Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

New Testament in a Year

Read the New Testament from start to finish, from Matthew to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Mathayo 13:1-30

Simulizi Kuhusu Mkulima Aliyepanda Mbegu

(Mk 4:1-9; Lk 8:4-8)

13 Siku hiyo hiyo Yesu alitoka nje ya nyumba na kukaa kando ya ziwa. Kundi kubwa wakakusanyika kumzunguka. Hivyo akapanda mtumbwini na kuketi. Watu wote wakabaki ufukweni. Kisha Yesu akatumia simulizi kuwafundisha mambo mengi. Akawaambia simulizi hii:

“Mkulima alitoka kwenda kupanda mbegu. Alipokuwa anatawanya mbegu, baadhi ziliangukia njiani. Ndege wakaja na kuzila zote. Mbegu zingine ziliangukia kwenye ardhi yenye mawe, ambako hakukuwa na udongo wa kutosha. Zikakua haraka pale, kwa sababu udongo haukuwa na kina. Lakini jua lilipowaka, likaichoma mimea. Mimea ikafa kwa sababu haikuwa na mizizi mirefu. Baadhi ya mbegu ziliangukia katikati ya miiba. Miiba ikakua na kusababisha mimea mizuri kuacha kukua. Lakini baadhi ya mbegu ziliangukia kwenye udongo wenye rutuba. Hapo zikakua na kuzaa nafaka. Baadhi ya mimea ikazaa nafaka mara mia zaidi, baadhi mara sitini na baadhi mara thelathini zaidi. Ninyi watu mnaoweza kunisikia, nisikilizeni!”

Kwa nini Yesu Alitumia Simulizi Kufundisha

(Mk 4:10-12; Lk 8:9-10)

10 Wafuasi wake wakamwendea Yesu na kumuuliza, “Kwa nini unatumia simulizi hizi kuwafundisha watu?”

11 Yesu akawajibu, “Mungu amewapa ninyi ujuzi wa kuelewa siri za ufalme wa Mungu, lakini hajawapa watu hawa wengine ujuzi huu. 12 Kisha akawaambia, ‘Zingatieni kwa makini kile mnachokisikia. Kwani jinsi mnavyosikiliza kwa makini, ndivyo mtakavyoelewa na kuzidi kuelewa. Kwa kuwa kila aliye na uelewa kidogo ataongezewa zaidi. Lakini wale wasiosikiliza kwa makini watapoteza hata ule uelewa mdogo walio nao.’ 13 Ndiyo sababu ninatumia simulizi hizi kuwafundisha watu: Wanaona, lakini hakika hawaoni. Wanasikia, lakini hakika hawasikii au kuelewa. 14 Hiyo inathibitisha alichosema nabii Isaya kuhusu wao kuwa kweli:

‘Ninyi watu mtasikia na kusikia,
    lakini hamtaelewa.
Mtatazama na kutazama,
    lakini hakika hamtaona.
15 Ndiyo, akili za watu hawa sasa zimefungwa.
    Wana masikio, lakini hawasikii vizuri.
Wana macho, lakini wameyafumba.
    Iwapo akili zao zisingekuwa zimefungwa,
wangeona kwa macho yao;
    wangesikia kwa masikio yao;
Iwapo wangeelewa kwa akili zao.
    Kisha wangenigeukia na kuponywa.’(A)

16 Bahati gani mliyonayo ninyi. Mnaelewa mnachokiona kwa macho yenu. Na mnaelewa mnachosikia kwa masikio yenu. 17 Ninaweza kuwathibitishia, manabii na watakatifu wengi walitaka kuona mnayoyaona. Lakini hawakuyaona. Walitaka kusikia mnayosikia sasa. Lakini hawakuyasikia.

Yesu Afafanua Simulizi Kuhusu Mbegu

(Mk 4:13-20; Lk 8:11-15)

18 Hivyo sikilizeni maana ya simulizi hiyo kuhusu mkulima:

19 Vipi kuhusu mbegu zilizoangukia njiani? Hizo zinafanana na watu wanaosikia mafundisho kuhusu ufalme wa Mungu lakini hawauelewi. Mwovu huja na kuyachukua yaliyopandwa katika mioyo yao.

20 Na vipi kuhusu mbegu zilizoangukia kwenye udongo wenye mawe? Hizo zinafanana na watu wanaosikia mafundisho haraka na kwa furaha huyapokea. 21 Lakini hawaruhusu mafundisho kutawala maisha yao. Huyatunza kwa muda mfupi. Mara tatizo au mateso yanapokuja kwa sababu ya mafundisho waliyoyapokea, wanaacha kuyafuata.

22 Na vipi kuhusu mbegu zilizoanguka katikati ya miiba? Hizo zinafanana na watu wanaosikia mafundisho lakini huyaruhusu mahangaiko ya maisha na kutaka utajiri, hufanya mafundisho yasikue. Hivyo mafundisho hayazai mazao mazuri katika maisha yao.

23 Lakini vipi kuhusu mbegu zilizoanguka kwenye udongo wenye rutuba? Hizo ni sawa na watu wanaosikia mafundisho na kuyaelewa. Hukua na kuzaa mazao mazuri, wakati mwingine mara mia, wakati mwingine mara sitini, na wakati mwingine mara thelathini zaidi.”

Simulizi Kuhusu Ngano na Magugu

24 Kisha Yesu akatumia simulizi nyingine kuwafundisha. Yesu akasema, “Ufalme wa Mungu unafanana na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. 25 Usiku ule, kila mtu alipokuwa amelala, adui wa yule mtu akaja na kupanda magugu katikati ya ngano kisha akaondoka. 26 Baadaye, ngano ikakua na vichwa vya nafaka vikaota juu ya mimea. Kisha mtumishi akayaona magugu. 27 Watumwa wa mwenye shamba wakaja na akasema, ‘Bwana ulipanda mimea mizuri kwenye shamba lako. Magugu yametoka wapi?’

28 Yule mtu akajibu, ‘Adui alipanda magugu.’

Wale watumwa wakauliza, ‘Je, unataka twende na kung'oa magugu?’

29 Akajibu, ‘Hapana, kwa sababu mtakapokuwa mnang'oa magugu, mtaweza pia kung'oa ngano. 30 Yaacheni magugu na ngano vikue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati wa mavuno nitawaambia wafanyakazi hivi: Kwanza, yakusanyeni magugu na kuyafunga pamoja ili myachome. Kisha kusanyeni ngano na kuileta ghalani mwangu.’”

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International