M’Cheyne Bible Reading Plan
Iweni Waangalifu Mnapokosoa Wengine
(Lk 6:37-38,41-42)
7 Msiwahukumu wengine, ili Mungu asiwahukumu ninyi pia. 2 Mtahukumiwa jinsi ile ile mnavyowahukumu wengine. Mungu atawatendea kama mnavyowatendea wengine.
3 Kwa nini unaona vumbi iliyo katika jicho la rafiki yako, na hujali kipande cha mti kilicho katika jicho lako? 4 Kwa nini unamwambia rafiki yako, ‘Ngoja nitoe vumbi lililo katika jicho lako wakati wewe mwenyewe bado una kipande cha mti katika jicho lako?’ 5 Ewe mnafiki! Ondoa kwanza kipande cha mti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utaweza kuona vizuri na kutoa vumbi katika jicho la rafiki yako.
6 Msiwape mbwa kitu kitakatifu, watawageuka na kuwadhuru. Na msiwatupie nguruwe lulu zenu kwa kuwa watazikanyaga tu.
Mwombeni Mungu Kile Mnachohitaji
(Lk 11:9-13)
7 Endeleeni kumwomba Mungu, naye atawapa, endeleeni kutafuta nanyi mtapata, endeleeni kubisha nanyi mtafunguliwa mlango. 8 Ndiyo, yeyote anayeendelea kuomba atapokea. Yeyote anayeendelea kutafuta atapata. Na yeyote anayeendelea kubisha atafunguliwa mlango.
9 Ni nani kati yenu aliye na mwana ambaye akimwomba mkate atampa jiwe? 10 Au akimwomba samaki, atampa nyoka? Bila shaka hakuna! 11 Ijapokuwa ninyi watu ni waovu, lakini bado mnajua kuwapa vitu vyema watoto wenu. Hakika Baba yenu wa mbinguni atawapa vitu vyema wale wamwombao.
Kanuni ya Muhimu Sana
12 Watendee wengine kama ambavyo wewe ungetaka wao wakutendee. Hii ndiyo tafsiri ya torati[a] na mafundisho ya manabii.
Wachache tu Ndiyo Huiona Njia ya Uzima
(Lk 13:24)
13 Unapaswa kuingia katika uzima wa kweli kupitia lango lililo jembamba. Kwa kuwa lango ni pana na njia inayoelekea katika uharibifu nayo ni pana na watu wengi wanaifuata njia hiyo. 14 Lakini lango la kuelekea katika uzima wa kweli ni jembamba. Na njia iendayo huko ni ngumu kuifuata. Na ni watu wachache wanaoiona.
Kile Wanachokifanya watu Kinadhihirisha jinsi gani Walivyo
(Lk 6:43-44; 13:25-27)
15 Mjihadhari na manabii wa uongo wanaokuja kwenu wakijifanya kondoo wasio na madhara ingawa ni watu hatari kama mbwa mwitu. 16 Mtawatambua watu hawa kwa matendo yao. Mambo mazuri hayatoki kwa watu wabaya, kama ambavyo zabibu haitokani na miiba, na tini hazitokani na mbigiri. 17 Vile vile, kila mti mzuri huzaa matunda mazuri na mti mbaya huzaa matunda mabaya. 18 Mti mzuri hauwezi kuzaa matunda mabaya, na wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri. 19 Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa kwenye moto. 20 Mtawatambua manabii hawa wa uongo kwa matendo yao.
21 Si kila aniitaye Bwana ataingia katika ufalme wa Mungu. Watakaoingia ni wale tu wafanyao yale ambayo Baba yangu wa mbinguni anataka. 22 Siku ya mwisho wengi wataniiita Bwana. Watasema, ‘Bwana, kwa nguvu za jina lako tulihubiri. Na kwa nguvu za jina lako tulitoa mashetani na kufanya miujiza mingi.’ 23 Ndipo nitawaambia waziwazi, ‘Ondokeni kwangu, ninyi waovu. Sikuwahi kuwajua.’
Aina Mbili za Watu
(Lk 6:47-49)
24 Kila anayeyasikia mafundisho yangu na kuyatii ni kama mwenye hekima aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba. 25 Mvua kubwa iliponyesha na mafuriko yakaja, na upepo ukavuma sana, na kuipiga sana nyumba yake. Lakini, nyumba yake haikuanguka kwa sababu ilijengwa kwenye mwamba.
