utajiri mbinguni. Kisha njoo unifuate!”
22 Lakini kijana aliposikia Yesu anamwambia kuhusu kugawa pesa yake, alihuzunika. Hakutaka kufanya hivi kwa kuwa alikuwa tajiri sana. Hivyo aliondoka.
23 Ndipo Yesu aliwaambia wafuasi wake, “Ukweli ni huu, itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. 24 Ndiyo, ninawaambia, ni rahisi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”
25 Wafuasi waliposikia hili walishangaa. Wakauliza, “Sasa ni nani ataweza kuokolewa?”
26 Yesu akawatazama na kuwaambia, “Hili haliwezekani kwa wanadamu, Lakini yote yanawezekana kwa Mungu.”
27 Petro akamwambia, “Tuliacha kila kitu tulichonacho na kukufuata wewe. Tutapata nini?”
28 Yesu akawaambia, “Wakati wa ulimwengu mpya utakapofika, Mwana wa Adamu ataketi kwenye kiti chake cha enzi, kikuu na chenye utukufu mwingi. Na ninaweza kuwaahidi kuwa ninyi mnaonifuata mtaketi kwenye viti kumi na viwili vya enzi, na mtayahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. 29 Kila aliyeacha nyumba, ndugu, dada, baba, mama, watoto au shamba na akanifuata atapata zaidi ya yale aliyoacha. Na atapata uzima wa milele. 30 Watu wengi walio wa kwanza sasa watakuwa wa mwisho siku zijazo. Na walio wa mwisho sasa watakuwa wa kwanza siku zijazo.
Paulo Akiwa Efeso
19 Apolo alipokuwa katika mji wa Korintho, Paulo alikuwa anatembelea baadhi ya sehemu akiwa njiani kwenda Efeso. Alipofika Efeso waliwakuta baadhi ya wafuasi wa Bwana. 2 Akawauliza, “Mlimpokea Roho Mtakatifu mlipoamini?”
Wafuasi hao wakamwambia, “Hatujawahi hata kusikia kuhusu Roho Mtakatifu!”
3 Paulo akawauliza, “Kwa hiyo ni mlibatizwa kwa ubatizo gani?”
Wakasema, “Kwa ubatizo aliofundisha Yohana.”
4 Paulo akasema, “Yohana aliwaambia watu wabatizwe kuonesha kuwa walidhamiria kubadili maisha yao. Aliwaambia watu kuamini katika yule atakaye kuja baada yake, naye huyo ni Yesu.”
5 Wafuasi hawa waliposikia hili, wakabatizwa katika jina la Bwana Yesu. 6 Kisha Paulo akawawekea mikono, na Roho Mtakatifu akaja juu yao. Wakaanza kuzungumza na kutabiri katika lugha tofauti. 7 Walikuwepo wanaume kama kumi na mbili katika kundi hili.
8 Paulo akaingia katika sinagogi na akazungumza kwa ujasiri. Aliendelea kufanya hivi kwa miezi mitatu. Alizungumza na Wayahudi, akijaribu kuwashawishi kukubali alichokuwa anawaambia kuhusu ufalme wa Mungu. 9 Lakini baadhi yao wakawa wakaidi, wakakataa kuamini. Waliikashifu Njia[a] ya Bwana mbele ya kila mtu. Hivyo Paulo aliwaacha Wayahudi hawa na kuwachukua wafuasi wa Bwana pamoja naye. Alikwenda mahali ambapo mtu aitwaye Tirano alikuwa na shule. Hapo Paulo alizungumza na watu kila siku. 10 Alifanya hivi kwa miaka miwili na kila mtu aliyeishi Asia, Wayahudi na Wayunani alilisikia neno la Bwana.
Wana wa Skewa
11 Mungu alimtumia Paulo kufanya miujiza ya kipekee. 12 Baadhi ya watu walichukua vitambaa vya mkononi na nguo zilizovaliwa na Paulo na kuziweka juu ya wagonjwa. Wagonjwa waliponywa na pepo wabaya waliwatoka watu.
13-14 Pia baadhi ya Wayahudi walikuwa wanasafiri huku na huko wakiwatoa pepo wabaya kwa watu. Wana saba wa Skewa, mmoja wa viongozi wa makuhani, walikuwa wakifanya hili. Wayahudi hawa walijaribu kutumia jina la Bwana kuyatoa mapepo kwa watu. Wote walikuwa wanasema, “Katika jina la Bwana Yesu anayezungumzwa na Paulo ninakuamuru utoke!”
15 Lakini wakati fulani pepo akawaambia Wayahudi hawa, “Ninamfahamu Yesu, na ninafahamu kuhusu Paulo, na ninyi ni nani?”
16 Kisha mtu aliyekuwa na pepo ndani yake akawarukia. Alikuwa na nguvu kuliko wote. Akawapiga, akawachania nguo za na kuwavua, nao wakakimbia kutoka katika nyumba ile wakiwa uchi.
