Book of Common Prayer
Paulo Apelekwa Kaisaria
23 Ndipo Kamanda akawaita maofisa wawili wa jeshi. Akawaambia, “Ninataka baadhi ya watu kwenda Kaisaria. Andaeni askari mia mbili. Pia andaeni askari sabini waendao kwa farasi na mia mbili wa kubeba mikuki. Iweni tayari kuondoka saa tatu usiku. 24 Andaeni baadhi ya farasi kwa ajili ya Paulo kuendesha ili aweze kupelekwa kwa Gavana Feliki salama.” 25 Kamanda aliandika barua kuhusu Paulo. Hivi ndivyo alivyosema:
26 Kutoka kwa Klaudio Lisiasi.
Kwenda kwa Mheshimiwa Gavana Feliki.
Salamu:
27 Baadhi ya Wayahudi walimkamata mtu huyu na walikuwa karibu ya kumwua. Lakini nilipogundua kuwa ni raia wa Rumi, nilikwenda pamoja na askari wangu tukamwokoa. 28 Nilitaka kufahamu kwa nini walikuwa wanamshitaki. Hivyo nikampeleka kwenye mkutano wa baraza lao. 29 Hivi ndivyo nilivyoona: Wayahudi walisema mtu huyu alifanya mambo mabaya. Lakini mashitaka haya yalihusu sheria zao za Kiyahudi, na hakukuwa kosa lolote linaloweza kusababisha kufungwa au kifo. 30 Nimeambiwa kuwa baadhi ya Wayahudi walikuwa wanafanya mpango wa kumwua. Hivyo nimeamua kumleta kwako. Pia nimewaambia Wayahudi hao wakwambie walichonacho dhidi yake.
31 Askari walifanya kile walichoambiwa. Walimchukua Paulo na kumpeleka kwenye mji wa Antipatri usiku ule. 32 Siku iliyofuata askari wa farasi walikwenda na Paulo mpaka Kaisaria, lakini askari wengine na wale wa mikuki walirudi kwenye jengo la jeshi mjini Yerusalemu. 33 Askari wa farasi waliingia Kaisaria, wakampa barua Gavana Feliki, kisha wakamkabidhi Paulo kwake.
34 Gavana akaisoma barua na kumwuliza Paulo, “Unatoka jimbo gani?” Gavana alitambua kuwa Paulo alikuwa anatoka Kilikia. 35 Gavana akasema, “Nitakusikiliza Wayahudi wanaokushitaki watakapokuja hapa pia.” Kisha gavana akaamuru Paulo awekwe kwenye jumba la kifalme. (Jengo hili lilijengwa na Herode.)
Yesu Ajibu Swali Lenye Mtego
(Mt 22:15-22; Lk 20:20-26)
13 Viongozi wa Kidini wakamtumia baadhi ya Mafarisayo na Maherode ili kumkamata kama akisema chochote kimakosa. 14 Wale waliotumwa walifika na kumwambia, “Mwalimu tunajua, kwamba wewe ni mkweli, na tena hujali yale watu wanayoyafikiri kuhusu wewe, kwa sababu wewe hubabaishwi na wadhifa wa mtu. Lakini unafundisha ukweli wa njia ya Mungu. Tuambie ni haki kulipa kodi kwa Kaisari ama la? Je, tulipe au tusilipe?”
15 Lakini Yesu aliutambua unafiki wao na akawaambia, “Kwa nini mnanijaribu hivi? Mniletee moja ya sarafu ya fedha mnazotumia ili niweze kuiangalia.” 16 Hivyo wakamletea sarafu, naye akawauliza, “Je, sura hii na jina hili ni la nani?” Nao wakamwambia, “Ya Kaisari.”
17 Ndipo Yesu alipowaambia, “Mpeni Kaisari vilivyo vyake, na Mungu mpeni vilivyo vyake.” Wakastaajabu sana kwa hayo.
Baadhi ya Masadukayo Wajaribu Kumtega Yesu
(Mt 22:23-33; Lk 20:27-40)
18 Kisha Masadukayo wakamjia. (Hawa ni wale wanaosema hakuna ufufuo wa wafu.) Wakamwuliza, 19 “Mwalimu, Musa alituandikia kwamba ikiwa kaka wa mtu atafariki na kumwacha mke asiye na watoto, Basi yule kaka lazima aoe mke yule wa nduguye na kuzaa naye watoto kwa ajili ya kaka yake aliyefariki. 20 Palikuwepo na ndugu wa kiume saba. Wa kwanza alioa mke, naye alikufa bila kuacha mtoto yeyote. 21 Wa pili naye akamwoa yule mke wa nduguye wa kwanza aliyeachwa naye akafa bila kuacha watoto wowote. Ndugu wa tatu pia alifanya vivyo hivyo. 22 Ndugu wote wale saba walimwoa yule mwanamke na wote hawakupata watoto. Mwisho wa yote, yule mwanamke pia akafariki, 23 Katika ufufuo, pale wafu watakapofufuka toka katika kifo, Je, yeye atakuwa mke wa nani? Kwani wote saba walikuwa naye kama mke wao.”
24 Yesu akawaambia, “Hakika hii ndiyo sababu mmekosa sana: Hamyajui Maandiko wala uwezo wa Mungu. 25 Kwa kuwa wafu wanapofufuka toka katika wafu, hawaoi wala kuolewa. Badala yake wanakuwa kama malaika walioko Mbinguni. 26 Lakini kuhusu kufufuka kwa wafu, Je, hamjasoma katika kitabu cha Musa katika sura ile ya kichaka kinachoungua? Pale ndipo Mungu alipomwambia Musa, ‘Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo.’(A) 27 Yeye si Mungu wa waliokufa, bali wa wale wanaoishi. Hivyo ninyi mmekosa sana.”
© 2017 Bible League International