Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Paulo Akiwa Athene
16 Paulo alipokuwa akiwasubiri Sila na Timotheo katika mji wa Athene, aliudhika kwa sababu aliona mji ulikuwa umejaa sanamu. 17 Alipokuwa katika sinagogi alizungumza na Wayahudi na Wayunani waliokuwa wakimwabudu Mungu wa kweli. Alikwenda pia katika sehemu za wazi za umma za mikutano na kuzungumza na kila aliyekutana naye. 18 Baadhi ya wanafalsafa Waepikureo[a] na baadhi ya wanafalsafa Wastoiko[b] walibishana naye.
Baadhi yao walisema, “Mtu huyu hakika hajui anachokisema. Anajaribu kusema nini?” Paulo alikuwa anawaambia Habari Njema kuhusu Yesu na ufufuo. Hivyo walisema, “Anaonekana anatueleza kuhusu baadhi ya miungu wa kigeni.”
19 Walimchukua Paulo kwenye mkutano wa baraza la Areopago. Wakasema, “Tafadhali tufafanunile hili wazo jipya ambalo umekuwa ukifundisha. 20 Mambo unayosema ni mapya kwetu. Hatujawahi kusikia mafundisho haya, na tunataka kufahamu yana maana gani.” 21 (Watu wa Athene na wageni walioishi pale walitumia muda wao bila kufanya kazi yoyote isipokuwa kusikiliza na kuzungumza kuhusu mawazo mapya.)
22 Ndipo Paulo alisimama mbele ya mkutano wa baraza la Areopago na kusema, “Watu wa Athene, kila kitu ninachokiona hapa kinanionyesha kuwa ninyi ni watu wa dini sana. 23 Nilikuwa natembea katika mji wenu na nimeona mambo mnayoyaabudu. Niliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya juu yake: ‘Kwa Mungu Asiyejulikana.’ Mnamwabudu mungu msiyemjua. Huyu ni Mungu ninayetaka kuwaambia habari zake.
24 Ni Mungu aliyeumba ulimwengu na kila kitu ndani yake. Ni Bwana wa mbingu na nchi. Haishi katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya kibinadamu. 25 Ndiye anayewapa watu uzima, pumzi na kila kitu wanachohitaji. Hahitaji msaada wowote kutoka kwao. Ana kila kitu anachohitaji. 26 Mungu alianza kwa kumwumba mtu mmoja, na kutoka kwake aliumba mataifa yote mbalimbali, na akawaweka kila mahali ulimwenguni. Na aliamua ni wakati gani na wapi ambapo angewaweka ili waishi.
27 Mungu alitaka watu wamtafute yeye, na pengine kwa kumtafuta kila mahali, wangempata. Lakini hayuko mbali na kila mmoja wetu. 28 Ni kupitia Yeye tunaweza kuishi, kufanya yale tunayofanya na kuwa kama tulivyo. Kama baadhi ya methali zenu zilivyokwisha sema, ‘Sote tunatokana naye.’
29 Huo ndio ukweli. Sote tunatokana na Mungu. Hivyo ni lazima msifikiri kuwa Yeye ni kama kitu ambacho watu hukidhania au kukitengeneza. Hivyo ni lazima tusifikiri kuwa ametengenezwa kwa dhahabu, fedha au jiwe. 30 Hapo zamani watu hawakumwelewa Mungu, naye Mungu hakulijali hili. Lakini sasa anawaagiza wanadamu kila mahali kubadilika na kumgeukia Yeye. 31 Amekwisha chagua siku ambayo atawahukumu watu wote ulimwenguni katika namna isiyo na upendeleo. Atafanya hili kwa kumtumia mtu aliyemchagua zamani zilizopita. Na alithibitisha kwa kila mtu kwamba huyu ndiye mtu atakayefanya. Alilithibitisha kwa kumfufua kutoka kwa wafu!”
© 2017 Bible League International