Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

M’Cheyne Bible Reading Plan

The classic M'Cheyne plan--read the Old Testament, New Testament, and Psalms or Gospels every day.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Error: Book name not found: Gen for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Marko 2

Yesu Amponya Aliyepooza

(Mt 9:1-8; Lk 5:17-26)

Siku chache baadaye Yesu alirudi Kapernaumu na habari zikaenea kuwa yupo nyumbani. Hivyo watu wengi walikusanyika kumsikiliza akifundisha na haikuwapo nafasi iliyobaki kabisa ndani ya nyumba, hata nje ya mlango. Yesu alipokuwa akifundisha, baadhi ya watu walimleta kwake mtu aliyepooza amwone. Mtu huyo alikuwa amebebwa na rafiki wanne. Watu hao hawakuweza kumfikisha mgonjwa kwa Yesu kwa sababu ya umati wa watu ulioijaza nyumba yote. Hivyo walipanda na kuondoa paa juu ya sehemu aliposimama Yesu. Baada ya kutoboa tundu darini[a] kwenye paa, wakateremsha kirago alimokuwa amelala yule aliyepooza. Yesu alipoona imani waliyokuwa nayo wale waliomleta na yule mwenye kupooza, alimwambia, “Mtoto wangu, dhambi zako zimesamehewa.”

Baadhi ya walimu wa sheria walikuwa wamekaa pale. Nao waliona kile alichokifanya Yesu na wakawaza miongoni mwa wenyewe, “Kwa nini mtu huyu anasema maneno kama hayo? Si anamtukana Mungu! Kwani hakuna awezaye kusamehe dhambi ila Mungu.”

Mara moja Yesu alifahamu walichokuwa wakikifikiri wale walimu wa sheria, hivyo akawaambia, “Kwa nini mna maswali kama hayo mioyoni mwenu? Wakati akiwa duniani Mwana wa Adamu anayo mamlaka ya kusamehe dhambi. Lakini nitawezaje kulithibitisha hili kwenu? Pengine mnafikiri ilikuwa rahisi kwangu kumwambia mtu huyu aliyepooza ‘Dhambi zako zimesamehewa,’ kwa sababu hilo haliwezi kuthibitishwa kwamba hakika limetokea. Lakini vipi nikimwambia mtu huyu, ‘Simama! Beba kirago chako na utembee’? 10 Hapo ndipo mtakapoweza kuona kama kweli ninayo mamlaka hayo ama sina!” Kwa hiyo Yesu akamwambia mtu yule aliyepooza, “Nitalithibitishaje hili kwako? 11 Ninakwambia hivi, ‘Inuka! Beba kirago chako uende nyumbani!’”

12 Yule mtu aliyepooza alisimama na bila kusita, akabeba kirago chake na akatoka nje ya nyumba wakati kila mmoja akiona. Matokeo yake ni kuwa wote walishangazwa na mambo hayo. Wakamsifu Mungu na kusema, “Hatujawahi kuona kitu kama hiki!”

Lawi (Mathayo) Amfuata Yesu

(Mt 9:9-13; Lk 5:27-32)

13 Mara nyingine tena Yesu akaelekea kandoni mwa ziwa, na watu wengi walikuwa wakimwendea, naye akawafundisha. 14 Alipokuwa akitembea kando ya ufukwe wa ziwa, alimwona Lawi mwana wa Alfayo ameketi katika mahala pake pa kukusanyia kodi. Yesu akamwambia, “Nifuate!” Hivyo Lawi akainuka na kumfuata.

15 Baadaye Yesu na wafuasi wake wa karibu walikuwa wakila chakula cha jioni nyumbani kwa Lawi. Wakusanya kodi wengi na watu wengine wenye sifa mbaya nao wakamfuata Yesu. Hivyo wengi wao walikuwa wakila pamoja na Yesu na wanafunzi wake. 16 Baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa pamoja na Mafarisayo walipomwona Yesu akila na wenye dhambi na wanaokusanya kodi, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini Yesu anakula na wenye kukusanya kodi na watu wengine wenye dhambi?”

17 Yesu alipolisikia hili akawaambia, “Wale walio wagonjwa ndio wanaomhitaji daktari si wale walio wazima wa afya. Mimi nimekuja kuwakaribisha wenye dhambi waje kwangu sikuja kwa ajili ya wale wanaotenda kila kitu kwa haki.”

