Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

M’Cheyne Bible Reading Plan

The classic M'Cheyne plan--read the Old Testament, New Testament, and Psalms or Gospels every day.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Error: Book name not found: Gen for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Mathayo 21

Yesu Aingia Yerusalemu Kama Mfalme

(Mk 11:1-11; Lk 19:28-38; Yh 12:12-19)

21 Yesu na wafuasi wake walipokaribia Yerusalemu, walisimama Bethfage kwenye kilima kinachoitwa Mlima wa Mizeituni. Wakiwa hapo Yesu aliwatuma wafuasi wake wawili mjini. Aliwaambia, “Nendeni kwenye mji mtakaoweza kuuona huko. Mtakapoingia katika mji huo, mtamwona punda na mwanapunda wake.[a] Wafungueni wote wawili, kisha waleteni kwangu. Mtu yeyote akiwauliza kwa nini mnawachukua punda, mwambieni, ‘Bwana anawahitaji. Atawarudisha mapema.’”

Hili lilitimiza maneno yaliyosemwa na nabii:

“Waambie watu wa Sayuni,[b]
    ‘Mfalme wako anakuja sasa.
Ni mnyenyekevu na amempanda punda.
    Na amempanda mwana punda dume tena safi.’”(A)

Wafuasi walikwenda na kufanya yale walioambiwa na Yesu. Waliwaleta kwake punda jike na mwanapunda. Waliwafunika punda kwa nguo zao na Yesu akaketi juu yao. Akiwa njiani kuelekea Yerusalemu, watu wengi walitandaza mavazi yao barabarani kwa ajili Yake. Wengine walikata matawi ya miti na kuyatandaza barabarani ili kumkaribisha. Wengine walimtangulia Yesu, na wengine walikuwa nyuma yake. Wote walipaza sauti wakisema:

“Msifuni[c] Mwana wa Daudi!
‘Karibu! Mungu ambariki yeye
    ajaye katika jina la Bwana!’(B)
Msifuni Mungu wa mbinguni!”

10 Kisha Yesu aliingia Yerusalemu. Watu wote mjini wakataharuki. Wakauliza, “Mtu huyu ni nani?”

11 Kundi la watu waliomfuata Yesu wakajibu, “Huyu ni Yesu. Ni nabii kutoka katika mji wa Nazareti ulio Galilaya.”

Yesu Asafisha Eneo la Hekalu

(Mk 11:15-19; Lk 19:45-48; Yh 2:13-22)

12 Yesu alipoingia katika eneo la Hekalu, aliwatoa nje wote waliokuwa wanauza na kununua vitu humo. Alizipindua meza za watu waliokuwa wanabadilishana pesa. Na alipindua viti vya watu waliokuwa wanauza njiwa. 13 Yesu aliwaambia, “Maandiko yanasema, ‘Hekalu langu litaitwa nyumba ya sala.’(C) Lakini mmelibadilisha na kuwa ‘maficho ya wezi’.(D)

14 Baadhi ya watu waliokuwa wasiyeona na walemavu wa miguu walimjia Yesu alipokuwa eneo la Hekalu, naye aliwaponya. 15 Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria waliona mambo ya ajabu aliyokuwa anatenda. Na waliona watoto walivyokuwa wanamsifu wakisema, “Sifa kwa Mwana wa Daudi.” Mambo haya yote yaliwakasirisha makuhani na walimu wa sheria.

16 Wakamwuliza Yesu, “Unasikia wanayosema watoto hawa?”

Akajibu, “Ndiyo. Maandiko yanasema,

‘Umewafundisha watoto wadogo na watoto
    wanyonyao kusifu.’(E)

Hamjasoma Maandiko haya?”

