Book of Common Prayer
27 Usiku wa kumi na nne tulikuwa bado tunasukumwa na upepo katika bahari ya Adriatiki. Mabaharia wakadhani tulikuwa karibu na nchi kavu. 28 Wakatupa kamba iliyofungwa kitu kizito kwenye ncha yake. Wakakuta kwamba kina cha maji ni futi mia moja na ishirini.[a] Wakaendelea mbele kidogo na kutupa kamba tena. Kina kilikuwa futi tisini.[b] 29 Mabaharia waliogopa kwa kudhani kwamba tungegonga miamba, hivyo wakatupa nanga nne kwenye maji. Kisha wakaomba mchana ufike. 30 Baadhi ya mabaharia walitaka kuiacha meli, waliishusha majini mtumbwi wa kuokolea. Walitaka watu wengine wadhani kuwa walikuwa wanatupa nanga upande wa mbele wa meli. 31 Lakini Paulo alimwambia ofisa wa jeshi na askari wengine, “Iwapo watu hawa hawatakaa ndani ya meli, mtapoteza matumaini yote ya kupona.” 32 Hivyo askari wakakata kamba na kuuacha mtumbwi uanguke majini.
33 Kabla ya kupambazuka Paulo alianza kuwashawishi watu wote kula. Alisema, “Kwa wiki mbili mmekuwa mnasubiri na kuangalia, hamjala kwa siku kumi na nne. 34 Sasa ninawasihi mle chakula, mnakihitaji ili kuishi. Hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza hata unywele mmoja kutoka kwenye kichwa chake.” 35 Baada ya kusema hili, Paulo alichukua baadhi ya mikate akamshukuru Mungu kwa ajili ya mikate hiyo mbele yao wote. Akakata kipande na kuanza kula. 36 Watu wote wakafarijika na kuanza kula pia. 37 (Walikuwemo watu mia mbili sabini na sita ndani ya meli.) 38 Tulikula kila tulichohitaji. Kisha tukaanza kumwaga nafaka baharini ili meli iwe nyepesi.
Meli Yaharibiwa
39 Mchana ulipofika, mabaharia waliiona nchi kavu, lakini hawakupafahamu mahali pale. Waliona ghuba yenye ufukwe na walitaka kuipeleka meli ufukweni ikiwa wangeweza. 40 Hivyo walikata kamba kwenye nanga na kuziacha nanga ndani ya bahari. Wakati huo huo walifungua kamba zilizokuwa zinaushikilia usukani. Kisha wakanyanyua tanga la mbele na kutweka tanga kuelekea ufukweni. 41 Lakini meli uligonga mwamba wa michanga. Sehemu ya mbele ya meli ilikwama pale na haikuweza kutoka. Kisha mawimbi makubwa yakaanza kuvunja sehemu ya nyuma ya meli vipande vipande.
42 Askari waliamua kuwaua wafungwa ili asiwepo mfungwa hata mmoja atakayeogelea na kutoroka. 43 Lakini Yulio, ofisa wa jeshi alitaka Paulo asiuawe. Hivyo hakuwaruhusu askari kuwaua wafunga. Aliwaambia watu wanaoweza kuogelea, waruke majini kwenda nchi kavu. 44 Wengine walitumia mbao au vipande vya meli. Hivi ndivyo ambavyo watu wote walifika nchi kavu wakiwa salama.
Karamu ya Pasaka
(Mt 26:17-25; Lk 22:7-14,21-23; Yh 13:21-30)
12 Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, ambapo kila mara mwana kondoo alitolewa sadaka kwa ajili ya Pasaka. Wanafunzi wa Yesu wakamwendea na kumwuliza, “Ni wapi unapotaka tuende kukuandalia ili uweze kuila Karamu ya Pasaka?”
13 Hivyo Yesu aliwatuma wanafunzi wake wawili, naye akawaeleza, “ingieni mjini, na mtakutana na mtu mmoja aliyebeba gudulia la maji. Mfuateni, 14 popote pale atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba ile, ‘mwalimu anasema, utuonyeshe chumba ambacho yeye na wanafunzi wake wanaweza kuila Karamu ya Pasaka.’ 15 Naye atawaonesha chumba kikubwa ghorofani, klichoandaliwa tayari kwa ajili yetu. Basi mtuandalie chakula pale.”
16 Wanafunzi wa Yesu waliondoka na kuelekea mjini. Huko walikuta kila kitu kama vile Yesu alivyowaeleza Hivyo, waliandaa mlo wa Pasaka.
17 Wakati wa jioni Yesu alienda pamoja na wanafunzi wake kumi na mbili katika nyumba ile. 18 Wote walipokuwa wameketi mezani wakila, Yesu akasema, “Mniamini ninapowambia kwamba mmoja wenu, yule anayekula nami sasa atanitoa kwa maadui zangu.”
19 Wanafunzi walihuzunika sana kusikia jambo hili. Kila mmoja akamwambia Yesu, “Hakika siyo mimi?”
20 Akawaambia, “Ni mmoja wa wale kumi na mbili; na ni yule atakayechovya mkate katika bakuli pamoja nami. 21 Mwana wa Adamu atakiendea kifo chake kama ilivyoandikwa juu yake. Lakini itakuwa ya kutisha namna gani kwa mtu yule ambaye kupitia yeye Mwana wa Adamu anasalitiwa. Itakuwa bora mtu huyu asingelikuwa amezaliwa.”
Chakula cha Bwana
(Mt 26:26-30; Lk 22:15-20; 1 Kor 11:23-25)
22 Na walipokuwa wakila Yesu aliuchukua mkate, akamshukuru Mungu kwa huo. Akamega vipande, akawapa wanafunzi wake, na kusema, “Chukueni na mle mkate huu. Ni mwili wangu.”
23 Kisha akakichukua kikombe chenye divai, akamshukuru Mungu kwa hicho, akawapa. Wote wakanywa toka kile kikombe. 24 Kisha akasema, “Kinywaji hiki ni damu yangu ambayo kwayo Mungu anafanya agano na watu wake. Damu yangu inamwagika kwa manufaa ya watu wengi. 25 Ninawaambia kweli sitakunywa diva tena mpaka siku ile nitakapokunywa divai mpya katika Ufalme wa Mungu.”
26 Na wao wakaimba mwimbo wa sifa na kutoka na kuelekea kwenye Mlima wa Miti ya Mizeituni.
© 2017 Bible League International