Book of Common Prayer
Paulo Akiwa Korintho
18 Baadaye, Paulo aliondoka Athene na kwenda katika mji wa Korintho. 2 Akiwa huko alikutana na Myahudi aliyeitwa Akila, aliyezaliwa katika jimbo la Ponto. Lakini yeye na mke wake aliyeitwa Prisila, walikuwa tu ndiyo wamehamia Korintho kutoka Italia. Waliondoka Italia kwa sababu Kaisari Klaudio alikuwa ametoa amri Wayahudi wote waondoke Rumi. Paulo alikwenda kuwatembelea Akila na Prisila. 3 Walikuwa watengenezaji wa mahema,[a] kama alivyokuwa Paulo, hivyo alikaa na kufanya kazi pamoja nao.
4 Kila siku ya Sabato Paulo alikwenda kwenye sinagogi na kuzungumza na Wayahudi na Wayunani, akijaribu kuwashawishi wamwamini Yesu. 5 Lakini baada ya Sila na Timotheo kufika kutoka Makedonia, Paulo alitumia muda wake wote kuuhubiri ujumbe wa Mungu kwa Wayahudi, akiwaeleza kuwa Yesu ndiye Masihi. 6 Lakini walimpinga Paulo na wakaanza kumtukana. Hivyo Paulo akakung'uta mavumbi kutoka kwenye nguo zake.[b] Akawaambia, “Msipookolewa, itakuwa makosa yenu ninyi wenyewe! Nimefanya yote ninayoweza kufanya. Baada ya hili nitawaendea watu wasio Wayahudi tu.”
7 Paulo aliondoka katika sinagogi na kuhamia nyumbani kwa Tito Yusto, mtu aliyekuwa anamwabudu Mungu wa Kweli, nyumba yake ilikuwa jirani na sinagogi. 8 Krispo aliyekuwa kiongozi wa sinagogi lile, pamoja na watu wote waliokuwa wanaishi nyumbani mwake walimwamini Bwana Yesu. Watu wengi katika mji wa Korintho walimsikiliza Paulo, wakaamini na wakabatizwa.
9 Wakati wa usiku, Paulo aliona maono. Bwana alimwambia, “Usiogope, na usiache kuzungumza na watu. 10 Niko pamoja nawe, na hakuna atakayeweza kukudhuru. Kuna watu wangu wengi katika mji huu.” 11 Paulo alikaa pale kwa mwaka mmoja na nusu akiwafundisha watu ujumbe wa Mungu.
Baadhi ya Watu Wawa na Mashaka na Mamlaka ya Yesu
(Mt 16:1-4; Lk 11:16,29)
11 Mafarisayo wakamwendea Yesu na kuanza kubishana naye. Ili kumjaribu wakamwomba ishara kutoka mbinguni. 12 Yesu alihema kwa nguvu na kusema, “Kwa nini kizazi kinataka ishara? Ninawaambia ukweli: hakuna ishara itakayooneshwa kwa kizazi hiki.” 13 Kisha Yesu akawaacha, akapanda tena katika mashua, na akaondoka kwenda upande wa pili wa ziwa.
Wafuasi Washindwa Kumwelewa Yesu
(Mt 16:5-12)
14 Wakati huo huo wanafunzi walikuwa wamesahau kuleta mikate yo yote, na hawakuwa na kitu kingine isipokuwa mkate mmoja. 15 Yesu akawaonya, akasema, “Mwe mwangalifu! Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na ile ya Herode.”
16 Nao wakaanza kujadiliana haya miongoni mwao: “Labda alisema hivi kwa sababu hatukuwa na mkate wowote.”
17 Akijua walichokuwa wakikisema, akawaambia, “Kwa nini mnajadiliana juu ya kutopata mkate? Je! Bado hamwoni na kuelewa? Je! Mmezifunga akili zenu. 18 Mnayo macho; Je! Hamwoni? Mnayo masikio; Je! Hamwezi kusikia? Mnakumbuka? 19 Nilipomega na kugawa mikate mitano kwa watu 5,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa masalia ya mikate?”
Wakasema “Kumi na viwili”.
20 “Nilipomega na kugawa mikate saba kwa watu 4,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa masalia ya mikate?”
Wakasema “Saba”.
21 Kisha akawaambia, “Bado hamwelewi?”
© 2017 Bible League International