Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Mwana wa Mungu yu sawa na Mungu
15 Hakuna anayeweza kumwona Mungu,
lakini Mwana anafanana kabisa na Mungu.
Anatawala juu ya kila kitu kilichoumbwa.
16 Kwa uweza wake, vitu vyote viliumbwa:
vitu vya angani na ardhini, vinavyoonekana na visivyoonekana,
watawala wote wa kiroho, wakuu, enzi, na mamlaka.
Kila kitu kiliumbwa kupitia Yeye na kwa ajili yake.
17 Mwana alikuwapo kabla ya kuumbwa kitu chochote,
na vyote vinaendelea kuwepo kwa sababu yake.
18 Yeye ni kichwa cha mwili,
yaani kanisa.
Yeye ni mwanzo wa maisha yajayo,
ni wa kwanza miongoni mwa wote watakaofufuliwa kutoka kwa wafu.[a]
Hivyo katika mambo yote yeye ni mkuu zaidi.
19 Mungu alipendezwa kwamba ukamilifu wa uungu wake
uishi ndani ya Mwana.
20 Na kupitia Yeye, Mungu alifurahi
kuvipatanisha tena vitu vyote kwake Yeye mwenyewe;
vilivyoko mbinguni na vilivyoko duniani.
Mungu alileta amani kupitia sadaka ya damu ya Mwanaye msalabani.
21 Hapo mwanzo mlitengwa na Mungu, na mlikuwa adui zake katika fikra zenu, kwa sababu ya maovu mliyotenda kinyume naye. 22 Lakini sasa amewafanya kuwa marafiki zake tena, kupitia kifo cha Kristo katika mwili wake. Ili kwa njia hiyo awalete kwake mkiwa watakatifu, msio na lawama na msiohukumiwa jambo lolote mbele zake; 23 na hiki ndicho kitatokea mkiendelea kuiamini Habari Njema mliyoisikia. Mwendelee kuwa imara na kudumu katika imani. Jambo lolote lisiwafanye mkaliacha tumaini lenu mlilopokea mlipoisikia Habari Njema. Habari Njema ile ile ambayo imehubiriwa kwa kila mtu duniani, ndiyo kazi ambayo mimi, Paulo, nilipewa kufanya.
© 2017 Bible League International