M’Cheyne Bible Reading Plan
Yohana Atuma Watu Kumwuliza Yesu Swali
(Lk 7:18-35)
11 Yesu alipomaliza maelekezo haya kwa wafuasi wake kumi na wawili wa karibu, aliondoka mahali pale. Akaenda katika miji ya Galilaya kuwafundisha watu na kuwaeleza ujumbe wa Mungu.
2 Yohana alipokuwa gerezani, alisikia kuhusu mambo yaliyokuwa yanatokea; mambo ambayo Masihi angefanya. Hivyo akawatuma baadhi ya wafuasi wake kwa Yesu. 3 Wakamuuliza, “Wewe ni yule tuliyekuwa tunamngojea, au tumsubiri mwingine?”
4 Yesu akajibu, “Rudini mkamwambie Yohana yale mliyosikia na kuona: 5 Vipofu wanaona. Viwete wanatembea. Watu wenye magonjwa ya ngozi wanaponywa. Wasiyesikia wanasikia. Wafu wanafufuliwa. Na habari njema inahubiriwa kwa maskini. 6 Heri ni kwa wale wasio na shida kunikubali.”
7 Wafuasi wa Yohana walipoondoka, Yesu alianza kuongea na watu kuhusu Yohana. Alisema, “Ninyi watu mlikwenda jangwani kuona nini? Mtu aliye dhaifu, kama unyasi unaoyumbishwa na upepo? 8 Hakika, ni nini mlichotarajia kuona? Aliyevaa mavazi mazuri? Hakika si hivyo. Watu wote wanaovaa mavazi mazuri wanapatikana katika ikulu za wafalme. 9 Hivyo mlitoka kuona nini? Nabii? Ndiyo, Yohana ni nabii. Lakini ninawaambia, Yeye ni zaidi ya hilo. 10 Andiko hili liliandikwa kuhusu Yohana:
‘Sikiliza! Nitamtuma mjumbe mbele yako.
Yeye ataandaa njia kwa ajili yako.’(A)
11 Ukweli ni kuwa Yohana Mbatizaji ni mkuu kuliko yeyote aliyewahi kuja katika ulimwengu huu. Lakini hata mtu asiye wa muhimu katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko Yohana. 12 Tangu wakati wa Yohana Mbatizaji ulipokuja mpaka sasa, Ufalme wa Mungu umekabiliwa na mashambulizi. Watu wenye nguvu wamejaribu kuudhibiti ufalme huu.[a] 13 Kabla ya Yohana kuja, Sheria ya Musa na manabii wote wamesema kuhusu mambo ambayo yangetokea. 14 Na ikiwa mnaamini waliyosema, basi Yohana ni Eliya. Ndiye waliyesema angekuja. 15 Ninyi watu mnaonisikia, sikilizeni!
16 Ninaweza kusema nini kuhusu watu wanaoishi leo? Watu siku ya leo ni kama watoto wanaokaa katika masoko. Kundi moja la watoto linaliambia kundi lingine,
17 ‘Tuliwapigia filimbi,
lakini hamkucheza;
tuliimba wimbo wa maziko,
lakini hamkuhuzunika.’
18 Kwa nini ninasema watu wako hivyo? Kwa sababu Yohana alikuja na hakula vyakula vya kawaida na kunywa divai, na watu walisema, ‘Ana pepo ndani yake.’ 19 Mwana wa Adamu amekuja akila na kunywa, na watu husema, ‘Mwangalie! Hula sana na kunywa divai nyingi. Ni rafiki wa wakusanya kodi na wenye dhambi wengine.’ Lakini hekima inaonesha kuwa sahihi kutokana na yale inayotenda.”
