Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

M’Cheyne Bible Reading Plan

The classic M'Cheyne plan--read the Old Testament, New Testament, and Psalms or Gospels every day.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Error: Book name not found: Gen for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Mathayo 2

Wenye Hekima Waja Kumwona Yesu

Yesu alizaliwa katika mji wa Bethlehemu ya Uyahudi wakati Herode alipokuwa mfalme. Baada ya Yesu kuzaliwa, baadhi ya wenye hekima kutoka mashariki walikuja Yerusalemu. Walipofika wakawauliza watu, “Yuko wapi mtoto aliyezaliwa ili awe Mfalme wa Wayahudi? Tuliiona nyota ilipochomoza na kutuonesha kuwa amezaliwa. Nasi tumekuja ili tumwabudu.”

Mfalme Herode aliposikia haya, yeye pamoja na watu wote wakaao Yerusalemu walikasirika sana. Herode aliitisha mkutano wa wakuu wote wa makuhani wa Kiyahudi na walimu wa sheria. Akawauliza ni wapi ambapo Masihi angezaliwa. Wakamjibu, “Ni katika mji wa Bethlehemu ya Yuda kama ambavyo nabii aliandika:

‘Bethlehemu, katika nchi ya Yuda,
    wewe ni wa muhimu miongoni mwa watawala wa Yuda.
Ndiyo, mtawala atakayewaongoza
    watu wangu Israeli, atatoka kwako.’”(A)

Kisha Herode akawaita na kufanya mkutano wa siri na wenye hekima kutoka mashariki. Akaelewa kwa usahihi wakati walipoiona nyota. Kisha akawaruhusu waende Bethlehemu. Akawaambia, “Nendeni mkamtafute mtoto kwa makini na mtakapompata mrudi na kunipa taarifa mahali alipo, ili nami pia niende kumwabudu.”

Wenye hekima walipomsikiliza mfalme, waliondoka. Waliiona tena ile nyota waliyoiona hapo mwanzo na wakaifuata. Nyota ile iliwaongoza mpaka mahali alipokuwa mtoto na kusimama juu ya sehemu hiyo. 10 Wenye hekima walipoona kuwa nyota ile imesimama, walifurahi na kushangilia kwa furaha.

11 Wenye hekima hao kisha waliingia katika nyumba alimokuwamo mtoto Yesu pamoja na Mariamu mama yake. Walisujudu na kumwabudu mtoto. Kisha wakafungua masanduku yenye zawadi walizomletea mtoto. Wakampa hazina za dhahabu, uvumba na manemane. 12 Lakini Mungu aliwaonya wenye hekima hao katika ndoto kuwa wasirudi tena kwa Herode. Hivyo kwa kutii walirudi nchini kwao kwa kupitia njia nyingine.

Yesu Apelekwa Uhamishoni Misri

13 Baada ya wenye hekima kuondoka, malaika wa Bwana akamjia Yusufu katika ndoto na kumwambia, “Damka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake ukimbilie Misri kwa sababu Herode amedhamiria kumwua mtoto na sasa atatuma watu kumtafuta. Na mkae Misri mpaka nitakapowaambia mrudi.”

14 Hivyo Yusufu alidamka na kutoka kwenda Misri akiwa na mtoto na mama yake. Nao waliondoka usiku. 15 Yusufu na familia yake walikaa huko Misri mpaka Herode alipofariki. Hili lilitukia ili maneno yaliyosemwa na nabii yatimie: “Nilimwita mwanangu atoke Misri.”(B)

Herode Aua Watoto wa Kiume Katika Mji wa Bethlehemu

16 Herode alipoona kuwa wenye hekima wamemfanya aonekane mjinga, alikasirika sana. Hivyo akatoa amri ya kuua watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili au chini ya miaka hiyo katika mji wa Bethlehemu na vitongoji vyake. Herode alifahamu kutoka kwa wenye hekima kwamba walikuwa wameiona nyota miaka miwili kabla. 17 Hili likatimiza yale yaliyosemwa na Mungu kupitia nabii Yeremia aliposema:

18 “Sauti imesikika Rama,
    sauti ya kilio na huzuni kuu.
Raheli akiwalilia watoto wake,
    na amekataa kufarijiwa
    kwa sababu watoto wake hawapo tena.”(C)

Yusufu na Familia Yake Warudi Kutoka Misri

19 Wakati Yusufu na familia yake wakiwa Misri, Herode alifariki. Malaika wa Bwana akamjia Yusufu katika ndoto 20 na akamwambia, “Damka! Mchukue mtoto na mama yake urudi Israeli, kwani waliojaribu kumwua mtoto wamekwisha kufa.”

