Add parallel Print Page Options

Yesu Ajaribiwa na Shetani

(Mt 4:1-11; Mk 1:12-13)

Akiwa amejaa Roho Mtakatifu, Yesu akarudi kutoka Mto Yordani. Kisha Roho Mtakatifu akamwongoza mpaka nyikani kwa muda wa siku arobaini, alikojaribiwa na Ibilisi. Katika muda wote huo hakula chakula chochote na baadaye akahisi njaa sana.

Ibilisi akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate.”

Yesu akamjibu, “Maandiko yanasema, ‘Watu hawataishi kwa mkate tu.’”(A)

Kisha mwovu akamchukua Yesu na kwa muda mfupi akamwonyesha falme zote za ulimwengu. Mwovu akamwambia, “Nitakufanya uwe mfalme wa sehemu zote hizi. Utakuwa na mamlaka juu yao, na utapata utukufu wote. Yote yametolewa kwangu. Ninaweza kumpa yeyote kadri ninavyopenda. Nitakupa vyote hivi, ikiwa utaniabudu tu.”

Yesu akajibu, “Maandiko yanasema, ‘Ni lazima umwabudu Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.’”(B)

Ndipo Shetani akamwongoza Yesu mpaka Yerusalemu na kumweka mahali palipo juu katika mnara wa Hekalu. Akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, jirushe! 10 Kwani Maandiko yanasema,

‘Mungu atawaamuru
    malaika zake wakulinde.’(C)

11 Pia imeandikwa kuwa,

‘Mikono yao itakudaka,
    ili usijikwae mguu wako kwenye mwamba.’”(D)

12 Yesu akajibu, “Pia, Maandiko yanasema: ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’”(E)

13 Shetani alipomaliza kumjaribu Yesu katika namna zote, alimwacha akaenda zake hadi wakati mwingine.

Yesu Aanza Kazi yake Galilaya

(Mt 4:12-17; Mk 1:14-15)

14 Yesu alirudi Galilaya akiwa na nguvu za Roho Mtakatifu. Habari zake zilisambaa katika eneo lote lililozunguka Galilaya. 15 Alianza kufundisha katika masinagogi na kila mtu alimsifu.

Yesu Aenda Kwenye Mji wa Kwao

(Mt 13:53-58; Mk 6:1-6)

16 Yesu alisafiri akaenda katika mji aliokulia wa Nazareti. Siku ya Sabato alikwenda kwenye sinagogi kama alivyokuwa akifanya. Alisimama ili asome. 17 Akapewa gombo la nabii Isaya. Akalivingirisha kulifungua na akapata mahali palipoandikwa haya:

18 “Roho wa Bwana yu juu yangu,
    amenichagua ili
    niwahubiri maskini habari njema.
Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao
    na kuwaambia wasiyeona
    kuwa wanaweza kuona tena.
Amenituma kuwapa uhuru wale wanaoteswa
19     na kutangaza kuwa wakati wa Bwana
    kuonesha wema wake umefika.”(F)

20 Yesu akalivingirisha gombo akalifunga, akalirudisha kwa msaidizi na kuketi chini. Kwa kuwa kila mtu ndani ya sinagogi alimwangalia kwa makini, 21 Alianza kuzungumza nao. Akasema, “Maandiko haya yametimilika mlipokuwa mnanisikia nikiyasoma!”

22 Kila mtu pale akasema alipenda namna ambavyo Yesu alizungumza. Walishangaa kumsikia akisema maneno haya ya ajabu. Wakaulizana, “Inawezekanaje? Huyu si mwana wa Yusufu?”

23 Yesu akawaambia, “Ninafahamu mtaniambia mithali hii ya zamani: ‘Daktari, jitibu mwenyewe.’ Mnataka kusema ‘Tulisikia mambo yote uliyotenda Kapernaumu. Yatende pia hapa katika mji wako mwenyewe!’” 24 Lakini Yesu akasema, “Ukweli ni huu, nabii hakubaliki katika mji wa kwao.

