New Testament in a Year
Yesu ni Bwana Juu ya Siku ya Sabato
(Mk 2:23-28; Lk 6:1-5)
12 Katika wakati huo huo, Yesu alikuwa anasafiri akipita katika mashamba ya nafaka siku ya Sabato. Wafuasi wake walikuwa pamoja naye, na walikuwa na njaa. Hivyo walianza kuchuma nafaka na kula. 2 Mafarisayo walioliona hili, wakamwambia Yesu, “Tazama! Wafuasi wako wanafanya kitu ambacho ni kinyume na sheria yetu kufanya katika siku ya Sabato.”
3 Yesu akawaambia, “Mmekwisha soma alichofanya Daudi wakati yeye na wale waliokuwa pamoja naye walipokuwa na njaa. 4 Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu. Yeye na wale waliokuwa pamoja naye walikula mkate uliotolewa kwa Mungu. Ilikuwa kinyume cha sheria kwa Daudi au wale waliokuwa pamoja naye kula mkate huo. Makuhani pekee ndio walioruhusiwa kuula. 5 Na mmekwisha soma katika Sheria ya Musa kuwa katika kila Sabato makuhani kwenye Hekalu wanavunja Sheria kwa kufanya kazi Siku ya Sabato. Lakini hawakosei kwa kufanya hivyo. 6 Ninawaambia kuwa kuna kitu hapa ambacho ni kikuu kuliko Hekalu. 7 Maandiko yanasema, ‘Sihitaji dhabihu ya wanyama; Ninataka ninyi muoneshe wema kwa watu.’(A) Hakika hamjui hilo linamaanisha nini. Iwapo mngelielewa, msingewahukumu wale ambao hawajafanya chochote kibaya.
8 Mwana wa Adamu ni Bwana juu ya siku ya Sabato.”
Yesu Amponya Mtu Siku ya Sabato
(Mk 3:1-6; Lk 6:6-11)
9 Kutoka hapo Yesu alikwenda katika sinagogi lao. 10 Ndani ya sinagogi alikuwemo mtu aliyepooza mkono. Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa pale walikuwa wanatafuta sababu ya kumshitaki Yesu kwa kutenda kitu kibaya, hivyo walimuuliza, “Je, ni halali kuponya siku ya Sabato?”
11 Yesu akajibu, “Ikiwa mmoja wenu ana kondoo na akatumbukia shimoni siku ya Sabato, utamsaidia kumtoa yule kondoo katika shimo. 12 Hakika mtu ni bora kuliko kondoo. Hivyo ni sawa kutenda wema siku ya Sabato.”
13 Kisha Yesu akamwambia mtu mwenye mkono uliopooza, “Unyooshe mkono wako.” Mtu yule akaunyoosha mkono wake, na ukawa mzima tena, kama mkono mwingine. 14 Lakini Mafarisayo waliondoka na wakaweka mipango ya kumuua Yesu.
Yesu ni Mtumishi Aliyechaguliwa na Mungu
15 Yesu alitambua kuwa Mafarisayo walikuwa wanapanga kumuua. Hivyo aliondoka mahali pale na watu wengi walimfuata. Akawaponya wote waliokuwa wagonjwa, 16 lakini aliwaonya wasiwaambie wengine yeye alikuwa nani. 17 Hii ilikuwa ni kuthibitisha kile ambacho nabii Isaya alisema alipozungumza kwa niaba ya Mungu:
18 “Hapa ni mtumishi wangu,
niliyemchagua.
Ndiye ninayempenda,
na ninapendezwa naye.
Nitamjaza Roho yangu,
naye ataleta haki kwa mataifa.
19 Hatabishana au kupiga kelele;
hakuna atakayesikia sauti yake mitaani.
20 Hatavunja wala kupindisha unyasi.
Hatazimisha hata mwanga hafifu.
Hatashindwa mpaka ameifanya haki kuwa mshindi.
21 Watu wote watatumaini katika yeye.”(B)
Nguvu ya Yesu Inatoka kwa Mungu
(Mk 3:20-30; Lk 11:14-23; 12:10)
22 Kisha baadhi ya watu wakamleta mtu kwa Yesu. Mtu huyu alikuwa asiyeona na hakuweza kuzungumza, kwa sababu alikuwa na pepo ndani yake. Yesu akamponya na akaweza kuzungumza na kuona. 23 Watu wote walikishangaa kile Yesu alichotenda. Walisema, “Pengine ni Mwana wa ahadi wa Daudi!”
© 2017 Bible League International