17 Kisha Yesu akawaacha na akaenda katika mji wa Bethania akalala huko.

Yesu Aulaani Mtini

(Mk 11:12-14,20-24)

18 Mapema asubuhi iliyofuata, Yesu alikuwa anarudi mjini Yerusalemu naye alikuwa na njaa. 19 Aliuona mtini karibu na njia na akaenda kuchuma tini kwenye mti huo. Yalikuwepo maua tu. Hivyo Yesu akauambia mti ule, “Hautazaa matunda tena!” Mtini ukakauka na kufa hapo hapo.

20 Wafuasi wake walipoona hili, walishangaa sana. Wakauliza, “Imekuwaje mtini ukakauka na kufa haraka hivyo?”

21 Yesu akajibu, “Ukweli ni kuwa, mkiwa na imani na msiwe na mashaka, mtaweza kufanya kama nilivyofanya kwa mti huu. Na mtaweza kufanya zaidi ya haya. Mtaweza kuuambia mlima huu, ‘Ng'oka na ujitupe baharini.’ Na ikiwa una imani, litafanyika. 22 Mkiamini, mtapokea kila mnachoomba.”

Viongozi Wawa na Mashaka Kuhusu Mamlaka ya Yesu

(Mk 11:27-33; Lk 20:1-8)

23 Yesu aliingia katika eneo la Hekalu na akaanza kufundisha humo. Viongozi wa makuhani na viongozi wa wazee wakamjia. Wakasema, “Tuambie! Una mamlaka gani ya kufanya mambo haya unayofanya? Na nani amekupa mamlaka hii?”

24 Yesu akajibu, “Nitawauliza swali pia. Mkinijibu, ndipo nitawaambia nina mamlaka gani ya kufanya mambo haya. 25 Niambieni: Yohana alipowabatiza watu, mamlaka yake ilitoka kwa Mungu au kwa wanadamu?”

Makuhani na viongozi wa Kiyahudi wakajadiliana kuhusu swali la Yesu, wakasemezana, “Tukisema, ‘Ubatizo wa Yohana ulitoka kwa Mungu,’ atasema, ‘Sasa kwa nini hamkumwamini Yohana?’ 26 Lakini hatuwezi kusema ubatizo wa Yohana ulitoka kwa watu wengine. Tunawaogopa watu, kwa sababu wote wanaamini kuwa Yohana alikuwa nabii.”

27 Hivyo wakamwambia Yesu, “Hatujui jibu.”

Yesu akasema, “Basi hata mimi siwaambii aliyenipa mamlaka ya kufanya mambo haya.”

Yesu Atumia Simulizi Kuhusu Wana Wawili

28 “Niambieni mnafikiri nini kuhusu hili: Alikuwepo mtu mwenye wana wawili. Alimwendea mwanaye wa kwanza na kumwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’

29 Mwanaye akasema, ‘Siendi.’ Lakini baadaye akabadili uamuzi wake na akaenda.

30 Kisha baba akamwendea mwanaye mwingine na kumwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’ Akajibu, ‘Sawa baba, nitakwenda kufanya kazi.’ Lakini hakwenda.

31 Ni yupi kati ya wana hawa wawili alimtii baba yake?”

Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Ni mwana wa kwanza.”

Yesu akawaambia, “Ukweli ni huu, ninyi ni wabaya kuliko watoza ushuru na makahaba. Ukweli ni kuwa hao wataingia katika ufalme wa Mungu kabla yenu. 32 Yohana alikuja akiwaonesha njia sahihi ya kuishi, na hamkumwamini. Lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini Yohana. Mliona yaliyotokea, lakini hamkubadilika na mlikataa kumwamini.

Yesu Atoa Simulizi Kuhusu Shamba la Mzabibu

(Mk 12:1-12; Lk 20:9-19)

33 Sikilizeni simulizi hii: Alikuwepo mtu aliyemiliki shamba la mizabibu. Alijenga uzio kuzunguka shamba lile la mizabibu na akachimba shimo kwa ajili ya kukamulia zabibu.[d] Kisha akajenga mnara wa lindo. Akalikodisha shamba kwa wakulima kisha akasafiri. 34 Wakati wa kuvuna zabibu ulipofika, akawatuma watumishi wake waende kwa wakulima ili apate gawio lake la zabibu.

