New Testament in a Year
Yesu Afundisha Kuhusu Kutoa
6 Mnapofanya jambo jema, kuweni waangalifu msilifanye mbele za watu wengine ili wawaone. Mtakapofanya hivyo hamtapata thawabu kutoka kwa Baba yenu wa mbinguni.
2 Unapowapa maskini na wahitaji, usilipigie mbiu sana jambo hilo. Maana hivyo ndivyo wanavyofanya wanafiki kwenye makusanyiko.[a] Wao hupiga mbiu kabla ya kutoa ili watu wawaone, kwa kuwa hutaka kila mtu awasifu. Ukweli ni kuwa, hiyo ndiyo thawabu yote waliyokwishapata. 3 Hivyo unapowapa maskini, mtu yeyote asijue unachofanya.[b] 4 Kutoa kwako kunapaswa kufanyika sirini kwa kuwa Baba yako huona mambo yanayofanywa sirini, naye atakupa thawabu.
Yesu Afundisha Kuhusu Maombi
(Lk 11:2-4)
5 Mnapoomba, msiwe kama wanafiki. Wanapenda kusimama kwenye masinagogi na kwenye pembe za mitaa na kuomba kwa kupaza sauti. Wanapenda kuonwa na watu. Ukweli ni kuwa hiyo ndiyo thawabu yote watakayopata. 6 Lakini unapoomba, unapaswa kuingia katika chumba chako cha ndani na ufunge mlango. Kisha mwombe Baba yako aliye mahali pa siri. Yeye anayaona mambo yanayofanyika katika siri na hivyo atakupa thawabu.
7 Na unapoomba usiwe kama watu wasiomjua Mungu. Wao kila wanapoomba wanarudia maneno yale yale, tena na tena, wakidhani kuwa wanapoyarudia maneno hayo mara nyingi watasikiwa na Mungu na kujibiwa maombi yao. 8 Msiwe kama wao. Baba yenu anajua yale mnayohitaji kabla hamjamwomba. 9 Hivyo, hivi ndivyo mnapaswa kuomba:
‘Baba yetu uliye mbinguni,
Jina lako lipewe utukufu.
10 Ufalme wako uje.
Mapenzi yako yafanyike hapa dunia,
kama yanavyofanyika huko mbinguni.
11 Utupe leo chakula tunachohitaji.
12 Utusamehe dhambi zetu,
kama tunavyowasamehe wale wanaotukosea.
13 Usiruhusu tukajaribiwa,
lakini utuokoe na Yule Mwovu.’[c]
14 Mkiwasemehe wengine makosa waliyowatendea, Baba yenu wa mbinguni naye atawasamehe makosa yenu pia. 15 Lakini msipowasamehe wengine, Baba Yenu wa mbinguni hatawasamehe ninyi.
Yesu Afundisha Kuhusu Kufunga
16 Mnapofunga, msijionyeshe kuwa na huzuni kama wanafiki wanavyofanya. Hukunja nyuso zao kwa kuonesha kuwa wana huzuni ili watu wawaone kuwa wamefunga. Ukweli ni kuwa wamekwishapata thawabu yao yote. 17 Hivyo unapofunga, nawa uso wako na ujiweke katika mwonekano mzuri, 18 ili watu wasijue kuwa umefunga, isipokuwa Baba yako, aliye nawe hata sirini. Anaweza kuona yanayofanywa sirini, naye atakupa thawabu.
© 2017 Bible League International