New Testament in a Year
21 Ndugu watakuwa kinyume cha ndugu zao wenyewe na kuwapeleka kwenda kuuawa. Baba watawapeleka watoto wao wenyewe kuuawa. Watoto watapigana kinyume na wazazi wao na watawapeleka kuuawa. 22 Kila mtu atawachukia kwa sababu mnanifuata mimi. Lakini atakayekuwa mwaminifu mpaka mwisho ataokolewa. 23 Mnapotendewa vibaya katika mji mmoja, nendeni katika mji mwingine. Ninawaahidi kuwa hamtamaliza kwenda katika miji ya Israeli kabla Mwana wa Adamu hajarudi.
24 Wanafunzi si wazuri kuliko mwalimu wao. Watumwa si wazuri kuliko bwana wao. 25 Inatosha kwa wanafunzi kuwa kama walimu wao na watumwa kuwa kama bwana wao. Iwapo watu hao wananiita ‘mtawala wa pepo’, na mimi ni kiongozi wa familia, basi ni dhahiri kwa kiasi gani watawatukana ninyi, mlio familia yangu!
Mwogopeni Mungu, Siyo Watu
(Lk 12:2-7)
26 Hivyo msiwagope watu hao. Kila kitu kilichofichwa kitaoneshwa. Kila kilicho siri kitajulikana. 27 Ninayowaambia ninyi faraghani myaseme hadharani. Kila ninachowanong'oneza nawataka mkiseme kwa sauti kila mtu asikie.
28 Msiwaogope watu. Wanaweza kuua mwili, lakini hawawezi kuiua roho. Mnapaswa kumwogopa Mungu, anayeweza kuuharibu mwili na roho jehanamu. 29 Ndege wanapouzwa, ndege wawili wadogo hugharimu senti moja tu. Lakini hakuna hata mmoja wa ndege hao wadogo anaweza kufa bila Baba yenu kufahamu. 30 Mungu anafahamu idadi ya nywele katika vichwa vyenu. 31 Hivyo msiogope. Mna thamani kuliko kundi kubwa la ndege.
Msiionee Haya Imani Yenu
(Lk 12:8-9)
32 Iwapo mtawaambia watu wengine kuwa mnaniamini, nitamwambia Baba yangu aliye mbinguni kuwa ninyi ni wangu. 33 Lakini ikiwa mtasimama mbele ya wengine na kusema kuwa hamniamini, nitamwambia Baba yangu aliye mbinguni kuwa ninyi si wangu.
Kumfuata Yesu Kunaleta Matatizo
(Lk 12:51-53; 14:26-27)
34 Msidhani kuwa nilikuja duniani kuleta amani. Sikuja kuleta amani. Nilikuja kuleta vita. 35 Nimekuja ili hili litokee:
‘Mwana atamgeuka baba yake.
Binti atamgeuka mama yake.
Binti mkwe atamgeuka mama mkwe wake.
36 Hata watu wa familia zenu watakuwa adui zenu.’(A)
37 Wale wanaowapenda baba zao au mama zao kuliko wanavyonipenda mimi hawana thamani kwangu. Na wale wanaowapenda wana wao au binti zao kuliko wanavyonipenda mimi hawastahili kuwa wafuasi wangu. 38 Wale ambao hawataupokea msalaba waliopewa wanaponifuata hawastahili kuwa wanafunzi wangu na kunifuata. 39 Wale wanaojaribu kuyatunza maisha waliyonayo, watayapoteza. Lakini wale wanaoyaacha maisha yao kwa ajili yangu watapata uzima halisi.
Mungu Atawabariki Wanaowakaribisha Ninyi
(Mk 9:41)
40 Yeyote anayewakubali ninyi ananikubali mimi. Na yeyote anayenikubali anamkubali yule aliyenituma. 41 Yeyote anayemkubali nabii kwa sababu ni nabii atapata ujira wa nabii. Na yeyote anayemkubali mwenye haki kwa sababu ni mwenye haki atapata ujira anaoupata mwenye haki. 42 Yeyote anayemsaidia mmoja wa wafuasi wangu hawa wanyenyekevu kwa sababu ni wafuasi wangu hakika atapata ujira, hata ikiwa wanawapa tu kikombe cha maji baridi.”
© 2017 Bible League International