Maonyo Kwa Wanaomkataa Yesu
(Lk 10:13-15)
20 Kisha Yesu akaanza kuikosoa miji ambako alifanya miujiza yake mingi. Aliikosoa miji hii kwa sababu watu katika miji hii hawakubadili maisha yao na kuacha kutenda dhambi. 21 Yesu alisema, “Itakuwa vibaya kwako Korazini! Itakuwa vibaya kwako Bethsaida![b] Ikiwa miujiza hii hii ingetokea Tiro na Sidoni,[c] watu huko wangeshabadili maisha yao kitambo. Wangekwishavaa magunia na kujimwagia majivu kuonesha kuwa wanasikitikia dhambi zao. 22 Lakini ninawaambia, siku ya hukumu itakuwa vibaya zaidi kwako kuliko Tiro na Sidoni.
23 Nawe Kapernaumu, utakwezwa mpaka mbinguni? Hapana! Utatupwa chini mpaka Kuzimu. Nimetenda miujiza mingi ndani yako. Iwapo miujiza hii ingetokea Sodoma,[d] watu huko wangeacha kutenda dhambi na ungekuwa bado ni mji hata leo. 24 Lakini ninakuambia, itakuwa vibaya kwako siku ya hukumu kuliko Sodoma.”
Yesu Awapa Pumziko Watu Wake
(Lk 10:21-22)
25 Kisha Yesu akasema, “Ninakusifu wewe, Baba, Bwana wa mbinguni na duniani. Ninashukuru kwa sababu umeyaficha mambo haya kwa wale wanaofikiri kuwa ni wenye hekima na werevu sana. Lakini umeyaonesha haya kwa watu walio kama watoto wadogo.[e] 26 Ndiyo, Baba, ulifanya hivi kwa sababu hakika ndivyo ulivyotaka kufanya.
27 Baba yangu amenipa kila kitu. Hakuna amjuaye Mwana isipokuwa Baba peke yake. Na hakuna amjuaye Baba isipokuwa Mwana ndiye anayemjua Baba. Na watu pekee watakaomjua Baba ni wale ambao Mwana atachagua kuwaonesha.
28 Njooni kwangu ninyi nyote mliochoka kutokana na mizigo mizito mnayolazimishwa kubeba. Nitawapa pumziko. 29 Chukueni nira yangu,[f] jifunzeni kutoka kwangu. Mimi ni mwema na mnyenyekevu katika roho. Nanyi mtaweza kupumzika. 30 Ndiyo, nira yangu ni rahisi. Mzigo ninaowapa muubebe ni mwepesi.”
Petro Arudi Yerusalemu
11 Mitume na waamini katika Uyahudi walisikia kwamba watu wasio Wayahudi wameyapokea mafundisho ya Mungu pia. 2 Lakini Petro alipokuja Yerusalemu, baadhi ya waamini wa Kiyahudi[a] walimkosoa. 3 Walisema, “Uliingia katika nyumba za watu wasio Wayahudi ambao hawajatahiriwa na ukala pamoja nao!”
4 Hivyo Petro akawaelezea namna ilivyotokea. 5 Akasema, “Nilikuwa katika mji wa Yafa. Nilipokuwa nikiomba, niliona maono. Niliona kitu kikishuka chini kutoka mbinguni. Kilionekana kama shuka kubwa ikishushwa chini kwa pembe zake nne. Kikaja chini karibu yangu. 6 Nilipotazama ndani yake, niliona aina zote za wanyama, pamoja na wale wa porini, wanyama wanaotambaa na ndege. 7 Nilisikia sauti ikiniambia. Chinja chochote hapa na ule!”
8 “Lakini nilisema, ‘Siwezi kufanya hivyo Bwana! Sijawahi kula kitu cho chote kisicho safi au kisichostahili kuliwa kama chakula.’
