Book of Common Prayer
Imani na Kazi Njema
14 Ndugu zangu, ikiwa mtu atasema kuwa anayo imani lakini hafanyi kitu, imani hiyo haina manufaa yoyote. Imani ya jinsi hiyo haiwezi kumwokoa mtu yeyote. 15 Kama ndugu au dada anahitaji mavazi na anapungukiwa chakula cha kila siku, 16 na ukawaambia, “Mungu awe nanyi! Mkahifadhiwe mahala pa joto na mle vizuri!” Hiyo ina manufaa gani kwao? Usipowapa vitu wanavyovihitaji, maneno yako yanakosa maana! 17 Kwa jinsi hiyo hiyo, imani isipokuwa na matendo itakuwa imekufa.
18 Lakini mtu anaweza kuleta hoja kusema, “Watu wengine wanayo imani, na wengine wanayo matendo mema.” Jibu langu litakuwa, huwezi kunionyesha imani yako pasipo kufanya tendo lolote. Lakini mimi nitakuonesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu. 19 Je, mnaamini kwamba kuna Mungu mmoja tu? Vema! Hata mapepo yanaamini na kutetemeka kwa hofu.
20 Wewe mjinga! Je, unahitaji uthibitisho kwamba imani bila matendo haina manufaa? 21 Je, si baba yetu Ibrahimu alihesabiwa haki na Mungu kwa matendo yake alipomtoa sadaka mwanae Isaka juu ya madhabahu? 22 Kwa hakika unaweza kuiona imani hiyo ilifanya kazi pamoja na matendo yake. Kwa hiyo imani yake ilikamilishwa na matendo yake. 23 Ndipo yakatimizwa yale yaliyo kwenye Maandiko kuwa, “Ibrahimu alimwamini Mungu, na kwa imani hiyo akafanywa kuwa mwenye haki[a] kwa Mungu,”(A) na kwa sababu hiyo akaitwa “Rafiki wa Mungu”.(B) 24 Mnamwona mtu huyo amefanywa kuwa mwenye haki kwa Mungu kwa matendo yake wala siyo kwa imani peke yake.
25 Je, Rahabu[b] yule kahaba si alifanywa kuwa mwenye haki na Mungu kwa matendo aliyofanya, alipowasaidia wale waliokuwa wakipeleleza nchi kwa niaba ya watu wa Mungu. Aliwakaribisha nyumbani mwake na kuwawezesha kutoroka kwa njia nyingine.
26 Hivyo, kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo, imani imekufa ikiwa haina matendo.
Petro Amkana Yesu
(Mt 26:69-75; Lk 22:56-62; Yh 18:15-18,25-27)
66 Wakati Petro alipokuwa bado barazani, mtumishi wa kike wa kuhani mkuu alifika pale. 67 Alipomwona Petro akijipasha moto, alimkazia macho na kumwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu, Mnazareti.”
68 Lakini Petro alisema, “Hii si kweli, mie sifahamu wala kuelewa kile unachokisema.” Baada ya hapo Petro alitoka na kwenda barazani na hapo hapo jogoo akawika.
69 Yule mtumishi wa kike alipomwona alirudia tena kuwaeleza wale waliokuwa wamesimama pale, “Mtu huyu ni mmoja wao!” 70 Kwa mara nyingine tena Petro alikataa.
Baada ya muda mfupi wale waliokuwa wamesimama pale wakarudia tena kumwambia Petro, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa sababu wewe pia ni Mgalilaya.”
71 Petro akaanza kutoa maneno makali na kusema, “Naapa kwa Mungu, simjui mtu huyu mnayemzungumzia!”
72 Mara jogoo akawika kwa mara ya pili, na Petro akakumbuka lile neno la Yesu alilomwambia: “Kabla kogoo hajawika mara ya pili utanikana mara tatu.” Naye akavunjika moyo na kuanza kulia.
© 2017 Bible League International