35 Lakini wakulima waliwakamata wale watumishi na kumpiga mmoja wao. Wakamwua mwingine na wa tatu wakampiga kwa mawe mpaka akafa. 36 Hivyo mwenye shamba akawatuma baadhi ya watumishi wengine wengi zaidi ya aliowatuma hapo kwanza. Lakini wakulima wakawatendea kama walivyowatendea watumishi wa kwanza. 37 Hivyo mwenye shamba akaamua kumtuma mwanaye kwa wakulima. Alisema, ‘Wakulima watamheshimu mwanangu.’

38 Lakini wakulima walipomwona mwanaye, wakaambizana, ‘Huyu ni mwana wa mwenye shamba. Shamba hili litakuwa lake. Tukimwua, shamba la mizabibu litakuwa letu.’ 39 Hivyo wakulima wakamchukua mwana wa mwenye shamba, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu na kumwua.

40 Hivyo mmiliki wa shamba la mizabibu atawafanya nini wakulima hawa atakaporudi?”

41 Makuhani wa Kiyahudi na viongozi wakasema, “Kwa hakika atawaua watu hao waovu. Kisha atawakodishia wakulima wengine shamba hilo, watakaompa gawio la mazao yake wakati wa mavuno.”

42 Yesu akawaambia, “Hakika mmesoma hili katika Maandiko:

‘Jiwe walilolikataa waashi
    limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Bwana amefanya hivi,
    na ni ajabu kubwa kwetu kuliona.’(F)

43 Hivyo ninawaambia kuwa, ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na watapewa watu wanaofanya mambo anayoyataka Mungu katika ufalme wake. 44 Kila aangukaye kwenye jiwe hili atavunjika na litamsaga kila linayemwangukia.”[e]

45 Viongozi wa makuhani na Mafarisayo waliposikia simulizi hizi, wakajua kuwa Yesu alikuwa anawasema wao. 46 Walitaka kumkamata Yesu. Lakini waliogopa kwani watu waliamini kuwa Yesu ni nabii.

Error: Book name not found: Neh for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Matendo 21

Paulo Aenda Yerusalemu

21 Baada ya kuwaaga wazee tulitweka tanga moja kwa moja kwenda kwenye kisiwa cha Kosi. Siku iliyofuata tulikwenda kisiwa cha Rhode na kutoka pale tulikwenda Patara. Tulipata meli hapo iliyokuwa inakwenda maeneo ya Foeniki. Tukapanda meli na tukatweka tanga kuondoka.

Tulitweka tanga na kusafiri karibu na kisiwa cha Kipro. Tuliweza kukiona upande wa kaskazini, lakini hatukusimama. Tulisafiri mpaka katika jimbo la Shamu. Tulisimama Tiro kwa sababu meli ilitakiwa kupakua mizigo yake pale. Tuliwapata wafuasi wa Bwana pale na tukakaa pamoja nao kwa siku saba. Walimuonya Paulo asiende Yerusalemu kwa sababu ya kile walichoambiwa na Roho Mtakatifu. Lakini muda wetu wa kukaa pale ulipokwisha, tulirudi kwenye meli na kuendelea na safari yetu. Wafuasi wote, hata wanawake na watoto walikuja pamoja nasi pwani. Tulipiga magoti ufukweni sote, tukaomba, na tukaagana. Kisha tukaingia melini, na wafuasi wa Bwana wakarudi nyumbani.

Tuliendelea na safari yetu kutoka Tiro na kwenda katika mji wa Ptolemai. Tuliwasalimu waamini pale na kukaa nao kwa siku moja. Siku iliyofuata tuliondoka Ptolemai na kwenda katika mji wa Kaisaria. Tulikwenda nyumbani kwa Filipo na kukaa kwake, alikuwa mhubiri wa Habari Njema. Alikuwa mmoja wa wasaidizi saba.[a] Alikuwa na mabinti wanne mabikira waliokuwa na karama ya kutabiri.

