M’Cheyne Bible Reading Plan
Sheria ya Mungu na Desturi za Kibinadamu
(Mk 7:1-23)
15 Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria kutoka Yerusalemu walimjia Yesu na kumwuliza, 2 “Kwa nini wafuasi wako hawatii desturi tulizorithi kutoka kwa viongozi wetu wakuu walioishi hapo zamani? Wafuasi wako hawanawi mikono kabla ya kula!”
3 Yesu akajibu, “Na kwa nini mnakataa kutii amri ya Mungu ili muweze kuzifuata desturi zenu? 4 Mungu alisema, ‘Ni lazima umtii baba na mama yako.’(A) Na Mungu alisema pia kuwa, ‘Kila anayemnenea vibaya mama au baba yake lazima auawe.’(B) 5 Lakini mnafundisha kuwa mtu anaweza kumwambia baba au mama yake, ‘Nina kitu ninachoweza kukupa kukusaidia, Lakini sitakupa, bali nitampa Mungu.’ 6 Mnawafundisha kutowatii baba zao. Hivyo mnafundisha kuwa si muhimu kufanya kile alichosema Mungu. Mnadhani ni muhimu kufuata mila na desturi zenu mlizonazo. 7 Enyi wanafiki! Isaya alikuwa sahihi alipozungumza kwa niaba ya Mungu kuhusu ninyi aliposema:
8 ‘Watu hawa wananiheshimu kwa maneno tu,
lakini mimi si wa muhimu kwao.
9 Ibada zao kwangu hazina maana.
Wanafundisha kanuni za kibinadamu tu.’”(C)
10 Yesu akawaita watu. Akasema, “Sikieni na mwelewe nitakachosema. 11 Si chakula kinachoingia mdomoni kinachomtia mtu unajisi,[a] bali kile kinachomtoka mdomoni mwake.” 12 Kisha wafuasi wakamjia na kumwuliza, “Unajua kuwa Mafarisayo wamekasirika kutokana na yale uliyosema?”
13 Yesu akajibu, “Kila mti ambao haukupandwa na Baba yangu wa mbinguni utang'olewa. 14 Kaeni mbali na Mafarisayo. Wanawaongoza watu, lakini ni sawa na wasiyeona wanaowaongoza wasiyeona wengine. Na kama asiyeona akimwongoza asiyeona mwingine, wote wawili wataangukia shimoni.”
15 Petro akasema, “Tufafanulie yale uliyosema awali kuhusu kile kinachowatia watu najisi.”
16 Yesu akasema, “Bado mna matatizo ya kuelewa? 17 Hakika mnajua kuwa vyakula vyote vinavyoingia kinywani huenda tumboni. Kutoka huko hutoka nje ya mwili. 18 Lakini mambo mabaya ambayo watu wanasema kwa vinywa vyao hutokana na mawazo yao. Na hayo ndiyo yanayoweza kumtia mtu unajisi. 19 Mambo mabaya haya yote huanzia akilini: mawazo maovu, mauaji, uzinzi, uasherati, wizi, uongo, na matukano. 20 Haya ndiyo mambo yanayowatia watu unajisi. Kula bila kunawa mikono hakuwezi kuwafanya watu wasikubaliwe na Mungu.”
Yesu Amsaidia Mwanamke Asiye Myahudi
(Mk 7:24-30)
21 Kutoka pale, Yesu alikwenda maeneo ya Tiro na Sidoni. 22 Mwanamke Mkanaani kutoka eneo hilo akatokea na kuanza kupaza sauti, “Bwana, Mwana wa Daudi, tafadhali nisaidie! Binti yangu ana pepo ndani yake, na anateseka sana.”
23 Lakini Yesu hakumjibu. Hivyo wanafunzi wake wakamwendea Yesu na kumwambia, “Mwambie aondoke, anaendelea kupaza sauti na hatatuacha.”
24 Yesu akajibu, “Mungu alinituma niwasaidie kondoo wa Mungu waliopotea, watu wa Israeli.”[b]
25 Ndipo mwanamke alikuja mahali alipokuwa Yesu na kuinama mbele yake. Akasema, “Bwana, nisaidie!”
26 Akamjibu kwa kumwambia, “Si sahihi kuwapa mbwa mkate wa watoto.”
27 Mwanamke akasema, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula vipande vya chakula vinavyoanguka kutoka kwenye meza za mabwana zao.”
28 Kisha Yesu akamjibu, “Mwanamke, una imani kuu! Utapata ulichoomba.” Wakati huo huo binti wa yule mwanamke akaponywa.
Yesu Awaponya Watu Wengi
29 Kisha Yesu akatoka pale na kwenda pwani ya Ziwa Galilaya. Alipanda vilima na akaketi chini.
30 Kundi kubwa la watu likamwendea. Walileta watu wengine wengi waliokuwa wagonjwa na kuwaweka mbele yake. Walikuwepo watu wasioweza kutembea, wasiyeona, walemavu wa miguu, wasiyesikia na wengine wengi. 31 Watu walishangaa walipoona kuwa waliokuwa wasiyesema walianza kusema, walemavu wa miguu waliponywa, waliokuwa hawawezi kutembea waliweza kutembea, wasiyeona waliweza kuona. Kila mtu alimshukuru Mungu wa Israeli kwa hili.
Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 4,000
(Mk 8:1-10)
32 Kisha Yesu akawaita wafuasi wake na kuwaambia, “Ninawaonea huruma watu hawa. Wamekuwa pamoja nami kwa siku tatu, na sasa hawana chakula. Sitaki niwaache waende wakiwa na njaa. Wanaweza kuzimia njiani wanaporudi nyumbani.”
33 Wafuasi wakamwuliza Yesu, “Tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha watu wote hawa? Tuko nyikani mbali ni miji.”
34 Yesu akawauliza, “Mna mikate mingapi?”
Wakamjibu, “Tuna mikate saba na samaki wadogo wachache.”
35 Yesu akawaambia watu waketi chini. 36 Akaichukua mikate saba na samaki. Akamshukuru Mungu kwa sababu ya chakula. Akaigawa vipande vipande, akawapa wafuasi wake na wafuasi wakawapa watu chakula. 37 Watu wote walikula mpaka wakashiba. Baada ya hili, wafuasi walijaza vikapu saba kwa vipande vya chakula vilivyosalia ambavyo havikuliwa. 38 Walikuwepo wanaume 4,000 pale waliokula. Walikuwepo pia wanawake na watoto. 39 Baada ya wote kula, Yesu akawaambia watu wanaweza kwenda nyumbani. Alipanda mashua na kwenda eneo la Magadani.
Mkutano Yerusalemu
15 Kisha baadhi ya watu kutoka Uyahudi wakaja Antiokia na kuanza kuwafundisha jamii ya waamini wasio Wayahudi, wakisema, “Hamwezi kuokolewa ikiwa hamkutahiriwa kama Musa alivyotufundisha.” 2 Paulo na Barnaba wakayapinga mafundisho haya na wakahojiana na kubishana na watu hawa juu ya hili. Hivyo kundi la waamini likaamua kuwatuma Paulo, Barnaba, na baadhi ya watu wengine Yerusalemu ili kujadiliana na mitume na wazee kuhusu suala hili.
3 Kanisa liliwapa wale waliotumwa kila kitu walichohitaji kwa ajili ya safari yao. Walisafiri kupitia maeneo ya Foeniki na Samaria, ambako walieleza kwa undani mambo yote namna ambavyo wasio Wayahudi wamemgeukia Mungu wa kweli. Habari hii iliwafurahisha waamini wote. 4 Walipofika Yerusalemu, mitume, wazee na kanisa lote waliwakaribisha. Paulo, Barnaba, na wengine wakaeleza yote ambayo Mungu alitenda kupitia wao. 5 Baadhi ya waamini mjini Yerusalemu waliokuwa Mafarisayo,[a] walisimama na kusema, “Waamini wasio Wayahudi lazima watahiriwe. Ni lazima tuwaambie waitii Sheria ya Musa!”
6 Ndipo mitume na wazee wakakusanyika kulichunguza jambo hili. 7 Baada ya majadiliano ya muda mrefu, Petro akasimama na kuwaambia, “Ndugu zangu, nina uhakika mnakumbuka kilichotokea siku za nyuma. Mungu alinichagua kutoka miongoni mwenu kuzihubiri Habari Njema kwa watu wasio Wayahudi. Kupitia mimi walisikia Habari Njema na kuamini. 8 Mungu anamfahamu kila mtu, hata mawazo yao, na amewakubali watu hawa wasio Wayahudi. Amelionyesha hili kwetu kwa kuwapa Roho Mtakatifu kama alivyotupa sisi. 9 Mbele za Mungu, wasio Wayahudi hawako tofauti na sisi. Mungu aliisafisha mioyo yao walipoamini. 10 Kwa nini sasa mnawatwisha mzigo mzito kwenye shingo zao? Je, mnajaribu kumkasirisha Mungu? Sisi na baba zetu hatukuweza kuubeba mzigo huo. 11 Hapana, tunaamini kuwa sisi na watu hawa tutaokolewa kwa namna moja iliyo sawa, ni kwa neema ya Bwana Yesu.”
12 Ndipo kundi lote likawa kimya. Waliwasikiliza Paulo na Barnaba walipokuwa wanaeleza kuhusu ishara na maajabu ambayo kupitia wao Mungu aliwatendea watu wasio Wayahudi. 13 Walipomaliza kusema, Yakobo akasema, “Ndugu zangu, nisikilizeni. 14 Simoni Petro ametueleza namna ambavyo siku za mwanzoni Mungu alilionyesha pendo lake kwa watu wasio Wayahudi, kwa kuwakubali na kuwafanya kuwa watu wake. 15 Maneno ya manabii yanakubaliana na hili:
16 ‘Nitarudi baada ya hili.
Nitaijenga nyumba ya Daudi tena.
Imeanguka chini.
