New Testament in a Year
Yesu Atumia Mfano wa Wakulima Katika Shamba la Mizabibu
20 Ufalme wa Mungu umefanana na mtu aliyemiliki shamba la mizabibu. Asubuhi mmoja akatoka kwenda kuajiri watu ili walime katika shamba lake la mizabibu. 2 Alikubaliana nao kuwa atawalipa sarafu moja ya fedha ikiwa watafanya kazi siku ile. Kisha akawapeleka kwenye shamba la mizabibu kulima.
3 Ilipofika saa tatu asubuhi mtu huyo alitoka na kwenda sokoni ambako aliwaona baadhi ya watu wamesimama na hawafanyi kazi yo yote. 4 Akawaambia, ‘Ikiwa mtakwenda kufanya kazi shambani kwangu, nitawalipa kutokana na kazi yenu.’ 5 Hivyo walikwenda kufanya kazi kwenye shamba lake la mizabibu.
Ilipofika saa sita mchana na saa tisa alasiri alitoka tena. Na nyakati zote mbili aliwaajiri watu wengine waende kufanya kazi shambani mwake. 6 Ilipofika saa kumi na moja alikwenda sokoni tena. Akawaona watu wengine wamesimama pale. Akawauliza, ‘Kwa nini mmesimama hapa siku nzima na hamfanyi kazi?’
7 Wakasema, ‘Hakuna aliyetupa kazi.’
Mwenye shamba akawaambia, ‘Basi mnaweza kwenda kufanya kazi katika shamba langu la mizabibu.’
8 Mwishoni mwa siku, mwenye shamba akamwambia msimamizi wa wafanyakazi wote, ‘Waite wafanyakazi na uwalipe wote. Anza kwa kulipa watu niliowaajiri mwishoni, na malizia kwa wale niliowaajiri mwanzoni.’
9 Wafanyakazi walioajiriwa saa kumi na moja jioni walipata malipo yao. Kila mfanyakazi alipata sarafu moja ya fedha. 10 Ndipo wafanyakazi walioajiriwa kwanza wakaja kupokea malipo yao. Walidhani wangelipwa zaidi ya wengine. Lakini kila mmoja wao alipokea sarafu moja ya fedha. 11 Walipopata sarafu ya fedha, walimlalamikia mmiliki wa shamba. 12 Walisema, ‘Watu hao walioajiriwa mwishoni wamefanya kazi saa moja tu. Lakini umewalipa sawa na sisi. Na tumefanya kazi siku nzima kwenye jua kali.’
13 Lakini mmiliki wa shamba akamwambia mmoja wao, ‘Rafiki, nimekulipa kama tulivyopatana, ulikubali kufanya kazi kwa malipo ya sarafu moja ya fedha. Sawa? 14 Hivyo chukua malipo yako na uende. Ninataka kumlipa mtu niliyemwajiri mwishoni sawa na kiasi nilichokulipa. 15 Ninaweza kufanya chochote ninachotaka na pesa yangu. Wewe unao wivu[a] na unataka kuwadhuru wengine kwa kuwa mimi ni mkarimu?’
16 Hivyo walio wa mwisho sasa watakuwa wa kwanza siku zijazo. Na walio wa kwanza sasa watakuwa wa mwisho siku zijazo.”
© 2017 Bible League International