Book of Common Prayer
6 Maandiko yanasema kitu hicho hicho kuhusu Ibrahimu. “Ibrahimu alimwamini Mungu, na Mungu akaikubali imani yake na akamhesabia haki.”(A) 7 Hivyo mnapaswa kuelewa kuwa watoto sahihi wa Ibrahimu ni wale walio na imani. 8 Maandiko yalieleza ambacho kingetokea katika siku zijazo. Maandiko haya yalisema kwamba Mungu angewafanya wasio Wayahudi kuwa wenye haki kwa njia ya imani. Mungu alizisema Habari Njema hizi kwa Ibrahimu kabla haijatokea. Mungu alimwambia Ibrahimu, “Kwa kukubariki wewe, nitawabariki watu wote duniani.”(B) 9 Kwa hiyo, wale wote wanaoweka imani yao kwa Mungu ndiyo wanaobarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwaminifu.
10 Lakini watu wale wanaodhani kuwa kutii sheria ndicho kitu muhimu sana daima hukaa chini ya tishio la laana. Kama vile Maandiko yanavyosema, “Amelaaniwa mtu yeyote atakayeacha kuzishika na kuzitii sheria hizi zote.”(C) 11 Hivyo ni dhahiri kuwa hakuna anayeweza kuhesabiwa haki mbele za Mungu kwa kuifuata sheria. Maandiko yanasema, “Mwenye haki mbele za Mungu ataishi kwa imani.”(D)
12 Sheria haitegemei imani. Hapana, inasema kuwa njia pekee ambayo mtu anaweza kupata uzima kwa njia ya sheria ni kwa kutii amri zake.[a] 13 Sheria inasema kuwa sisi Wayahudi tuko chini ya laana kwa kutokuitii daima. Lakini Kristo alituweka huru kutoka katika laana hiyo. Alikubali kulaaniwa na sheria ili atuokoe. Maandiko yanasema, “Yeyote anayening'inizwa mtini[b] yuko chini ya laana.”(E) 14 Kwa sababu ya yale aliyoyafanya Kristo Yesu, baraka ambazo Mungu alimwahidi Ibrahimu zilitolewa pia kwa wasio Wayahudi. Kristo alikufa ili kwamba kwa kumwamini sisi sote, Wayahudi na wasio Wayahudi, tuweze kumpokea Roho ambaye Mungu aliahidi.
30 Siwezi kufanya jambo lolote peke yangu. Ninahukumu kama vile ninavyoagizwa. Na hukumu yangu ni halali, kwa sababu sitafuti kujifurahisha mwenyewe. Bali ninataka tu kumfurahisha yeye aliyenituma.”
Yesu Asema Zaidi Na Viongozi wa Kiyahudi
31 “Endapo nitawaeleza watu mambo yangu mwenyewe, watu hawatakuwa na uhakika kama yale ninayosema ni kweli. 32 Lakini yupo mwingine anayewaeleza watu mambo yangu, nami nafahamu kuwa yale anayoyasema juu yangu ni kweli.
33 Mliwatuma watu kwa Yohana, naye akawaambia yaliyo kweli. 34 Hivyo sihitaji mtu yeyote wa kuwaeleza watu juu yangu, isipokuwa nawakumbusha ninyi yale aliyoyasema Yohana ili muweze kuokolewa. 35 Yohana alikuwa kama taa iliyowaka na kutoa mwanga, nanyi mlipata raha mkiufurahia mwanga wake japo kwa muda.
36 Hata hivyo uthibitisho nilionao mwenyewe juu yangu ni mkuu kuliko chochote alichokisema Yohana. Mambo ninayofanya ndiyo yanayonithibitisha. Haya ndiyo Baba aliyonipa kufanya. Nayo yanadhihirisha kuwa Baba alinituma. 37 Na Baba aliyenituma yeye mwenyewe ametoa uthibitisho juu yangu. Lakini hamjawahi kabisa kuisikia sauti yake. Hamjawahi pia kuuona uso wake jinsi ulivyo. 38 Mafundisho ya Baba hayakai ndani yenu, kwa sababu hamumwamini yule aliyetumwa na Baba. 39 Mnajifunza Maandiko kwa makini. Nanyi mnafikiri kuwa yanawapa uzima wa milele. Maandiko haya haya yanaeleza habari zangu! 40 Lakini mnakataa kuja kwangu kuupata huo uzima.
41 Sitaki kutukuzwa nanyi ama na mwanadamu mwingine yeyote. 42 Hata hivyo ninawajua ninyi, na ninajua kwamba hamna upendo kwa Mungu. 43 Nimekuja kutoka kwa Baba yangu nami ni msemaji wake, lakini hamnikubali. Lakini watu wengine wakija wakijisemea mambo yao tu, mnawakubali! 44 Ninyi mnapenda kupeana sifa kila mmoja kwa mwenzake. Lakini hamjaribu kupata sifa zinazotoka kwa Mungu wa pekee. Hivyo mtawezaje kuamini? 45 Msifikiri kwamba mimi ndiye nitakayesimama mbele za Baba na kuwashtaki. Musa ndiye atakayewashtaki. Na ndiye mliyetegemea angeliwaokoa. 46 Kama kwa hakika mlimwamini Musa, nami mlipaswa kuniamini, kwa sababu yeye aliandika habari juu yangu. 47 Lakini hamuyaamini aliyoyaandika, hivyo hamuwezi kuyaamini ninayoyasema.”
© 2017 Bible League International