25-26 Wakati wa Eliya mvua haikunyesha katika Israeli kwa miaka mitatu na nusu. Chakula hakikuwepo mahali popote katika nchi yote. Palikuwa wajane wengi katika Israeli wakati huo. Lakini Eliya hakutumwa kwenda kwa mmoja wa wajane waliokuwa katika Israeli bali kwa mjane aliyekuwa katika mji wa Sarepta, jirani na Sidoni.

27 Na, palikuwa wenye ugonjwa mbaya wa ngozi wengi walioishi katika Israeli wakati wa nabii Elisha, lakini hakuna aliyeponywa isipokuwa Naamani, aliyetoka katika nchi ya Shamu, siyo Israeli.”

28 Watu wote waliposikia hili, walikasirika sana. 29 Wakasimama na kumlazimisha Yesu atoke nje ya mji. Mji wao ulijengwa juu ya kilima. Wakamchukua Yesu mpaka ukingo wa kilima ili wamtupe. 30 Lakini alipita katikati yao na kwenda zake.

Yesu Amweka Huru Mtu Kutoka Pepo Mchafu

(Mk 1:21-28)

31 Yesu akashuka kwenda Kapernaumu, mji uliokuwa Galilaya. Siku ya Sabato aliwafundisha watu. 32 Nao walishangaa sana namna alivyokuwa akifundisha kwa sababu mafundisho yake yalikuwa na mamlaka.

33 Ndani ya sinagogi alikuwepo mtu aliyekuwa na roho chafu, kutoka kwa yule Mwovu, ndani yake. Akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, “Aiii! 34 Unataka nini kwetu Yesu wa Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Ninajua wewe ni nani; Wewe ni Mtakatifu wa Mungu.” 35 Lakini Yesu akamkemea yule pepo na kumwambia, “Nyamaza kimya! Umtoke mtu huyu!” Ndipo pepo akamtupa yule mtu chini mbele ya watu, akamtoka bila kumjeruhi sehemu yoyote ya mwili wake.

36 Watu wakashangaa. Wakasemezana wao kwa wao, “Hii inamaanisha nini? Kwa mamlaka na uwezo anaamuru pepo wachafu na wanatoka!” 37 Hivyo habari kuhusu Yesu zikaenea kila mahali katika eneo lote.

Yesu Amponya Mkwewe Petro

(Mt 8:14-17; Mk 1:29-34)

38 Yesu akatoka katika sinagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni.[a] Mama mkwe wa Simoni alikuwa mgonjwa sana. Alikuwa na homa kali. Nao walimwomba Yesu amsaidie. 39 Yesu alisimama karibu yake na kuiamuru homa kuondoka. Homa ikamwacha, naye akasimama na kuanza kuwahudumia.

Yesu Aponya Wengine Wengi

40 Jua lilipokuchwa, watu wote waliwaleta kwa Yesu jamaa na rafiki zao walioumwa na wenye magonjwa mengi tofauti. Yesu aliweka mikono yake juu ya kila mgonjwa na kuwaponya wote. 41 Pepo nao waliwatoka watu wengi. Mapepo yalipiga kelele yakisema “Wewe ni Mwana wa Mungu.” Lakini Yesu alitoa amri yenye nguvu kwa mapepo yasiseme, kwa sababu yalijua alikuwa ni Masihi.

Yesu Aenda Katika Miji Mingine

(Mk 1:35-39)

42 Siku iliyofuata Yesu alijitenga na kwenda mahali ili awe peke yake. Watu wakawa wakimtafuta. Walipompata, walijaribu kumzuia asiondoke. 43 Lakini akawaambia, “Ni lazima nihubiri Habari Njema kuhusu Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, kwa sababu nilitumwa kufanya hivyo.”

44 Kisha Yesu akahubiri Habari Njema katika masinagogi ya Uyahudi.

Footnotes

  1. 4:38 Simoni Jina jingine la Simoni lilikuwa Petro. Pia katika 5:3,4,5,10.