Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
2 Ninamjua mtu mmoja[a] katika Kristo aliyechukuliwa juu katika mbingu ya tatu. Hili lilitokea miaka 14 iliyopita. Sifahamu ikiwa mtu huyu alikuwa ndani ya mwili wake au nje ya mwili wake, lakini Mungu anajua. 3-4 Na ninajua kuwa mtu huyu alichukuliwa juu paradiso. Sijui kama alikuwa katika mwili wake au nje ya mwili wake. Mungu pekee ndiye anajua. Lakini mtu huyu aliyasikia mambo ambayo hana uwezo wa kuyasimulia. Alisikia mambo ambayo mtu yeyote anaruhusiwa kuyasema. 5 Nitajivunia mtu wa namna hiyo, lakini sitajivuna juu yangu mwenyewe. Nitajivuna tu katika madhaifu yangu.
6 Lakini ikiwa nilitaka kujivuna, sitakuwa nikizungumza kama mjinga, kwa sababu ningekuwa nasema iliyo kweli. Lakini sitajivuna tena zaidi, kwa sababu sitaki watu wanifikirie kwa ubora zaidi kuliko wanavyoniona nikitenda ama kusikia ninayosema.
7 Lakini imenipasa kutojivuna zaidi juu ya mambo ya ajabu yaliyoonyeshwa kwangu. Kwa sababu hiyo nilipewa tatizo lenye maumivu;[b] malaika toka kwa Shetani; aliyetumwa kwangu kunitesa, ili nisiweze kufikiri kwamba mimi ni bora zaidi kuliko watu wengine. 8 Nilimwomba Bwana mara tatu kuliondoa tatizo hili kwangu. 9 Lakini Bwana alisema, “Neema yangu ndiyo unayoihitaji. Ni pale tu unapokuwa dhaifu ndipo kila kitu kinapoweza kufanyika katika uwezo wangu.” Hivyo nitajivunia udhaifu wangu kwa furaha. Hapo ndipo uweza wa Kristo unaweza kukaa ndani yangu. 10 Ndiyo, nina furaha kuwa na madhaifu ikiwa ni kwa ajili ya Kristo. Nina furaha kuaibishwa na kupitia magumu. Nina furaha ninapoteswa na kupata matatizo, kwa sababu ni pale nilipodhaifu ndipo ninapokuwa na nguvu.
Yesu Aenda Kwenye Mji wa Kwao
(Mt 13:53-58; Lk 4:16-30)
6 Yesu akaondoka pale, na kwenda katika mji wa kwao; na wanafunzi wake wakamfuata. 2 Sabato ilipofika, alianza kufundisha katika sinagogi. Watu wengi walishangazwa walipomsikiliza. Wakasema, “Mtu huyu alipata wapi mambo haya? Alipata wapi hekima hii? Na anaifanyaje miujiza hii inayofanyika kwa mikono yake? 3 Je, yeye si yule seremala? Je, yeye si mwana wa Maria? Je, yeye si kaka yake Yakobo, Yusufu, Yuda, na Simoni? Je, dada zake hawaishi hapa katika mji wetu?” Kulikuwa na vikwazo vilivyowazuia wasimkubali.
4 Yesu akawaambia, “kila mtu humheshimu nabii isipokuwa watu wa mji wa kwao mwenyewe, jamaa zake mwenyewe na wale wa nyumbani mwake mwenyewe.” 5 Yesu hakuweza kufanya miujiza ya aina yoyote pale, isipokuwa aliweka mikono juu ya wagonjwa wachache na kuwaponya. 6 Naye akashangazwa na jinsi watu wa mji wa kwao mwenyewe walivyokosa kuwa na imani. Kisha Yesu alizunguka vijijini akiwafundisha watu.
Yesu Awatuma Kazi Mitume Wake
(Mt 10:1,5-15; Lk 9:1-6)
7 Akawaita kwake wanafunzi wake kumi na wawili, na akaanza kuwatuma wawili wawili. Akawapa uwezo wa kuwaweka huru watu kutoka pepo wachafu. 8 Akawapa amri kuwa wasichukue kitu chochote kwa ajili ya safari yao isipokuwa fimbo; hawakupaswa kuchukua mkate, mfuko, hata kubeba fedha kwenye mikanda yao. 9 Aliwaruhusu kuvaa makobazi lakini wasichukue kanzu ya pili. 10 Naye akawambia, “ikiwa mtu atawapa mahali pa kuishi mkae katika nyumba hiyo kwa muda wote mtakapokuwa katika mji ule msihamehame kutoka nyumba moja hadi nyingine. 11 Ikiwa hamtakaribishwa ama kusikilizwa katika mji wowote au mahali popote, kwa kuwaonya kunguteni mavumbi toka miguuni mwenu.”
12 Kwa hiyo mitume wakatoka na kuhubiri ili watu watubu. 13 Mitume wakafukuza mashetani wengi na kuwapaka mafuta ya mizeituni[a] wagonjwa wengi na kuwaponya.
© 2017 Bible League International