Swali Kuhusu Kufunga

(Mt 9:14-17; Lk 5:33-39)

18 Siku moja wafuasi wa Yohana Mbatizaji na Mafarisayo walikuwa wanafunga. Baadhi ya watu walimjia Yesu na kumwuliza, “Mbona wafuasi wa Yohana na wafuasi wa Mafarisayo wanafunga, lakini kwa nini wanafunzi wako hawafungi.”

19 Yesu akawajibu, “Katika sherehe ya arusi hutarajii marafiki wa bwana arusi wawe na huzuni wakati yeye mwenyewe yupo pamoja nao. Hakika hawatafunga ikiwa bwana arusi bado yuko pamoja nao. 20 Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao, na wakati huo ndipo watakapofunga.

21 Hakuna anayeshona kiraka kipya cha nguo kwenye vazi la zamani. Ikiwa atafanya hivyo kiraka hicho kipya kitajikunjakunja na kulinyofoa vazi hilo zee nalo litachanika vibaya zaidi. 22 Vivyo hivyo hakuna awekaye divai mpya ndani ya viriba vya zamani[b] vilivyozeeka. Akifanya hivyo, divai ile itachacha na hewa yake itavipasua vibuyu hivyo vya ngozi na kuviharibu kabisa pamoja na divai yenyewe. Badala yake mtu anaweka divai mpya ndani ya vibuyu vipya vya ngozi vya kuwekea divai.”

Yesu ni Bwana Juu ya Siku ya Sabato

(Mt 12:1-8; Lk 6:1-5)

23 Ikatokea kwamba katika siku ya Sabato Yesu na wanafunzi wake walikuwa wakipita katika mashamba ya nafaka. Wanafunzi wake walianza kuchuma masuke ya nafaka ile walipopita. 24 Baadhi ya Mafarisayo walipoliona hilo wakamwambia Yesu, “Tazama, kwa nini wanafunzi wako wanafanya hivi? Ni kinyume cha sheria kuchuma masuke ya nafaka katika siku ya Sabato?”

25 Yesu akajibu, “Hakika mmesoma kile alichofanya Daudi pale yeye pamoja na watu aliokuwa nao walipopata njaa na kuhitaji chakula. 26 Ilikuwa wakati wa Abiathari Kuhani Mkuu. Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu na kula mkate uliotolewa kwa Bwana. Sheria ya Musa inasema ni makuhani peke yao ndio watakaoweza kuula mkate ule. Daudi aliwapa pia ule mkate mtakatifu watu waliokuwa pamoja naye.”

27 Ndipo Yesu akawaambia mafarisayo, “Siku ya Sabato ilifanywa kwa faida ya watu. Watu hawakuumbwa ili watawaliwe na Sabato. 28 Kwa hiyo Mwana wa Adamu ambaye ni Bwana juu ya kila kitu, pia ni Bwana juu ya siku ya Sabato.”

Error: Book name not found: Esth for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Warumi 2

Huwezi Kuwahukumu Wengine

Je, unadhani unaweza kuwahukumu watu wengine? Unakosea. Wewe pia una hatia ya dhambi. Unawahukumu kwa kuwa wanatenda mabaya, lakini wewe unatenda yale wanayotenda. Hivyo unapowahukumu, unajihukumu wewe mwenyewe. Lakini tunajua kwamba Mungu yuko sahihi kwa kuwahukumu wote wanaotenda mambo ya jinsi hiyo! Lakini kwa kuwa unatenda mambo sawa na wale unaowahukumu, hakika unaelewa kuwa Mungu atakuadhibu nawe pia. Unawezaje kufikiri kuwa utaiepuka hukumu yake? Mungu amekuwa mwema kwako. Na amekuwa mvumilivu sana, akisubiri ubadilike. Lakini haufikirii jambo lolote kuhusu wema wake mkuu. Pengine huelewi kwamba Mungu ni mwema kwako ili ubadili moyo na maisha yako.

