Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Paulo Azungumza na Wazee kutoka Efeso
17 Tukiwa Mileto Paulo alitume ujumbe kwenda Efeso, akiwaambia wazee wa kanisa la Efeso waje kwake.
18 Walipofika, Paulo akawaambia, “Mnafahamu kuhusu maisha yangu tangu siku ya kwanza nilipofika Asia. Mnafahamu namna nilivyoishi wakati wote nilipokuwa pamoja nanyi. 19 Wayahudi walipanga hila kinyume nami, na hila zao zilinisababishia matatizo mengi. Lakini mnafahamu kwamba daima nilimtumikia Bwana, nyakati zingine kwa machozi. Sikujipendelea mimi mwenyewe kwanza. 20 Daima niliwatendea mema. Niliwahubiri Habari Njema kuhusu Yesu sehemu za wazi mbele ya watu na pia nilifundisha katika nyumba zenu. 21 Nilimwambia kila mtu, Myahudi na Myunani, kubadilika na wakamgeukia Mungu. Niliwaambia wote wamwamini Bwana wetu Yesu.
22 Lakini sasa ni lazima nimtii Roho na kwenda Yerusalemu. Sifahamu nini kitanipata huko. 23 Ninafahamu kitu kimoja kwamba katika kila mji Roho Mtakatifu huniambia kwamba matatizo na hata kufungwa gerezani kunanisubiri. 24 Siujali uhai wangu mwenyewe. Jambo la muhimu zaidi ni mimi kuimaliza kazi yangu. Ninataka niimalize huduma ambayo Bwana Yesu alinipa niifanye, nayo ni kuwahubiri watu Habari Njema kuhusu neema ya Mungu.
25 Na sasa nisikilizeni. Ninafahamu kwamba hakuna mmoja wenu atakayeniona tena. Wakati wote nilipokuwa pamoja nanyi, niliwahubiri Habari Njema kuhusu ufalme wa Mungu. 26 Hivyo leo ninaweza kuwaambia kitu kimoja ambacho nina uhakika nacho: Mungu hatanilaumu ikiwa baadhi yenu hamtaokoka. 27 Ninaweza kusema hivi kwa sababu ninajua niliwaambia yote ambayo Mungu anataka mfahamu. 28 Jilindeni ninyi wenyewe pamoja na watu wote mliopewa na Mungu. Naye Roho Mtakatifu amewapa ninyi kazi ya kuwachunga[a] kondoo hawa.[b] Ni lazima muwe wachungaji wa kanisa la Mungu,[c] watu ambao Mungu aliwanunua kwa damu ya Mwanaye wa pekee.[d] 29 Ninafahamu ya kwamba nikishaondoka, baadhi ya watu watakuja kwenye kundi letu. Watakuwa kama mbwa mwitu na watajaribu kuwaangamiza kondoo. 30 Pia, watu kutoka kwenye kundi lenu wenyewe wataanza kufundisha mambo yasiyo sahihi. Watawaongoza baadhi ya wafuasi wa Bwana mbali na kweli ili wawafuate katika upotovu wao. 31 Hivyo iweni waangalifu! Na daima kumbukeni mambo niliyofanya kwa miaka mitatu nilipokuwa pamoja nanyi. Sikuacha kumkumbusha kila mmoja wenu jinsi anavyopaswa kuishi, nikiwashauri usiku na mchana na kulia kwa ajili yenu.
32 Sasa ninawaweka katika uangalizi wa Mungu. Ninategemea ujumbe wa neema yake kuwaimarisha ninyi. Ujumbe huo unaweza kuwapa ninyi baraka ambazo Mungu huwapa watakatifu wake wote. 33 Nilipokuwa pamoja nanyi, sikutamani pesa ya mtu yeyote au nguo nzuri. 34 Mnafahamu kwamba daima nilifanya kazi kwa mikono yangu mwenyewe ili nimudu mahitaji yangu mwenyewe na mahitaji ya watu waliokuwa pamoja nami. 35 Daima niliwaonesha kwamba mnapaswa kufanya kazi nilivyofanya na kuwasaidia wadhaifu. Niliwafundisha kukumbuka maneno ya Bwana Yesu aliyosema, ‘Ni baraka kuu kutoa kuliko kupokea.’”
36 Paulo alipomaliza kuzungumza, alipiga magoti chini, na wote waliomba pamoja. 37-38 Walilia sana. Kilichowahuzunisha sana ilikuwa kauli ya Paulo alipowaambia kuwa hawatamwona tena. Walimkumbatia na kumbusu. Kisha walikwenda pamoja naye mpaka kwenye meli na wakaagana naye.
© 2017 Bible League International