Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
27 Siku saba zilipokuwa zinakaribia kumalizika, baadhi ya Wayahudi kutoka Asia walimwona Paulo katika eneo la Hekalu. Wakamshawishi kila mtu, kisha wakakusanyika kama kundi wakiwa na hasira, kisha wakamkamata Paulo 28 na wakapiga kelele wakisema, “Watu wa Israeli, tusaidieni! Huyu ndiye mtu anayefundisha mambo yaliyo kinyume na Sheria ya Musa, kinyume na watu wetu, na kinyume na Hekalu letu. Hivi ndivyo anavyowafundisha watu kila mahali. Na sasa amewaleta baadhi ya Wayunani katika eneo la Hekalu na amepanajisi mahali hapa patakatifu!” 29 (Wayahudi walisema hili kwa kuwa walimwona Trofimo akiwa na Paulo Yerusalemu. Trofimo alikuwa mwenyeji wa Efeso, Wayahudi walidhani kuwa Paulo alikuwa amempeleka eneo takatifu la Hekalu.)
30 Watu katika mji wote wakajaa hasira, na kila mtu akaja akikimbilia kwenye Hekalu. Wakamkamata Paulo na kumtoa nje ya eneo takatifu, malango ya Hekalu yakafungwa saa hiyo hiyo. 31 Walipokuwa wanajaribu kumwua Paulo, Kamanda wa jeshi la Rumi katika mji wa Yerusalemu akapata taarifa kuwa ghasia zilikuwa zimeenea mji wote. 32 Mara hiyo hiyo kamanda alikimbilia mahali ambako umati wa watu ulikuwa umekusanyika, aliwachukua baadhi ya maofisa wa jeshi na askari. Watu walipomwona kamanda na askari wake waliacha kumpiga Paulo.
33 Kamanda alikwenda mahali alipokuwa Paulo na akamkamata. Akawaambia askari wake wamfunge kwa minyororo miwili. Kisha akauliza, “Mtu huyu ni nani? Amefanya nini kibaya?” 34 Baadhi ya watu pale walipiga kelele wakisema kitu hiki na wengine walisema kingine. Kwa sababu ya kuchanganyikiwa huku na kelele kamanda hakujua ukweli kuhusu kilichotokea. Hivyo akawaambia askari wamchukue Paulo mpaka kwenye jengo la jeshi. 35-36 Umati wote ulikuwa unawafuata. Askari walipofika kwenye ngazi ilibidi wambebe Paulo. Walifanya hivi ili kumlinda, kwa sababu watu walikuwa tayari kumwumiza. Watu walikuwa wanapiga kelele wakisema, “Auawe!”
37 Askari walipokuwa tayari kumwingiza Paulo kwenye jengo la jeshi, Paulo alimwuliza kamanda akasema, “Je, ninaweza kukwambia kitu?”
Kamanda akasema, “Kumbe, unaongea Kiyunani? 38 Kwa hiyo wewe si mtu niliyemdhania. Nilidhani wewe ni Mmisri aliyeanzisha vurugu dhidi ya serikali siku si nyingi na akawaongoza magaidi elfu nne kwenda jangwani.”
39 Paulo akasema, “Hapana, Mimi ni Myahudi kutoka Tarso katika jimbo la Kilikia. Ni raia wa mji ule muhimu. Tafadhali niruhusu niseme na watu.”
© 2017 Bible League International