Book of Common Prayer
Paulo Azungumza na Feliki na Mkewe
24 Baada ya siku chache, Feliki alikuja na mke wake Drusila, aliyekuwa Myahudi. Feliki akaagiza Paulo apelekwe kwake. Alimsikiliza Paulo akiongea kuhusu kumwamini Yesu Kristo. 25 Lakini Feliki aliogopa Paulo alipoongelea kuhusu vitu kama kutenda haki, kuwa na kiasi, na hukumu itakayokuja baadaye. Akasema, “Unaweza kwenda sasa. Nitakapokuwa na muda mwingi, nitakuita.” 26 Lakini Feliki alikuwa na sababu nyingine ya kuzungumza na Paulo. Alitegemea Paulo angempa rushwa, hivyo alimwita Paulo mara nyingi na kuzungumza naye.
27 Lakini baada ya miaka miwili, Porkio Festo akawa gavana. Hivyo Feliki hakuwa gavana tena. Lakini alimwacha Paulo gerezani ili kuwaridhisha Wayahudi.
Paulo Aomba Kumwona Kaisari
25 Festo akawa gavana na siku tatu baadaye akasafiri kwenda Yerusalemu kutoka Kaisaria. 2 Viongozi wa makuhani na viongozi maarufu wa Kiyahudi wakatoa mashitaka dhidi ya Paulo mbele ya Festo. 3 Walimwomba Festo awasaidie. Walitaka amrudishe Paulo Yerusalemu kwa sababu walipanga kumwua akiwa njiani. 4 Lakini Festo alijibu, “Hapana, Paulo ataendelea kuwekwa Kaisaria. Nitaenda huko mimi mwenyewe hivi karibuni, 5 na viongozi wenu wanaweza kufuatana nami. Kama mtu huyu hakika amefanya chochote kibaya, wanaweza kumshitaki huko.”
6 Festo alikaa Yerusalemu kwa siku nane au kumi zaidi kisha alirudi Kaisaria. Siku iliyofuata Festo akawaambia askari wamlete Paulo mbele yake. Festo alikuwa amekaa kwenye kiti cha hukumu. 7 Paulo aliingia kwenye chumba na Wayahudi waliokuja kutoka Yerusalemu walisimama kumzunguka. Walileta mashitaka mengi mazito dhidi yake, lakini hawakuweza kuthibitisha chochote. 8 Paulo alijitetea mwenyewe, akasema, “Sijatenda kitu chochote kibaya kinyume na sheria ya Kiyahudi, kinyume na Hekalu au kinyume na Kaisari.”
9 Lakini Festo alitaka kuwaridhisha Wayahudi. Hivyo alimwuliza Paulo, “Unataka kwenda Yerusalemu ili nikakuhukumu huko kutokana na mashitaka haya?”
10 Paulo akasema, “Kwa sasa nimesimama kwenye kiti cha hukumu cha Kaisari. Hapa ndipo ninatakiwa kuhukumiwa. Sijatenda lolote baya kwa Wayahudi na unafahamu hilo. 11 Ikiwa nilitenda chochote kibaya na sheria inasema ni lazima nife, basi ninakubali kuwa ninapaswa kufa. Siombi kuokolewa kutokana na kifo. Lakini kama mashitaka haya siyo ya kweli, basi hakuna anayeweza kunikabidhi kwa watu hawa. Hapana, Nataka Kaisari aisikilize kesi yangu!”
12 Festo alijadiliana na washauri wake kuhusu hili. Kisha akasema, “Umeomba kumwona Kaisari, basi utakwenda kwa Kaisari!”
Je, Masihi ni Mwana wa Daudi?
(Mt 22:41-46; Lk 20:41-44)
35 Yesu alipokuwa akifundisha katika mabaraza ya Hekalu, alisema, “Inawezekana vipi walimu wa Sheria kusema kwamba Kristo ni mwana wa Daudi? 36 Daudi mwenyewe kwa kupitia Roho Mtakatifu alisema,
‘Bwana Mungu alimwambia Bwana Mfalme wangu:
Keti karibu nami upande wangu wa kuume,
nami nitawaweka adui zako chini ya udhibiti wako.’[a](A)
37 Daudi anamwita Masihi ‘Bwana’. Itakuwaje tena Kristo awe yote Bwana na pia mwana wa Daudi?”
Hapo lilikuwepo kundi kubwa la watu liliokuwa likimsikiliza kwa furaha.
Yesu Anawakosoa Walimu wa Sheria
(Mt 23:6-7; Lk 11:43; 20:45-47)
38 Katika mafundisho yake alisema, “Jihadharini na walimu wa Sheria.” Wao wanapenda kutembea huko na huko katika mavazi yanayopendeza huku wakipenda kusalimiwa masokoni, 39 Hao wanapenda kukaa viti vya mbele katika masinagogi na kupewa sehemu muhimu zaidi za kukaa katika karamu za chakula. 40 Hawa huwadanganya wajane ili wazichukue nyumba zao na wanasali sala ndefu ili kujionesha kwa watu. Watu hawa watapata hukumu iliyo kubwa zaidi.
Mjane Aonesha Jinsi Ulivyo Utoaji wa Kweli
(Lk 21:1-4)
41 Yesu aliketi mahali kuvuka pale palipokuwepo na sanduku la matoleo, alitazama jinsi ambavyo watu walikuwa wakiweka sadaka zao sandukuni. Matajiri wengi waliweka fedha nyingi. 42 Kisha mjane maskini alikuja na kuweka sarafu mbili ndogo za shaba, ambazo zilikuwa na thamani ndogo sana.
43 Yesu aliwaita wanafunzi wake pamoja na kuwaambia, “Nawaambieni ukweli mjane huyu maskini ameweka sarafu mbili tu. Lakini ukweli ni kwamba ametoa zaidi ya matajiri wote wale.” 44 Kwa kuwa wote walitoa kile cha ziada walichokuwa nacho. Lakini yeye katika umasikini wake, aliweka yote aliyokuwa nayo. Na hiyo ilikuwa fedha yote aliyokuwa nayo kutumia wa maisha yake.
© 2017 Bible League International