21 Hivyo Yusufu alidamka na kumchukua mtoto Yesu na mama yake na kurudi Israeli. 22 Lakini Yusufu aliposikia kuwa Arkelao alikuwa mfalme wa Yuda baada ya baba yake kufa, aliogopa kwenda huko. Lakini baada ya kuonywa na Mungu katika ndoto, Yusufu aliondoka pamoja na familia yake akaenda sehemu za Galilaya. 23 Alikwenda katika mji wa Nazareti na kukaa huko. Hii ilitokea ili kutimiza maneno yale yaliyosemwa na manabii. Mungu alisema Masihi angeitwa Mnazareti.[a]

Error: Book name not found: Ezra for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Matendo 2

Kuja kwa Roho Mtakatifu

Siku ya Pentekoste ilipofika, wote walikuwa pamoja sehemu moja. Ghafla sauti ikaja kutoka mbinguni. Ilikuwa kama sauti ya upepo mkali unaovuma. Sauti hii ikajaa katika nyumba yote walimokuwa. Waliona miali iliyoonekana kama ndimi za moto. Miali ilitengana na kukaa juu ya kila mmoja wao pale. Wote walijaa Roho Mtakatifu na wakaanza kuzungumza kwa lugha tofauti. Roho Mtakatifu aliwapa uwezo wa kuzungumza lugha hizi.

Wakati haya yanatokea, walikuwepo Wayahudi waliorudi makwao. Hawa walikuwa wacha Mungu kutoka kila taifa ulimwenguni waliokuja mjini Yerusalemu. Kundi kubwa lilikusanyika kwa sababu walisikia kelele. Walishangaa kwa sababu, mitume walipokuwa wakitamka maneno kila mtu alisikia kwa lugha ya kwao.

Watu wote walilishangaa hili. Hawakuelewa ni kwa namna gani mitume waliweza kufanya hili. Wakaulizana, “Tazama! Watu wote hawa tunaowasikia wanatoka Galilaya.[a] Lakini tunawasikia wanatamka maneno kwa lugha zetu za asili. Hili linawezekanaje? Sisi tunatoka sehemu hizo mbalimbali: Parthia, Umedi, Elamu, Mesopotamia, Uyahudi, Kapadokia, Ponto, Asia, 10 Frigia, Pamfilia, Misri na maeneo ya Libya karibu na mji wa Kirene, Rumi, 11 Krete na Uarabuni. Baadhi yetu ni Wayahudi kwa kuzaliwa na wengine si Wayahudi, bali wamechagua kumwabudu Mungu kama Wayahudi. Tunatoka katika nchi hizi mbalimbali, lakini tunawasikia watu hawa wakizungumza kwa lugha zetu tofauti! Sisi sote tunaweza kuelewa yote wanayosema kuhusu matendo makuu ya Mungu.”

12 Watu wote walistaajabu na pia walichanganyikiwa. Wakaulizana, “Hii yote inamaanisha nini?” 13 Lakini wengine waliwacheka mitume, wakisema wamelewa kwa mvinyo mwingi waliokunywa.

Petro Azungumza na Watu

14 Ndipo Petro akasimama akiwa pamoja na mitume wengine kumi na moja. Akapaza sauti ili watu wote waweze kusikia. Alisema, “Ndugu zangu Wayahudi, nanyi nyote mnaoishi Yerusalemu. Nitawaeleza kuhusu jambo lililotokea, nisikilizeni kwa makini. 15 Watu hawa hawajalewa kwa mvinyo kama mnavyodhani; bado ni saa tatu asubuhi. 16 Lakini Nabii Yoeli aliandika kuhusu jambo hili mnaloliona likitokea hapa. Aliandika:

17 ‘Mungu anasema: Katika siku za mwisho,
    nitaimimina Roho yangu kwa watu wote.
Wana wenu na binti zenu watatabiri.
    Vijana wenu wataona maono,
    na wazee wenu wataota ndoto.
18 Katika siku hizo nitaimimina Roho
    yangu kwa watumishi wangu,
    wanaume na wanawake, nao watatabiri.
19 Nitafanya maajabu juu angani.
    Nitasababisha ishara chini duniani.
    Kutakuwa damu, moto na moshi mzito.
20 Jua litakuwa giza,
    na mwezi utakuwa mwekundu kama damu
    kabla ya ile siku kuu yenye utukufu ya Bwana kuja.
21 Na kila amwombaye Bwana’[b] ataokolewa.(A)

