Book of Common Prayer
Huduma ya Paulo kwa Wasio Wayahudi
3 Hivyo, mimi Paulo ni mfungwa kwa sababu ninamtumikia Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi msio Wayahudi. 2 Mnajua hakika ya kuwa Mungu alinipa kazi hii kupitia neema yake ili niwasaidie. 3 Mungu alinionyesha na nikaweza kuujua mpango wake wa siri. Nimekwisha kuandika kiasi fulani juu ya hili. 4 Na ikiwa mtasoma nilichowaandikia, mtajua kuwa ninaielewa siri ya kweli kuhusu Kristo. 5 Watu walioishi zamani hawakuambiwa siri hiyo. Lakini sasa, kupitia Roho, Mungu amewawezesha mitume na manabii wake watakatifu kuijua siri hiyo. 6 Na siri hiyo ni hii: Kwa kuikubali Habari Njema, wale wasio Wayahudi watashiriki pamoja na Wayahudi katika baraka alizonazo Mungu kwa ajili ya watu wake. Wao ni sehemu ya mwili mmoja, na wanashiriki manufaa ya ahadi ambayo Mungu aliitimiza kupitia Kristo Yesu.
7 Kwa kipawa cha neema ya Mungu, nilifanywa mtumishi wa kuihubiri Habari Njema. Alinipa neema hiyo kwa nguvu zake. 8 Mimi nisiye na umuhimu zaidi miongoni mwa watu wa Mungu. Lakini alinipa kipawa hiki cha kuwahubiri wasio Wayahudi Habari Njema kuhusu utajiri alionao Kristo. Utajiri huu ni mkuu na si rahisi kuuelewa kikamilifu. 9 Pia Mungu alinipa kazi ya kuwaambia watu kuhusu mpango wa siri yake ya kweli. Aliificha siri hii ya kweli ndani yake tangu mwanzo wa nyakati. Ndiye aliyeumba kila kitu. 10 Lengo lake lilikuwa kwamba watawala wote na mamlaka zote zilizo mbinguni zijue njia nyingi anazotumia kuionesha hekima yake. Watalijua hili kwa sababu ya kanisa. 11 Hii inaendana na mpango aliokuwa nao Mungu tangu mwanzo wa nyakati. Alitekeleza mpango wake kupitia Kristo Yesu Bwana wetu. 12 Kwa kuwa tu wake Kristo tunakuja mbele za Mungu tukiwa huru bila woga. Tunaweza kufanya hivi kwa sababu ya uaminifu wake Kristo.[a] 13 Hivyo ninawaomba msikate tamaa kutokana na yale yanayonipata. Mateso yangu ni faida kwenu, na pia ni kwa ajili ya heshima na utukufu wenu.
Yesu Amponya Mtumishi wa Afisa wa Jeshi
(Lk 7:1-10; Yh 4:43-54)
5 Yesu alikwenda Kapernaumu. Alipoingia mjini, afisa wa jeshi alimjia na kumwomba msaada. 6 Akasema, “Bwana, mtumishi wangu ni mgonjwa sana nyumbani na amelala kitandani. Hawezi hata kutingishika na ana maumivu makali sana.”
7 Yesu akamwambia yule afisa, “Nitakwenda nimponye.”
8 Yule afisa akajibu, “Bwana, mimi si mwema kiasi cha wewe kuingia katika nyumba yangu. Toa amri tu, na mtumishi wangu atapona. 9 Ninajua hii, kwa kuwa ninaelewa mamlaka. Kuna watu wenye mamlaka juu yangu, na nina askari walio chini ya mamlaka yangu. Nikimwambia askari mmoja ‘nenda’, huenda. Na nikimwambia mwingine ‘njoo’, huja. Pia nikimwambia mtumwa wangu ‘fanya hiki’, hunitii.”
10 Yesu aliposikia maneno hayo alishangaa. Akawaambia wale waliokuwa wakifuatana naye, “Ukweli ni kuwa, mtu huyu ana imani kuliko mtu yeyote niliyewahi kumwona katika Israeli. 11 Watu wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi na kula pamoja na Ibrahimu, Isaka, na Yakobo katika ufalme wa Mungu. 12 Na wale wanaopaswa kuwa katika ufalme watatupwa nje gizani. Na huko watalia na kusaga meno yao kwa sababu ya maumivu.”
13 Kisha Yesu akamwambia yule afisa, “Rudi nyumbani kwako. Mtumishi wako atapona kama unavyoamini.” Mtumishi wa afisa huyo akapona wakati ule ule.
Yesu Awaponya Watu Wengi
(Mk 1:29-34; Lk 4:38-41)
14 Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, alimkuta mama mkwe wake Petro amelala kitandani akiwa na homa. 15 Akamgusa mkono wake na homa ikamwacha, kisha akasimama na kuanza kumhudumia.
16 Ilipofika jioni, watu wengi waliokaliwa na mashetani waliletwa kwa Yesu. Naye aliyaamuru mashetani hayo kuwaacha watu. Na aliowaponya wagonjwa wote. 17 Hii ilitokea ili kutimiza maneno yaliyosemwa na nabii Isaya aliposema:
“Aliyaondoa magonjwa yetu
na kuyabeba madhaifu yetu.”(A)
© 2017 Bible League International