Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

New Testament in a Year

Read the New Testament from start to finish, from Matthew to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Mathayo 14:1-21

Herode Adhani Yesu ndiye Yohana Mbatizaji

(Mk 6:14-29; Lk 9:7-9)

14 Katika wakati huo, Herode, mtawala wa Galilaya, alisikia ambacho watu walikuwa wanasema kuhusu Yesu. Hivyo akawaambia watumishi wake, “Nadhani hakika mtu huyu ni Yohana Mbatizaji. Lazima amefufuka kutoka kwenye kifo, na ndiyo sababu anaweza kutenda miujiza hii.”

Kifo cha Yohana Mbatizaji

Kabla ya wakati huu, Herode alimkamata Yohana. Akamfunga kwa minyororo na kumweka gerezani. Alimkamata Yohana kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, kaka yake Herode. Yohana alikuwa amemwambia, “Si sahihi kwako kumwoa Herodia.” Herode alitaka kumwua, lakini aliwaogopa watu. Waliamini kuwa Yohana alikuwa nabii.

Siku ya kuzaliwa Herode, bintiye Herodia[a] alicheza mbele yake na kundi lake. Herode alifurahishwa naye sana. Hivyo aliapa kuwa atampa kitu chochote atakachotaka. Herodia alimshawishi binti yake kitu cha kuomba. Hivyo bintiye akamwambia Herode, “Nipe hapa kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sahani kubwa.”

Mfalme Herode alihuzunika sana. Lakini alikuwa ameahidi kumpa binti kitu chochote alichotaka. Na watu waliokuwa wakila pamoja na Herode walikuwa wamesikia ahadi yake. Hivyo Herode aliamuru kitu ambacho alikuwa ameomba apatiwe. 10 Akawatuma wanaume gerezani, ambako walikikata kichwa cha Yohana. 11 Na watu wakakileta kichwa cha Yohana kwenye sahani kubwa na kumpa yule msichana. Kisha yeye akakipeleka kichwa kwa mama yake, Herodia. 12 Wafuasi wa Yohana wakaja na kuuchukua mwili wa Yohana na kuuzika. Kisha wakaenda na kumwambia Yesu kilichotokea.

Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 5,000

(Mk 6:30-44; Lk 9:10-17; Yh 6:1-14)

13 Yesu aliposikia kilichotokea kwa Yohana, aliondoka kwa kutumia mtumbwi. Alikwenda peke yake mpaka mahali ambapo hakuna aliyekuwa akiishi. Lakini watu walisikia kuwa Yesu alikuwa ameondoka. Hivyo waliondoka katika miji na kumfuata. Walikwenda mahali alikokwenda kupitia nchi kavu. 14 Yesu alipotoka katika mtumbwi, aliwaona watu wengi. Akawahurumia, na kuwaponya waliokuwa wagonjwa.

15 Baadaye mchana huo, wafuasi walimwendea Yesu na kusema, “Hakuna anayeishi katika eneo hili. Na tayari muda umepita, hivyo waage watu ili waende katika miji na kujinunulia chakula.”

16 Yesu akasema, “Watu hawahitaji kuondoka. Wapeni ninyi chakula wale.”

17 Wafuasi wakajibu, “Lakini tuna mikate mitano na samaki wawili tu.”

18 Yesu akasema, “Leteni kwangu mikate na samaki.” 19 Kisha akawaambia watu waketi chini kwenye nyasi. Akaichukua mikate mitano na samaki wawili. Akatazama mbinguni na akamshukuru Mungu kwa ajili ya chakula. Kisha akaivunja mikate katika vipande, akawapa wafuasi wake nao wakawapa watu chakula. 20 Kila mmoja alikula mpaka akashiba. Walipomaliza kula, wafuasi walijaza vikapu kumi na mbili vya vipande vilivyosalia. 21 Walikuwepo wanaume 5,000, pamoja na wanawake na watoto waliokula.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International