26 Lakini kila anayeyasikia mafundisho yangu na asiyatii ni kama mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga. 27 Mvua kubwa iliponyesha na mafuriko kuja, na upepo ukavuma sana, nyumba yake ilianguka kwa kishindo kikuu.”
28 Yesu alipomaliza kufundisha, watu walishangaa sana namna alivyokuwa akifundisha. 29 Hakufundisha kama walimu wao wa sheria; alifundisha kwa mamlaka.[b]
Hotuba ya Stefano
7 Kuhani mkuu akamwambia Stefano, “Mambo haya ndivyo yalivyo?” 2 Stefano akajibu, “Ndugu zangu na baba zangu Wayahudi, nisikilizeni! Mungu wetu mkuu na mwenye utukufu alimtokea Ibrahimu, baba yetu, alipokuwa Mesopotamia. Kabla hajahamia Harani. 3 Mungu alimwambia, ‘Ondoka katika nchi yako na watu wako, kisha uende katika nchi nitakayokuonesha.’(A)
4 Hivyo Ibrahimu akaondoka katika nchi ya Ukaldayo[a] na kwenda kuishi Harani. Baada ya baba yake kufa, Mungu akamleta katika nchi hii, mahali mnapoishi sasa. 5 Lakini Mungu hakumpa Ibrahimu sehemu yoyote ya ardhi hii, hata eneo dogo lenye ukubwa wa unyayo wake. Lakini Mungu aliahidi kuwa atampa Ibrahimu nchi hii yeye na watoto wake hapo baadaye. Hii ilikuwa kabla Ibrahimu hajapata watoto.
6 Mungu alimwambia: ‘Wazao wako wataishi katika nchi nyingine. Watakuwa wageni. Watu wa huku watawafanya kuwa watumwa na kuwatendea vibaya kwa miaka mia nne. 7 Lakini nitaliadhibu taifa lililowafanya watumwa.’(B) Pia, Mungu alisema, ‘Baada ya mambo hayo kutokea, watu wako watatoka katika nchi hiyo. Kisha wataniabudu mahali hapa.’(C)
8 Mungu aliweka agano na Ibrahimu; alama ya agano hili ilikuwa tohara. Na Ibrahimu alipopata mwana, alimtahiri siku ya nane baada ya kuzaliwa. Jina la mwanaye lilikuwa Isaka. Pia, Isaka alimtahiri mwanaye Yakobo. Na Yakobo alifanya vivyo hivyo kwa wanaye, ambao ndiyo baba wakuu kumi na mbili wa watu wetu.
9 Baba zetu hawa walimwonea wivu Yusufu ndugu yao na wakamwuza ili awe mtumwa Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye, 10 akamwokoa kutoka katika matatizo yake yote. Wakati huo Farao alikuwa mfalme wa Misri. Alimpenda na akamheshimu Yusufu kwa sababu ya hekima ambayo Mungu alimpa. Farao alimfanya Yusufu kuwa gavana wa Misri na msimamizi wa watu wote na kila kitu katika kasri lake. 11 Lakini nchi yote ya Misri na Kanaani zikakosa mvua na mazao ya chakula hayakuweza kuota. Watu waliteseka sana na watu wetu hawakuweza kupata chakula chochote.
12 Lakini Yakobo aliposikia kulikuwa chakula Misri aliwatuma mababa zetu huko. Hii ilikuwa safari yao ya kwanza kwenda Misri. 13 Kisha walikwenda safari ya pili. Safari hii Yusufu akawaeleza ndugu zake yeye ni nani. Ndipo Farao akatambua kuhusu familia ya Yusufu. 14 Kisha Yusufu aliwatuma kaka zake wamwambie Yakobo, baba yake, ahamie Misri. Aliwaalika pia ndugu zake wote, jumla yao wote walikuwa watu sabini na tano. 15 Hivyo Yakobo alitelemka kwenda Misri. Yeye na baba zetu waliishi huko mpaka walipokufa. 16 Baadaye, miili yao ilihamishiwa Shekemu, ambako iliwekwa katika kaburi ambalo Ibrahimu alilinunua kwa fedha kutoka kwa wana wa Hamori.