10 Baada ya kuwa pale kwa siku kadhaa, nabii aliyeitwa Agabo alikuja kutoka Uyahudi. 11 Alikuja Kwetu na kuazima mkanda wa Paulo. Aliutumia mkanda huo na akajifunga mikono na miguu yake mwenyewe. Kisha akasema, “Roho Mtakatifu ananiambia, ‘Hivi ndivyo ambavyo Wayahudi walioko Yerusalemu watamfunga mtu anayeuvaa mkanda[b] huu. Kisha watamkabidhi kwa watu wasiomjua Mungu.’”

12 Tuliposikia hili, sisi na wafuasi wengine pale tukamsihi Paulo asiende Yerusalemu. 13 Lakini Paulo alisema, “Kwa nini mnalia na kunihuzunisha? Niko radhi kufungwa Yerusalemu. Niko tayari hata kufa kwa ajili ya jina la Bwana Yesu!”

14 Hatukuweza kumshawishi asiende Yerusalemu. Hivyo tuliacha kumsihi na tukasema, “Tunaomba lile alitakalo Bwana lifanyike.”

15 Baada ya hili, tulijiandaa na kuelekea Yerusalemu. 16 Baadhi ya Wafuasi wa Yesu kutoka Kaisaria walikwenda pamoja nasi. Wafuasi hawa walitupeleka nyumbani kwa Mnasoni, mtu kutoka Kipro, ambaye alikuwa mmoja wa watu wa kwanza kuwa wafuasi wa Yesu. Walitupeleka nyumbani kwake ili tukae pamoja naye.

Paulo Amtembelea Yakobo

17 Ndugu na dada wa Yerusalemu walitukabisha kwa furaha sana walipotuona. 18 Siku iliyofuata Paulo alikwenda pamoja nasi kumtembelea Yakobo. Wazee wote walikuwepo pia. 19 Baada ya kuwasalimu, Paulo aliwaambia hatua kwa hatua yote ambayo Mungu aliyatenda katikati ya watu wasio Wayahudi kupitia huduma yake.

20 Viongozi waliposikia hili, wakamsifu Mungu. Kisha wakamwambia Paulo, “Ndugu yetu, unaweza kuona maelfu ya Wayahudi wamekuwa waamini, lakini wanadhani ni muhimu kutii Sheria ya Musa. 21 Wameambiwa kuwa unawafundisha Wayahudi wanaoishi katika majimbo yasiyo ya Kiyahudi kuacha kufuata Sheria ya Musa. Wamesikia kuwa unawaambia wasiwatahiri watoto wao na wasifuate desturi zetu.

22 Tufanye nini? Wafuasi wayahudi hapa watajua kuwa umekuja. 23 Hivyo tutakwambia nini cha kufanya: Watu wanne miongoni mwa watu wetu wameweka nadhiri[c] kwa Mungu. 24 Wachukue watu hawa walio pamoja nawe na ushiriki katika ibada ya utakaso.[d] Lipia gharama zao ili wanyoe nywele za vichwa vyao. Hili litathibitisha kwa kila mmoja kuwa mambo waliyosikia kuhusu wewe si sahihi. Watajua kuwa wewe mwenyewe unaitii Sheria ya Musa katika maisha yako.

25 Tumekwisha watumia barua waamini wasio Wayahudi kuwaambia ambayo hawapaswi kufanya:

‘Wasile chakula kilichotolewa kwa sanamu.

Wasile nyama inayotokana na wanyama walionyongwa au nyama zilizo na damu ndani yake.

Wasijihusishe na uzinzi.’”