9 Lakini sauti kutoka mbinguni ikajibu tena, ‘Mungu amevitakasa vitu hivi. Usiseme havistahili kuliwa!’
10 Hili lilitokea mara tatu. Ndipo kitu chote kikachukuliwa kurudi mbinguni. 11 Saa hiyo hiyo baada ya hayo wakawepo watu watatu wamesimama nje ya nyumba nilimokuwa ninakaa. Walikuwa wametumwa kutoka Kaisaria kunichukua. 12 Roho Mtakatifu aliniambia niende nao bila kuwa na mashaka. Ndugu hawa hapa sita walikwenda pamoja nami, na tulikwenda katika nyumba ya Kornelio. 13 Alitwambia kuhusu malaika aliyemwona amesimama katika nyumba yake. Malaika alimwambia, ‘Tuma baadhi ya watu waenda Yafa kumchukua Simoni, ambaye pia anaitwa Petro. 14 Atazungumza na wewe. Ujumbe atakaokwambia utakuokoa wewe na kila mtu anayeishi katika nyumba yako.’
15 Nilipoanza kuzungumza, Roho Mtakatifu alikuja juu yao kama vile alivyokuja juu yetu mwanzo.[b] 16 Ndipo nilikumbuka maneno ya Bwana Yesu, aliyosema: ‘Yohana alibatiza katika maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu.’ 17 Mungu amewapa watu hawa karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo. Hivyo ningewezaje kupinga yale ambayo Mungu alitaka kufanya?”
18 Waamini wa Kiyahudi waliposikia hili, wakaacha kubisha. Wakamsifu Mungu na kusema, “Kwa hiyo Mungu anawaruhusu watu wasio Wayahudi kubadili mioyo yao na kuwa na maisha anayotoa!”
Habari Njema Zafika Antiokia
19 Waamini walitawanyika kwa sababu ya mateso[c] yaliyoanza baada ya Stefano kuuawa. Baadhi ya waamini walikwenda mbali mpaka Foeniki, Kipro na Antiokia. Walihubiri Habari Njema katika maeneo haya, lakini kwa Wayahudi tu. 20 Baadhi ya waamini hawa walikuwa watu kutoka Kipro na Kirene. Watu hawa walipofika Antiokia, walianza kuwahubiri watu wasio Wayahudi.[d] Waliwahubiri Habari Njema kuhusu Bwana Yesu. 21 Nguvu ya Bwana iliambatana na watu hawa, na idadi kubwa ya watu waliamini na kuamua kumfuata Bwana.
22 Kanisa katika mji wa Yerusalemu liliposikia kuhusu hili, lilimtuma Barnaba kwenda Antiokia. 23-24 Barnaba alikuwa mtu mwema, aliyejaa Roho Mtakatifu na imani. Alipokwenda Antiokia na kuona jinsi Mungu alivyowabariki waamini pale, alifurahi sana. Akawatia moyo wote, akasema, “Iweni waaminifu kwa Bwana daima. Mtumikieni Yeye kwa mioyo yenu yote.” Watu wengi zaidi wakawa wafuasi wa Bwana.
25 Kisha Barnaba alikwenda katika mji wa Tarso kumtafuta Sauli. 26 Alipompata, alimpeleka Antiokia. Walikaa pale mwaka mzima. Kila wakati kanisa lilipokusanyika, Barnaba na Sauli walikutana nao na kuwafundisha watu wengi. Ni katika mji wa Antiokia ambako wafuasi wa Bwana Yesu walianza kuitwa “Wafuasi wa Kristo”.[e]
27 Katika wakati huo huo baadhi ya manabii walitoka Yerusalemu na kwenda Antiokia. 28 Mmoja wao, aliyeitwa Agabo, huku akisaidiwa na Roho Mtakatifu, alisimama na kuzungumza. Alisema, “Wakati mbaya sana unakuja katika dunia yote. Hakutakuwa chakula kwa ajili ya watu kula.” (Kipindi hiki cha njaa kilitokea Klaudio alipokuwa mtawala wa Kirumi) 29 Wafuasi wa Bwana wakaamua kwamba kila mmoja wao atatuma kiasi anachoweza kuwasaidia ndugu wote[f] wanaoishi Uyahudi. 30 Walikusanya pesa na kuwapa Barnaba na Sauli, waliozipeleka kwa wazee, katika Uyahudi.
© 2017 Bible League International