Book of Common Prayer
9 Tulikuwa tumepoteza muda mwingi, na ilikuwa hatari kutweka tanga, kwa sababu tayari ilikuwa baada ya siku ya Kiyahudi ya kufunga.[a] Hivyo Paulo aliwaonya akasema, 10 “Ndugu zangu, ninaona kuwa kutakuwa shida nyingi katika safari hii. Meli, kila kitu ndani yake na pia hata maisha yetu yanaweza kupotea!” 11 Lakini nahodha na mmiliki wa meli hawakukubaliana na Paulo. Hivyo ofisa wa jeshi alikubali walichokisema badala ya kumwamini Paulo. 12 Pia, bandari ile haikuwa mahali pazuri kwa meli kukaa majira ya baridi, hivyo watu karibu wote wakaamua kwamba ni lazima tuondoke pale. Walitegemea kuwa tungeweza kufika Foeniki, ambako meli ingekaa majira ya baridi. Foeniki ulikuwa mji katika kisiwa cha Krete. Ulikuwa na bandari iliyotazama Kusini-Magharibi na Kaskazini-Magharibi.
Dhoruba
13 Ndipo upepo mzuri ukaanza kuvuma kutoka kusini. Watu ndani ya meli wakafikiri, “Huu ndio upepo tulioutaka, na sasa tumeupata!” Hivyo wakavuta nanga. Tulitweka tanga tukasafiri karibu na kisiwa cha Krete. 14 Lakini upepo wenye nguvu unaoitwa “Kaskazini-Mashariki” ulikuja kwa kukikatisha kisiwa. 15 Upepo huu uliichukua meli na kuisukumia mbali. Meli haikuweza kwenda kinyume na upepo, hivyo tulisimama tukijaribu kuuacha upepo utusukume.
16 Tulikwenda upande wa chini wa kisiwa kidogo kilichoitwa Kauda. Kisiwa kikatukinga dhidi ya upepo, tulichukua mtumbwi wa kuokolea watu, lakini ilikuwa vigumu sana kufanya hivyo. 17 Baada ya watu kuleta mtumbwi wa kuokolea, wakaifunga meli kamba kuizungushia ili iendelee kushikamana isipasuke. Waliogopa kwamba meli ingekwama kwenye mchanga wa pwani ya Sirti.[b] Hivyo walishusha tanga na kuiacha meli ichukuliwe na upepo.
18 Siku iliyofuata upepo ulivuma kinyume nasi kwa nguvu kiasi kwamba watu walitupa baadhi ya vitu kutoka katika shehena ya meli.[c] 19 Siku moja baadaye wakatupa vifaa vya meli. 20 Kwa siku nyingi hatukuweza kuliona jua au nyota. Dhoruba ilikuwa mbaya sana. Tulipoteza matumaini yote ya kuendelea kuwa hai, tulidhani tutakufa.
21 Watu hawakula kwa muda mrefu. Ndipo siku moja Paulo akasimama mbele yao na kusema, “Ndugu zangu, niliwaambia tusiondoke Krete. Mngenisikiliza msingepata tatizo hili na hasara hii. 22 Lakini sasa ninawaambia iweni na furaha. Hakuna hata mmoja wenu atakayekufa, lakini meli itapotea. 23 Usiku uliopita malaika kutoka kwa Mungu ninayemwabudu na ambaye mimi ni wake. 24 Aliniambia, ‘Paulo, usiogope! Ni lazima utasimama mbele ya Kaisari. Mungu amekupa ahadi hii: Ataokoa maisha ya wote wanaosafiri pamoja nawe.’ 25 Hivyo ndugu, msihofu kitu chochote. Ninamwamini Mungu, na nina uhakika kila kitu kitatokea kama malaika wake alivyoniambia. 26 Lakini tutajigonga kwenye kisiwa.”
Mpango wa Kumwua Yesu
(Mt 26:1-5; Lk 22:1-2; Yh 11:45-53)
14 Ilikuwa yapata siku mbili kabla ya Sikukuu ya Pasaka na Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Wakuu wa makuhani na walimu wa Sheria walikuwa wakitafuta njia, kwa ujanja fulani, ya kumkamata na kumuua Yesu. 2 Kwani walikuwa wakisema “tusifanye hivi wakati wa sherehe, ama sivyo watu watafanya fujo.”
Mwanamke Ampa Yesu Heshima
(Mt 26:6-13; Yh 12:1-8)
3 Yesu alikuwa Bethania, katika nyumba ya Simoni mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi. Wakati ameketi mezani mwanamke mmoja alimwijia. Naye alikuwa na gudulia la mawe lililojaa manukato ya bei ghali yaliyotengenezwa kwa nardo safi. Mwanamke huyo alilifungua gudulia lile kwa kulivunja na kumwagia Yesu manukato kichwani mwake.
4 Baadhi ya watu waliokuwa pale walikasirika na kulalamika miongoni mwao, “Kwa nini kuwepo na ufujaji wa manukato namna hii? 5 Gharama yake ni sawa na mshahara wa mwaka[a] mzima. Manukato haya yangeweza kuuzwa na fedha hiyo kupewa walio maskini.” Kisha wakamkosoa yule mwanamke kwa hasira kwa jambo alilolifanya.
6 “Lakini Yesu alisema mwacheni peke yake. Kwa nini mnamsumbua? Yeye amenifanyia kitendo chema. 7 Kwani siku zote mnao maskini pamoja nanyi na mnaweza kuwasaidia wakati wowote mnaopenda. Lakini hamtakuwa pamoja nami siku zote. 8 Yeye amefanya kile alichokiweza kufanya. Ameumwagia manukato mwili wangu kabla ya wakati kuuandaa kwa ajili ya maziko. 9 Ninawaambia kweli: Popote injili itakapohubiriwa ulimwenguni, kile alichokifanya kitasimuliwa kwa kumkumbuka.”
Yuda Akubali Kuwasaidia Adui wa Yesu
(Mt 26:14-16; Lk 22:3-6)
10 Kisha Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na mbili, aliwaendea viongozi wa makuhani ili kumsaliti Yesu kwao. 11 Nao walifurahi kusikia hivyo, na wakaahidi kumpa fedha. Kwa hiyo Yuda akaanza kutafuta wakati unaofaa wa kumsaliti.
© 2017 Bible League International