Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

New Testament in a Year

Read the New Testament from start to finish, from Matthew to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Mathayo 14:22-36

Yesu Atembea Juu ya Maji

(Mk 6:45-52; Yh 6:16-21)

22 Mara baada ya hili Yesu akawaambia wafuasi wake wapande kwenye mtumbwi. Akawaambia waende upande mwingine wa ziwa. Aliwaambia angekuja baadaye, alikaa pale ili kuwaaga watu. 23 Baada ya Yesu kuwaaga watu, alikwenda kwenye vilima peke yake kuomba. Ikawa jioni na alikuwa pale peke yake. 24 Wakati huu mtumbwi ilikuwa mbali kutoka pwani. Kwa kuwa upepo ulikuwa unavuma kinyume na mtumbwi, mtumbwi ulikuwa unapata msukosuko kwa sababu ya mawimbi.

25 Kati ya saa tisa na saa kumi na mbili asubuhi, wafuasi wa Yesu walikuwa bado ndani ya mtumbwi. Yesu akaenda kwao akitembea juu ya maji. 26 Iliwatisha walipomwona anatembea juu ya maji. Wakapiga kelele kwa woga “Ni mzuka!”

27 Lakini haraka Yesu akawaambia, “Msihofu! Ni mimi! Msiogope.”

28 Petro akasema, “Bwana, ikiwa hakika ni wewe, niambie nije kwako juu ya maji.”

29 Yesu akasema, “Njoo, Petro.”

Kisha Petro akauacha mtumbwi na kutembea juu ya maji kumwelekea Yesu. 30 Lakini Petro alipokuwa anatembea juu ya maji, aliyaona mawimbi na upepo. Aliogopa na kuanza kuzama katika maji. Akapiga kelele, “Bwana, niokoe!”

31 Haraka Yesu akamshika Petro kwa mkono wake. Akasema, “Imani yako ni ndogo. Kwa nini ulisita?”

32 Baada ya Petro na Yesu kuingia kwenye mtumbwi, upepo ukakoma. 33 Kisha wafuasi wakamwabudu Yesu na kusema, “Hakika wewe ni Mwana wa Mungu.”

Yesu Awaponya Watu Wengi Wagonjwa

(Mk 6:53-56)

34 Baada ya kuvuka ziwa, wakafika pwani katika eneo la Genesareti. 35 Baadhi ya watu pale wakamwona Yesu na wakamtambua kuwa ni nani. Hivyo wakatuma ujumbe kwa watu wengine katika eneo lote kuwa Yesu amekuja. Watu wakawaleta wagonjwa wao wote kwake. 36 Walimsihi Yesu awaruhusu waguse tu upindo wa vazi lake ili waponywe. Na wagonjwa wote waliogusa vazi lake waliponywa.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International