17 Watu wetu walipokuwa Misri idadi yao iliongezeka. Watu wetu walikuwa wengi mno huko. Ahadi ambayo Mungu aliiweka kwa Ibrahimu ilikuwa karibu kutimia. 18 Ndipo mfalme mwingine akaanza kutawala Misri, ambaye hakujua lolote kuhusu Yusufu. 19 Mfalme huyu aliwahadaa watu wetu. Akawatendea vibaya sana, akawalazimisha wawaache watoto wao nje ili wafe.
20 Huu ni wakati ambapo Musa alizaliwa. Alikuwa mtoto mzuri sana, na kwa miezi mitatu wazazi wake walimtunza nyumbani. 21 Walipolazimishwa kumtoa nje, Binti wa Farao alimchukua. Alimkuza kama mwanaye wa kumzaa. 22 Musa alielimishwa kwa elimu bora ya Kimisri. Wamisri walimfundisha kila kitu walichojua. Alikuwa mwenye nguvu katika yote aliyosema na kutenda.
23 Musa alipokuwa na umri wa miaka kama arobaini, aliamua kuwatembelea watu wake mwenyewe, watu wa Israeli. 24 Aliona mmoja wao ananyanyaswa na Mmisri, hivyo akamtetea; Musa akampiga na kumwua Mmisri ili kulipiza kwa kumwumiza Mwisraeli. 25 Musa alidhani kwamba watu wake wangeelewa kuwa Mungu alikuwa anamtumia kuwaokoa. Lakini hawakuelewa.
26 Siku iliyofuata, Musa akawaona wawili wa watu wake wakipigana. Alijaribu kuwapatanisha kwa kuwaambia, ‘Ninyi ni ndugu! Kwa nini mnataka kuumizana?’ 27 Aliyekuwa akimwumiza mwenzake akamsukuma Musa na akamwambia, ‘Nani amekufanya wewe uwe mtawala na mwamuzi wetu? 28 Unataka kuniua kama ulivyomwua yule Mmisri jana?’(D) 29 Musa alipomsikia akisema hili, alikimbia Misri. Alikwenda kuishi Midiani kama mgeni. Katika kipindi alichoishi huko, alipata wana wawili.
30 Miaka arobaini baadaye, Musa alipokuwa jangwani karibu na Mlima Sinai, malaika alimtokea katika mwali wa moto uliokuwa unawaka katika kichaka. 31 Musa alipoliona hili, alishangaa. Alisogea ili kuangalia kwa karibu. Akasikia sauti; ilikuwa sauti ya Bwana. 32 Bwana alisema, ‘Mimi ni Mungu yule yule aliyeabudiwa na baba zako. Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.’(E) Musa akaanza kutetemeka kwa woga. Aliogopa kukitazama kichaka.
33 Kisha Bwana akamwambia, ‘Vua viatu vyako, kwa sababu mahali uliposimama ni ardhi takatifu. 34 Nimewaona watu wangu wanavyoteseka sana Misri. Nimesikia watu wangu wakilia na nimeshuka ili kuwaokoa. Njoo sasa, Musa, ninakutuma urudi Misri.’(F)
35 Huyu ni Musa ndiye aliyekataliwa na watu wake. Walisema, ‘Nani amekufanya uwe mtawala na mwamuzi wetu?’(G) Lakini ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mtawala na mwokozi. Mungu alimtuma pamoja na msaada wa malaika,[b] ambaye Musa alimwona katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto. 36 Hivyo Musa aliwaongoza watu kutoka Misri. Alitenda maajabu na ishara za miujiza Misri, katika bahari ya Shamu na jangwani kwa miaka arobaini.
37 Huyu ni Musa yule yule aliyewaambia maneno haya watu wa Israeli: ‘Mungu atakupa nabii. Nabii huyo atakuja kutoka miongoni mwa watu wako mwenyewe. Atakuwa kama mimi.’(H) 38 Musa huyo huyo alikuwa pamoja na kusanyiko la watu wa Mungu jangwani. Alikuwa na malaika aliyezungumza naye alipokuwa Mlima Sinai, na alikuwa pamoja na baba zetu. Alipokea maneno yaletayo uzima kutoka kwa Mungu, na Musa akatupa sisi Maneno hayo.
