Add parallel Print Page Options

Yesu Aenda Kwenye Mji wa Kwao

(Mt 13:53-58; Mk 6:1-6)

16 Yesu alisafiri akaenda katika mji aliokulia wa Nazareti. Siku ya Sabato alikwenda kwenye sinagogi kama alivyokuwa akifanya. Alisimama ili asome. 17 Akapewa gombo la nabii Isaya. Akalivingirisha kulifungua na akapata mahali palipoandikwa haya:

18 “Roho wa Bwana yu juu yangu,
    amenichagua ili
    niwahubiri maskini habari njema.
Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao
    na kuwaambia wasiyeona
    kuwa wanaweza kuona tena.
Amenituma kuwapa uhuru wale wanaoteswa
19     na kutangaza kuwa wakati wa Bwana
    kuonesha wema wake umefika.”(A)

20 Yesu akalivingirisha gombo akalifunga, akalirudisha kwa msaidizi na kuketi chini. Kwa kuwa kila mtu ndani ya sinagogi alimwangalia kwa makini, 21 Alianza kuzungumza nao. Akasema, “Maandiko haya yametimilika mlipokuwa mnanisikia nikiyasoma!”

22 Kila mtu pale akasema alipenda namna ambavyo Yesu alizungumza. Walishangaa kumsikia akisema maneno haya ya ajabu. Wakaulizana, “Inawezekanaje? Huyu si mwana wa Yusufu?”

23 Yesu akawaambia, “Ninafahamu mtaniambia mithali hii ya zamani: ‘Daktari, jitibu mwenyewe.’ Mnataka kusema ‘Tulisikia mambo yote uliyotenda Kapernaumu. Yatende pia hapa katika mji wako mwenyewe!’” 24 Lakini Yesu akasema, “Ukweli ni huu, nabii hakubaliki katika mji wa kwao.

25-26 Wakati wa Eliya mvua haikunyesha katika Israeli kwa miaka mitatu na nusu. Chakula hakikuwepo mahali popote katika nchi yote. Palikuwa wajane wengi katika Israeli wakati huo. Lakini Eliya hakutumwa kwenda kwa mmoja wa wajane waliokuwa katika Israeli bali kwa mjane aliyekuwa katika mji wa Sarepta, jirani na Sidoni.

27 Na, palikuwa wenye ugonjwa mbaya wa ngozi wengi walioishi katika Israeli wakati wa nabii Elisha, lakini hakuna aliyeponywa isipokuwa Naamani, aliyetoka katika nchi ya Shamu, siyo Israeli.”

28 Watu wote waliposikia hili, walikasirika sana. 29 Wakasimama na kumlazimisha Yesu atoke nje ya mji. Mji wao ulijengwa juu ya kilima. Wakamchukua Yesu mpaka ukingo wa kilima ili wamtupe. 30 Lakini alipita katikati yao na kwenda zake.

Read full chapter