New Testament in a Year
Simulizi Kuhusu Msamaha
21 Kisha Petro akamwendea Yesu na kumwuliza, “Bwana, ndugu yangu akiendelea kunikosea, ninapaswa kumsamehe anaponikosea mara ngapi? Mara saba?”
22 Yesu akamjibu, “Ninakwambia, ni lazima umsamehe zaidi ya mara saba. Ni lazima uendelee kumsamehe hata kama atakukosea saba mara sabini.[a]
23 Ninawaambia kwa sababu ufalme wa Mungu unafanana na mfalme aliyetaka kupata taarifa kutoka kwa watumishi wake. 24 Mtumishi aliyekuwa anadaiwa na mfalme tani 300[b] za fedha aliletwa kwake. 25 Hakuwa na fedha za kutosha kulipa deni lake. Hivyo mfalme aliamuru kila kitu anachomiliki mtumishi yule kiuzwe ikiwa ni pamoja na mke na watoto wake.
26 Lakini mtumishi alipiga magoti na kumsihi mfalme akisema, ‘Nivumilie. Nitakulipa kila kitu unachonidai.’ 27 Mfalme alimhurumia. Hivyo akamsamehe yule mtumishi deni lote na akamwacha aende akiwa huru.
28 Lakini mtumishi huyo alipoondoka, alimwona mtumishi mwingine aliyekuwa anamdai sarafu mia za fedha. Akamkaba shingo yake na akasema, ‘Nilipe pesa ninayokudai!’
29 Mtumishi anayedaiwa akapiga magoti na kumsihi akisema, ‘Nivumilie. Nitakulipa kila kitu unachonidai.’
30 Lakini mtumishi wa kwanza alikataa kumvumilia. Alimwambia hakimu kuwa alikuwa anamdai pesa, na mtumishi yule alitupwa gerezani mpaka atakapoweza kulipa deni lake. 31 Watumishi wengine walipoona hili, walimhurumia mtumishi aliyefungwa gerezani. Hivyo walienda na kumwambia mfalme kila kitu kilichotokea.
32 Ndipo mfalme alimwita msimamizi wa kwanza na kumwambia, ‘Wewe ni mbaya sana! Ulinisihi nikusamehe deni lako, na nilikuacha ukaondoka bila kulipa kitu chochote! 33 Hivyo ulipaswa kumpa mtu yule mwingine anayetumika pamoja nawe rehema ile ile niliyokupa mimi.’ 34 Mfalme alikasirika sana. Hivyo alifungwa gerezani mpaka atakapoweza kulipa kila kitu anachodaiwa.
35 Mfalme huyu alifanya kama ambavyo Baba yangu wa mbinguni atawafanyia ninyi. Ni lazima umsamehe ndugu au dada yako kwa moyo wako wote, usipofanya hivyo, Baba yangu wa mbinguni hatakusamehe wewe.”
© 2017 Bible League International