New Testament in a Year
Yesu Awatuma Kazi Mitume Wake
(Mk 3:13-19; 6:7-13; Lk 6:12-16; 9:1-6)
10 Yesu aliwaita pamoja wafuasi wake kumi na mbili. Akawapa uwezo juu ya pepo wabaya ili waweze kuwafukuza na pia kuponya kila aina ya magonjwa na maradhi. 2 Haya ni majina ya mitume kumi na wawili:
Simoni (ambaye pia aliitwa Petro),
Andrea, kaka yake Petro,
Yakobo, mwana wa Zebedayo,
Yohana, kaka yake Yakobo,
3 Filipo,
Bartholomayo,
Thomaso,
Mathayo, mtoza ushuru,
Yakobo, mwana wa Alfayo,
Thadayo,
4 Simoni Mzelote,
Yuda Iskariote (yule ambaye baadaye alimsaliti Yesu).
5 Yesu aliwatuma mitume hawa kumi na wawili pamoja na maelekezo haya: “Msiende kwa watu wasio Wayahudi. Na msiingie katika miji ambako Wasamaria wanaishi. 6 Lakini nendeni kwa watu wa Israeli. Wako kama kondoo waliopotea. 7 Mtakapokwenda, waambieni hivi: ‘Ufalme wa Mungu umekaribia.’ 8 Waponyeni wagonjwa. Fufueni waliokufa. Waponyeni watu wenye magonjwa mabaya sana ya ngozi. Na toeni mashetani kwa watu. Ninawapa nguvu hii bure, hivyo wasaidieni wengine bure. 9 Msibebe pesa pamoja nanyi; dhahabu au fedha au shaba nyekundu. 10 Msibebe mikoba. Chukueni nguo na viatu mlivyovaa tu. Na msichukue fimbo ya kutembelea. Mfanyakazi anastahili kupewa anachohitaji.
11 Mnapoingia katika mji, tafuteni kwa makini hadi mumpate mtu anayefaa na mkae katika nyumba yake mpaka mtakapoondoka mjini. 12 Mtakapoingia katika nyumba hiyo, semeni, ‘Amani iwe kwenu.’ 13 Ikiwa watu katika nyumba hiyo watawakaribisha, wanastahili amani yenu. Wapate amani mliyowatakia. Lakini ikiwa hawatawakaribisha, hawastahili amani yenu. Ichukueni amani mliyowatakia. 14 Na ikiwa watu katika nyumba au mji watakataa kuwapokea au kuwasikiliza, basi ondokeni mahali hapo na mkung'ute mavumbi kutoka katika miguu yenu. 15 Ninaweza kuwathibitishia kuwa siku ya hukumu itakuwa vibaya sana kwa mji huo kuliko watu wa Sodoma na Gomora.[a]
Yesu Aonya Kuhusu Matatizo
(Mk 13:9-13; Lk 21:12-17)
16 Sikilizeni! Ninawatuma, nanyi mtakuwa kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. Hivyo muwe na akili kama nyoka. Lakini pia muwe kama njiwa na msimdhuru yeyote. 17 Muwe waangalifu! Wapo watu watakaowakamata na kuwapeleka ili kuwashitaki mbele ya mabaraza ya mijini. Watawachapa ndani ya masinagogi yao. 18 Mtasimamishwa mbele ya magavana na wafalme. Watu watawafanyia ninyi hivi kwa sababu mnanifuata. Mtakuwa mashahidi wangu mbele za wafalme na magavana hao na kwa watu wa mataifa mengine. 19 Mtakapokamatwa, msisumbuke kuhusu nini mtakachosema au namna gani mtakavyosema. Katika wakati huo mtapewa maneno ya kusema. 20 Si ninyi mtakaoongea; Roho wa Baba Mungu wenu atakuwa anaongea kupitia ninyi.
© 2017 Bible League International