22 Ndugu zangu Waisraeli, sikilizeni ninayowaambia: Mungu aliwaonesha wazi kuwa Yesu kutoka Nazareti alikuwa mtu wake. Mungu alilithibitisha hili kwa miujiza, maajabu na ishara alizotenda Yesu. Ninyi nyote mliyaona mambo haya, na mnajua hii ni kweli. 23 Yesu aliletwa kwenu, nanyi mkamwua. Kwa kusaidiwa na watu wasioijali sheria yetu, mlimpigilia msalabani. Lakini Mungu alijua hili lingetokea. Ulikuwa mpango wake, mpango alioutengeneza tangu mwanzo. 24 Yesu aliteseka kwa maumivu makali ya kifo, lakini Mungu alimweka huru. Akamfufua kutoka kwa wafu. Mauti ilishindwa kumshikilia. 25 Daudi alilisema hili kuhusu Yesu:

‘Sijasahau kuwa Bwana yu pamoja nami.
    Yupo hapa pembeni yangu,
    hivyo hakuna kinachoweza kunidhuru.
26 Ndiyo sababu ninafurahi sana,
    na ninaimba kwa furaha!
    Lipo tumaini hata kwa ajili ya mwili wangu huu dhaifu,
27 kwa sababu wewe Bwana hutaniacha kaburini.[c]
    Hautauacha mwili wa mtumishi wako mwaminifu[d] kuozea huko.
28 Umenionyesha njia iendayo uzimani.
    Kuwa pamoja nawe kutanijaza furaha.’(B)

29 Ndugu zangu, ninaweza kuwaambia kwa ujasiri kuhusu Daudi, baba yetu mkuu. Alikufa, akazikwa, na kaburi lake liko hapa pamoja nasi hata leo. 30 Alikuwa nabii na alijua kitu ambacho Mungu alisema. Mungu alimwahidi Daudi kwa kuweka Agano kuwa mzaliwa katika familia yake mwenyewe ataketi kwenye kiti cha enzi cha Daudi kama mfalme.[e] 31 Daudi aliliona hili kabla halijatokea. Ndiyo maana alisema hivi kuhusu mfalme ajaye:

‘Hakuachwa kaburini.
    Mwili wake haukuozea humo.’[f]

Daudi alizungumza kuhusu Masihi kufufuka kutoka kwa wafu. 32 Yesu ndiye ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Sisi sote ni mashahidi wa jambo hili. Tulimwona. 33 Yesu alichukuliwa juu mbinguni. Na sasa ameketi upande wa kulia wa Mungu. Baba amempa Roho Mtakatifu, kama alivyoahidi. Hivyo Yesu amemimina huyo Roho Mtakatifu na hiki ndicho mnachoona na kusikia 34 Daudi hakuchukuliwa mpaka mbinguni. Daudi mwenyewe alisema,

‘Bwana Mungu alimwambia Bwana wangu:
Keti upande wangu wa kuume
35     hadi nitakapowaweka maadui zako chini ya udhibiti wako.’[g](C)

36 Hivyo, watu wote wa Israeli wanapaswa kulijua hili bila kuwa na mashaka: Mungu amemfanya Yesu kuwa Bwana na Masihi. Ndiye yule mliyempigilia msalabani!”

37 Watu waliposikia hili wakahuzunika sana. Wakawauliza Petro na mitume wengine, “Ndugu zetu, tufanye nini?”

38 Petro akawaambia, “Geuzeni mioyo na maisha yenu na kila mmoja wenu abatizwe katika jina la Yesu Kristo. Ndipo Mungu atawasamehe dhambi zenu, na mtapokea zawadi ya Roho Mtakatifu. 39 Ahadi hii ni kwa ajili yenu ninyi, watoto wenu na vizazi vijavyo. Ni kwa kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu anamwita kwake mwenyewe.”

40 Petro aliwaonya kwa maneno mengine mengi; aliwasihi, akawaambia, “Jiokoeni na uovu unaofanywa na watu wanaoishi sasa!” 41 Ndipo wale walioyakubali yale aliyosema Petro wakabatizwa. Yapata watu elfu tatu waliongezwa kwenye kundi la waamini siku ile.

Ushirika wa Waamini

42 Waamini walitumia muda wao kusikiliza mafundisho ya mitume. Walishirikiana kila kitu kwa pamoja. Walikula[h] na kuomba pamoja. 43 Maajabu mengi na ishara nyingi zilikuwa zinatokea kupitia mitume, na hivyo kila mtu aliingiwa na hofu na akamtukuza Mungu. 44 Waamini wote walikaa pamoja, na kushirikiana kila kitu. 45 Waliuza mashamba yao na vitu walivyomiliki, kisha wakatoa fedha na kuwapa wenye kuhitaji. 46 Waamini waliendelea kukutana pamoja katika eneo la Hekalu. Pia walikula pamoja katika nyumba zao. Walikuwa na furaha kushirikiana chakula chao na walikula kwa mioyo mikunjufu. 47 Waamini walimsifu Mungu na waliheshimiwa na watu wote. Watu wengi zaidi waliokolewa kila siku, na Bwana alikuwa akiwaongeza kwenye kundi lao.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International