Book of Common Prayer
23 Kabla ya aliye mwaminifu kuja, sheria ilituweka sisi kama wafungwa. Hatukuwa huru hadi imani hii inayokuja[a] ilipofunuliwa kwetu. 24 Nina maana kuwa sheria ilikuwa ni mlezi aliyetusimamia[b] tu hadi Kristo alipokuja. Baada ya kuja kwake, tungefanyika kuwa wenye haki mbele za Mungu kwa njia ya imani. 25 Sasa kwa sababu imani hii imekuja, hatuhitaji tena kusimamiwa na kulelewa na sheria.
26 Hii ni kwa sababu ninyi nyote ni mali ya Kristo Yesu na ni watoto wa Mungu kwa njia ya imani. 27 Ndiyo, nyote mlibatizwa ili muunganike na Kristo. Hivyo sasa Kristo anawafunika kabisa kama kubadilisha nguo mpya kabisa. 28 Sasa, ndani ya Kristo haijalishi kama wewe u Myahudi au Myunani, mtumwa au huru, mwanaume au mwanamke. Wote mko sawa katika Kristo Yesu. 29 Na kwa vile ninyi ni wa Kristo, hivyo ninyi wazaliwa wa Ibrahamu. Ninyi ndiyo mtakaopokea baraka zote ambazo Mungu alimwahidi Ibrahimu.
4 Ninalolisema ni hili: Wakati mrithi wa vyote alivyomiliki baba yake bado ni mdogo, hana tofauti yo yote na mtumwa. Haijalishi kuwa anamiliki vitu vyote. 2 Wakati wa utoto bado anapaswa kuwatii wale waliochaguliwa kumtunza. Lakini anapoufikia umri ambao baba yake ameuweka, anakuwa huru. 3 Ndivyo ilivyo hata kwetu sisi. Mwanzoni tulikuwa kama watoto, tukiwa watumwa wa mamlaka za uovu[c] zinazoutawala ulimwengu huu wa sasa. 4 Lakini wakati sahihi ulipofika, Mungu akamtuma Mwanaye, aliyezaliwa na mwanamke na akaishi chini ya sheria. 5 Mungu alifanya hivi ili aweze kuwaweka huru wale waliokuwa chini ya sheria. Kusudi la Mungu lilikuwa kutuasili[d] sisi kama watoto wake.
6 Ninyi sasa ni watoto wa Mungu. Na ndiyo sababu Mungu amemtuma Roho wa Mwanaye mioyoni mwetu. Huyo Roho aliye ndani yetu hulia “Aba,[e] yaani Baba.” 7 Sasa ninyi si watumwa kama mwanzo. Ni watoto wa Mungu, na mtapokea kila kitu ambacho Mungu aliwaahidi watoto wake. Hii yote ni kwa sababu ya yale ambayo Mungu amewatendea ninyi.
Yesu ni Nuru ya Ulimwengu
12 Baadaye Yesu akazungumza tena na watu. Akasema, “Mimi ndiye nuru ya ulimwengu. Yeyote atakayenifuata mimi hataishi gizani kamwe. Atakuwa na nuru inayoleta uzima.”
13 Lakini Mafarisayo wakamwambia Yesu, “Unapojishuhudia mwenyewe, unakuwa ni wewe peke yako unayethibitisha kuwa mambo haya ni kweli. Hivyo hatuwezi kuyaamini unayosema.”
14 Yesu akajibu, “Ndiyo, nasema mambo haya juu yangu mwenyewe. Lakini watu wanaweza kuamini ninayosema, kwa sababu mimi najua nilikotoka. Pia najua ninakoenda. Lakini ninyi hamjui mimi ninakotoka wala ninakoenda. 15 Mnanihukumu kama watu wanavyowahukumu wengine. Mimi simhukumu mtu yeyote. 16 Lakini ikiwa ninahukumu, basi hukumu yangu ni ya kweli, kwa sababu ninapohukumu sifanyi hivyo peke yangu. Baba aliyenituma yuko pamoja nami. 17 Sheria yenu inasema kwamba mashahidi wawili wakilisema jambo hilo hilo, basi mnapaswa kukubali wanayosema. 18 Mimi shahidi ninayeshuhudia mambo yangu mwenyewe. Na Baba yangu aliyenituma ndiye shahidi wangu mwingine.”
19 Watu wakamwuliza, “Baba yako yuko wapi?”
Yesu akajibu, “Hamnijui mimi wala Baba yangu hamumjui. Lakini mngenijua mimi, mngemjua Baba pia.”
20 Yesu alisema maneno haya alipokuwa anafundisha katika eneo la Hekalu, karibu na chumba ambamo sadaka za Hekaluni zilitunzwa. Hata hivyo hakuna hata mmoja aliyemkamata, kwa sababu wakati sahihi wa kufanya hivyo ulikuwa bado haujafika.
© 2017 Bible League International