39 Lakini baba zetu hawakutaka kumtii Musa. Walimkataa, wakataka kurudi Misri. 40 Walimwambia Haruni, ‘Musa alituongoza kutoka katika nchi ya Misri. Lakini hatujui kilichompata. Hivyo tengeneza miungu ili iwe mbele yetu ituongoze.’(I) 41 Hivyo watu wakatengeneza kinyago kinachofanana na ndama. Kisha wakakitolea sadaka za kuteketezwa. Walifurahia kile walichotengeneza kwa mikono yao wenyewe. 42 Lakini Mungu akawaacha, nao wakaendelea kuabudu nyota na sayari.[c] Kitabu cha manabii[d] kinasema hivi:
‘Watu wa Israeli, hamkunipa dhabihu
jangwani kwa miaka arobaini.
43 Mlibeba hema kwa ajili ya kumwabudia Moleki,
na sanamu ya nyota ya mungu wenu Refani.
Hizi zilikuwa sanamu mlizotengeneza ili mziabudu.
Hivyo nitawahamishia mbali, kuvuka Babeli.’(J)
44 Baba zetu walikuwa na Hema Takatifu walipokuwa jangwani. Mungu alimwelekeza Musa jinsi ya kutengeneza hema hii. Aliitengeneza kwa kufuata ramani aliyoonyeshwa na Mungu. 45 Baadaye, Yoshua aliwaongoza baba zetu kuteka ardhi ya mataifa mengine. Watu wetu waliingia, na Mungu akawafukuza watu wengine. Watu wetu walipoingia katika ardhi hii mpya, waliibeba hema hii pamoja nao. Watu wetu waliipata hema hii kutoka kwa baba zao, na watu wetu waliitunza mpaka wakati wa Daudi. 46 Mungu alimpenda Daudi.[e] Na Daudi akamwomba Mungu amruhusu ajenge Hekalu kwa ajili ya watu wa Israeli[f] 47 Lakini Sulemani ndiye aliyemjengea Mungu Hekalu.
48 Lakini Mungu Aliye Juu sana hahitaji yumba zilizojengwa kwa mikono ya wanadamu ili aishi ndani yake. Nabii aliandika hivi:
49 ‘Bwana asema, Mbingu ni kiti changu cha enzi,
na dunia ni sehemu ya kuweka miguu yangu.
Hivyo mnadhani mnaweza kunijengea nyumba?
Je, ninahitaji mahali pa kupumzika?
50 Kumbukeni, niliumba vitu vyote hivi?’”(K)
51 Kisha Stefano akasema, “Enyi viongozi wa Kiyahudi mlio wakaidi! Mnakataa kumpa Mungu mioyo yenu na mnakataa hata kumsikiliza. Daima mko kinyume na Roho Mtakatifu. Baba zenu walikuwa vivyo hivyo, nanyi mko kama wao! 52 Walimtesa kila nabii aliyewahi kuishi. Waliwaua hata wale ambao zamani zilizopita walisema kwamba Mwenye Haki ilikuwa aje. Na sasa mmekuwa kinyume na Mwenye Haki na mmemwua. 53 Ninyi ndiyo mliipokea Sheria ya Mungu,[g] aliyoitoa kupitia malaika zake. Lakini hamtaki kuitii!”
Stefano Auawa
54 Waliokuwa kwenye mkutano wa baraza waliposikia maneno haya, walikasirika sana na wakamsagia meno Stefano kwa hasira. 55 Lakini Stefano, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alitazama juu mbinguni, na kuuona utukufu wa Mungu. Alimwona Yesu amesimama upande wa kulia wa Mungu. 56 Stefano akasema, “Tazama! Naona mbingu zimefunguka. Na ninamwona Mwana wa Adamu amesimama upande wa kulia wa Mungu.”
57 Kila mmoja pale akaanza kupiga kelele, wakaziba masikio yao kwa mikono yao. Wote kwa pamoja wakamvamia Stefano. 58 Wakamtoa nje ya mji na kuanza kumpiga kwa mawe. Mashahidi walioshuhudia uongo kinyume cha Stefano waliacha makoti yao kwa kijana aliyeitwa Sauli. 59 Walipokuwa wanampiga kwa mawe, Stefano aliomba, akisema, “Bwana Yesu, pokea roho yangu.” 60 Alianguka kwa magoti yake na kupaza sauti, akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii!” Haya yalikuwa maneno yake ya mwisho kabla ya kufa.
© 2017 Bible League International