Lakini wewe ni mkaidi sana! Unakataa kubadilika. Hivyo unaikuza hukumu yako wewe mwenyewe zaidi na zaidi. Utahukumiwa siku ile ambapo Mungu ataonesha hasira yake. Siku ambayo kila mtu ataona Mungu anavyowahukumu watu kwa haki.[a] Kama anavyosema, “Atamlipa au kumwadhibu kila mtu kutokana na matendo yale.”(A) Watu wengine hawachoki kutenda mema. Wanaishi kwa ajili ya utukufu na heshima kutoka kwa Mungu na kwa ajili ya maisha yasiyoweza kuharibiwa. Mungu atawapa watu hao uzima wa milele. Lakini wengine hutenda mambo yanayowafurahisha wao wenyewe. Hivyo hukataa yaliyo haki na huchagua kutenda mabaya. Watateseka kwa hukumu ya Mungu yenye hasira. Matatizo na mateso yatampata kila mmoja anayetenda uovu; kuanzia Wayahudi kwanza kisha wale wasio Wayahudi. 10 Lakini atampa utukufu, heshima na amani kila atendaye mema; wale wote wanaotenda mema; kuanzia Wayahudi kwanza kisha wale wasio Wayahudi. 11 Ndiyo, Mungu humhukumu kila mtu pasipo upendeleo, bila kujali yeye ni nani.

12 Watu walio na sheria na wote ambao hawajawahi kuisikia sheria, wote wako sawa wanapotenda dhambi. Watu wasio na sheria na ni watenda dhambi wataangamizwa. Vivyo hivyo, wale walio na sheria na ni watenda dhambi watahukumiwa kuwa na hatia kwa kutumia sheria. 13 Kuisikia sheria hakuwafanyi watu wawe wenye haki kwa Mungu. Wanakuwa wenye haki mbele zake, pale wanapotekeleza kile kinachoagizwa na sheria.

14 Fikirini kuhusu wasio Wahayudi ambao hawakukua wakiwa na sheria. Wanapotenda kama sheria inavyoamuru,[b] wanakuwa kielelezo cha sheria, ijapokuwa hawana sheria iliyoandikwa. 15 Wanaonesha kuwa wanafahamu kilicho sahihi na kibaya, kama sheria inavyoamuru na dhamiri zao zinakubali. Lakini wakati mwingine mawazo yao huwaambia kuwa wamekosea au wamefanya sahihi. 16 Hivi ndivyo itakavyokuwa siku ambayo Mungu atazihukumu siri za watu kupitia Yesu Kristo, sawasawa na Habari Njema ninayoihubiri.

Wayahudi na Sheria

17 Wewe unajiita Myahudi, na unajiona upo salama kwa kuwa tu una sheria. Kwa majivuno unadai kuwa wewe ni mmoja wa wateule wa Mungu. 18 Unajua yale ambayo Mungu anataka ufanye. Na unajua yaliyo muhimu, kwa sababu umejifunza sheria. 19 Unadhani kuwa wewe ni kiongozi wa watu wasioweza kuiona njia sahihi, na nuru kwa wale walio gizani. 20 Unafikiri unaweza kuwaonesha wajinga kilicho sahihi. Na unadhani kuwa wewe ni mwalimu wa wanaoanza kujifunza. Unayo sheria, na hivyo unadhani unajua kila kitu na una kweli yote. 21 Unawafundisha wengine, sasa kwa nini usijifundishe wewe wenyewe? Unawaambia usiibe, lakini wewe mwenyewe unaiba. 22 Unasema wasizini, lakini wewe mwenyewe una hatia ya dhambi hiyo. Unachukia sanamu, lakini unaziiba sanamu katika mahekalu yao. 23 Unajivuna sana kwamba una sheria ya Mungu, lakini unamletea Mungu aibu kwa kuivunja sheria yake. 24 Kama Maandiko yanavyosema, “Watu wa mataifa mengine wanamtukana Mungu kwa sababu yako.”[c]

25 Ikiwa mnaifuata sheria, basi kutahiriwa kwenu kuna maana. Lakini mkiivunja sheria, mnakuwa kama watu ambao hawakutahiriwa. 26 Wale wasiokuwa Wayahudi hawatahiriwi. Lakini wakiifuata sheria inavyosema, wanakuwa kama watu waliotahiriwa. 27 Mnayo sheria na tohara, lakini mnaivunja sheria. Hivyo wale wasiotahiriwa katika miili yao, lakini bado wanaitii sheria, wataonesha kuwa mna hatia.

28 Wewe si Myahudi halisi ikiwa utakuwa Myahudi tu kwa nje. Tohara halisi si ile ya nje ya mwili tu. 29 Myahudi halisi ni yule aliye Myahudi kwa ndani. Tohara halisi inafanywa moyoni. Ni kitu kinachofanywa na Roho, na hakifanyiki ili kufuata sheria iliyoandikwa. Na yeyote aliyetahiriwa moyoni kwa Roho hupata sifa kutoka kwa Mungu, siyo kutoka kwa watu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International