17 Watu wote katika Efeso, Wayahudi na Wayunani wakafahamu kuhusu hili. Wakaogopa na kumtukuza Bwana Yesu. 18 Waamini wengi walianza kukiri, wakisema mambo yote maovu waliyotenda. 19 Baadhi yao walikuwa wametumia uchawi huko nyuma. Waamini hawa walileta vitabu vyao vya uchawi na kuvichoma mbele ya kila mtu. Vitabu hivi vilikuwa na thamani ya sarafu hamsini elfu za fedha.[b] 20 Hivi ndivyo ambavyo neno la Bwana lilikuwa linasambaa kwa nguvu, likisababisha watu wengi kuamini.
Paulo Apanga Safari
21 Baada ya hili, Paulo alipanga kwenda Yerusalemu. Alipanga kupitia katika majimbo ya Makedonia na Akaya kisha kwenda Yerusalemu. Alisema, “Baada ya kwenda Yerusalemu, ni lazima niende Rumi pia.” 22 Timotheo na Erasto walikuwa wasaidizi wake wawili. Paulo aliwatuma watangulie Makedonia. Lakini yeye alikaa Asia kwa muda.
Tatizo Katika Mji wa Efeso
23 Lakini katika wakati huo huo kulikuwepo tatizo kuhusiana na Njia. Hivi ndivyo ilivyotokea: 24 Alikuwepo mtu aliyeitwa Demetrio aliyekuwa mfua fedha. Alikuwa akitengeneza sanamu ndogo za fedha zilizofanana na hekalu la Artemi, mungu mke. Wanaume waliokuwa wakifanya kazi hii walijipatia pesa nyingi sana.
25 Demetrio alifanya mkutano na watu hawa pamoja na wengine waliokuwa wanafanya kazi ya aina hiyo. Akawaambia, “Ndugu, mnafahamu kuwa tunapata pesa nyingi kutokana na kazi yetu. 26 Lakini angalieni kitu ambacho mtu huyu Paulo anafanya. Sikilizeni anachosema. Amewashawishi watu wengi katika Efeso na karibu Asia yote kubadili dini zao. Anasema miungu ambayo watu wanatengeneza kwa mikono si miungu wa kweli. 27 Ninaogopa hili litawafanya watu kuwa kinyume na biashara yetu. Lakini kuna tatizo jingine pia. Watu wataanza kufikiri kuwa hekalu la Artemi, mungu wetu mkuu halina maana. Ukuu wake utaharibiwa. Na Artemi ni mungu mke anayeabudiwa na kila mtu katika Asia na ulimwengu wote.”
28 Waliposikia hili, walikasirika sana. Wakapaza sauti zao wakisema, “Artemi, mungu mke wa Efeso ni mkuu!” 29 Mji wote ukalipuka kwa vurugu. Watu wakawakamata Gayo na Aristarko, waliotoka Makedonia waliokuwa wanasafiri na Paulo, wakawapeleka kwenye uwanja wa mji. 30 Paulo alitaka kwenda ili azungumze na watu, lakini wafuasi wa Bwana walimzuia. 31 Pia, baadhi ya viongozi katika jimbo la Asia waliokuwa rafiki zake walimtumia ujumbe wakimwambia asiende uwanjani.
32 Watu wengi walikuwa akipiga kelele kusema hili na wengine walisema jambo jingine. Mkutano ukawa na vurugu kubwa. Watu wengi hawakujua ni kwa nini walikwenda pale. 33 Baadhi ya Wayahudi wakamshawishi mtu mmoja aliyeitwa Iskanda asimame mbele ya umati, wakamwelekeza cha kusema. Iskanda alipunga mkono wake, akijaribu kuwaeleza watu jambo. 34 Lakini watu walipoona kuwa Iskanda ni Myahudi, wote wakaanza kupiga kelele ya aina moja. Kwa masaa mawili waliendelea kusema, “Artemi, mungu mke wa Efeso ni mkuu!”
35 Ndipo karani wa mji akawashawishi watu kunyamaza. Akawaambia, “Watu wa Efeso, kila mtu anafahamu kwamba Efeso ndiyo mji unaotunza hekalu la mungu mkuu mke Artemi. Kila mtu anafahamu pia kwamba tunatunza mwamba wake mtakatifu.[c] 36 Hakuna anayeweza kupinga hili, hivyo mnyamaze. Ni lazima mtulie na kufikiri kabla hamjafanya kitu chochote.
37 Mmewaleta watu[d] hawa hapa, lakini hawajasema kitu chochote kibaya kinyume na mungu wetu mke. Hawajaiba kitu chochote kutoka kwenye hekalu lake. 38 Tuna mahakama za sheria na wapo waamuzi. Je, Demetrio na watu hawa wanaofanya kazi pamoja naye wana mashitaka dhidi ya yeyote? Wanapaswa kwenda mahakamani wakawashtaki huko.
39 Kuna kitu kingine mnataka kuzungumzia? Basi njooni kwenye mikutano ya kawaida ya mji mbele ya watu. Litaweza kuamuriwa huko. 40 Ninasema hivi kwa sababu mtu mwingine anaweza kuona tukio hili la leo na akatushtaki kwa kuanzisha ghasia. Hatutaweza kufafanua vurugu hii, kwa sababu hakuna sababu za msingi za kuwepo mkutano huu.” 41 Baada ya karani wa mji kusema hili, aliwaambia watu kwenda majumbani mwao.
© 2017 Bible League International