Nitazijenga tena sehemu za nyumba yake zilizoangushwa chini.
Nitaifanya nyumba yake kuwa mpya.
17 Kisha wanadamu wengine wote,
watu niliowachagua kutoka mataifa mengine,
watataka kunifuata mimi, Bwana.
Hivi ndivyo Bwana anasema,
naye ndiye afanyaye mambo haya yote.’(A)
18 ‘Haya yote yalijulikana tangu zamani.’[b]
19 Hivyo nadhani tusiyafanye mambo kuwa magumu kwa wasio Wayahudi waliomgeukia Mungu. 20 Badala yake, tuwatumie barua kuwaambia mambo ambayo hawapaswi kutenda:
Wasile chakula kilichotolewa kwa sanamu maana chakula hiki huwa najisi.[c]
Wasijihusishe na dhambi ya zinaa.
Wasile nyama inayotokana na wanyama walionyongwa au nyama ambayo bado ina damu ndani yake.
21 Wasitende mojawapo ya mambo haya, kwa sababu bado kuna watu katika kila mji wanaofundisha Sheria ya Musa. Maneno ya Musa yamekuwa yakisomwa katika masinagogi kila siku ya Sabato kwa miaka mingi.”
Barua kwa Waamini Wasio Wayahudi
22 Mitume, wazee na kanisa lote wakataka kuwatuma baadhi ya watu wafuatane na Paulo na Barnaba kwenda Antiokia. Wakawachagua baadhi ya watu kutoka miongoni mwao wenyewe. Waliwachagua Yuda (ambaye pia aliitwa Barsaba) na Sila, watu walioheshimiwa na waamini. 23 Kundi la waamini likaandika barua na kuwatuma watu hawa. Barua ilisema:
Kutoka kwa mitume na wazee, ndugu zenu.
Kwa ndugu wote wasio Wayahudi katika mji wa Antiokia na katika majimbo ya Shamu na Kilikia.
Ndugu Wapendwa:
24 Tumesikia kuwa baadhi ya watu kutoka kwetu walikuja kwenu. Walichosema kiliwasumbua na kuwaudhi. Lakini hatukuwaambia kufanya hili. 25 Sisi sote tumekubaliana kuwachagua baadhi ya watu na kuwatuma kwenu. Watakuwa na rafiki zetu wapendwa, Barnaba na Paulo. 26 Barnaba na Paulo wameyatoa maisha yao kumtumikia Bwana wetu Yesu Kristo. 27 Hivyo tumewatuma Yuda na Sila pamoja nao. Watawaambia mambo yanayofanana. 28 Imempendeza Roho Mtakatifu na sisi kwamba tusiwatwishe mizigo ya ziada, isipokuwa kwa mambo haya ya muhimu:
29 Msile chakula kilichotolewa kwa sanamu.
Msile nyama inayotokana na wanyama walionyongwa au nyama ambayo bado ina damu ndani yake.
Msijihusishe na uzinzi.
Mkijitenga na mambo haya, mtakuwa mnaenenda vyema.
Wasalamu.
30 Hivyo Paulo, Barnaba, Yuda, na Sila waliondoka Yerusalemu na kwenda Antiokia. Walipofika huko walilikusanya kundi la waamini pamoja na wakawapa barua. 31 Waamini walipoisoma, wakafurahi na kufarijika. 32 Yuda na Sila ambao pia walikuwa manabii, waliwatia moyo waamini kwa maneno mengi na kuwafanya waimarike katika imani yao. 33 Baada ya Yuda na Sila kukaa pale kwa muda, waliondoka. Waamini waliwaruhusu waende kwa amani kisha wakarudi Yerusalemu kwa wale waliowatuma. 34 [d]
35 Lakini Paulo na Barnaba walikaa Antiokia. Wao na wengine wengi waliwafundisha waamini na kuwahubiri watu wengine Habari Njema kuhusu Bwana.
Paulo na Barnaba Watengana
36 Wakati fulani baadaye, Paulo akamwambia Barnaba, “Turudi katika miji yote tulikowahubiri watu ujumbe wa Bwana. Tuwatembelee waamini tuone wanaendeleaje.”
37 Barnaba alitaka Yohana Marko afuatane nao pia. 38 Lakini Yohana Marko hakukaa nao mpaka mwisho katika safari ya kwanza. Aliwaacha Pamfilia. Hivyo Paulo alisisitiza kuwa wasiende pamoja naye wakati huu. 39 Paulo na Barnaba walikuwa na mjadala mkali kuhusu hili. Ulikuwa mbaya sana ikabidi watengane na kwenda njia tofauti. Barnaba akatweka tanga kwenda Kipro, akamchukua Marko pamoja naye.
40 Paulo alimchagua Sila kwenda naye. Waamini Antiokia walimweka Paulo katika uangalizi wa Bwana na kumtuma. 41 Paulo na Sila walikwenda kwa kupitia katika majimbo ya Shamu na Kilikia, wakiyasaidia makanisa kuimarika.
© 2017 Bible League International