Paulo Akamatwa

26 Hivyo Paulo akawachukua wale watu wanne aliokuwa pamoja nao. Siku iliyofuata alishiriki kwenye ibada ya kuwatakasa. Kisha akaenda eneo la Hekalu na kutangaza siku ya mwisho ambapo kipindi cha utakaso kitakwisha na kwamba sadaka ingetolewa kwa ajili ya kila mmoja wa watu hao siku hiyo.

27 Siku saba zilipokuwa zinakaribia kumalizika, baadhi ya Wayahudi kutoka Asia walimwona Paulo katika eneo la Hekalu. Wakamshawishi kila mtu, kisha wakakusanyika kama kundi wakiwa na hasira, kisha wakamkamata Paulo 28 na wakapiga kelele wakisema, “Watu wa Israeli, tusaidieni! Huyu ndiye mtu anayefundisha mambo yaliyo kinyume na Sheria ya Musa, kinyume na watu wetu, na kinyume na Hekalu letu. Hivi ndivyo anavyowafundisha watu kila mahali. Na sasa amewaleta baadhi ya Wayunani katika eneo la Hekalu na amepanajisi mahali hapa patakatifu!” 29 (Wayahudi walisema hili kwa kuwa walimwona Trofimo akiwa na Paulo Yerusalemu. Trofimo alikuwa mwenyeji wa Efeso, Wayahudi walidhani kuwa Paulo alikuwa amempeleka eneo takatifu la Hekalu.)

30 Watu katika mji wote wakajaa hasira, na kila mtu akaja akikimbilia kwenye Hekalu. Wakamkamata Paulo na kumtoa nje ya eneo takatifu, malango ya Hekalu yakafungwa saa hiyo hiyo. 31 Walipokuwa wanajaribu kumwua Paulo, Kamanda wa jeshi la Rumi katika mji wa Yerusalemu akapata taarifa kuwa ghasia zilikuwa zimeenea mji wote. 32 Mara hiyo hiyo kamanda alikimbilia mahali ambako umati wa watu ulikuwa umekusanyika, aliwachukua baadhi ya maofisa wa jeshi na askari. Watu walipomwona kamanda na askari wake waliacha kumpiga Paulo.

33 Kamanda alikwenda mahali alipokuwa Paulo na akamkamata. Akawaambia askari wake wamfunge kwa minyororo miwili. Kisha akauliza, “Mtu huyu ni nani? Amefanya nini kibaya?” 34 Baadhi ya watu pale walipiga kelele wakisema kitu hiki na wengine walisema kingine. Kwa sababu ya kuchanganyikiwa huku na kelele kamanda hakujua ukweli kuhusu kilichotokea. Hivyo akawaambia askari wamchukue Paulo mpaka kwenye jengo la jeshi. 35-36 Umati wote ulikuwa unawafuata. Askari walipofika kwenye ngazi ilibidi wambebe Paulo. Walifanya hivi ili kumlinda, kwa sababu watu walikuwa tayari kumwumiza. Watu walikuwa wanapiga kelele wakisema, “Auawe!”

37 Askari walipokuwa tayari kumwingiza Paulo kwenye jengo la jeshi, Paulo alimwuliza kamanda akasema, “Je, ninaweza kukwambia kitu?”

Kamanda akasema, “Kumbe, unaongea Kiyunani? 38 Kwa hiyo wewe si mtu niliyemdhania. Nilidhani wewe ni Mmisri aliyeanzisha vurugu dhidi ya serikali siku si nyingi na akawaongoza magaidi elfu nne kwenda jangwani.”

39 Paulo akasema, “Hapana, Mimi ni Myahudi kutoka Tarso katika jimbo la Kilikia. Ni raia wa mji ule muhimu. Tafadhali niruhusu niseme na watu.”

40 Kamanda akamwambia Paulo unaweza kusema. Hivyo Paulo akasimama kwenye ngazi na kupunga mkono wake ili watu wanyamaze. Watu walinyamaza na Paulo akaanza kusema nao kwa Kiaramu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International