Book of Common Prayer
5 Ninyi ni watoto wa Mungu wapendwao, hivyo jitahidini kuwa kama yeye. 2 Ishini maisha ya upendo. Wapendeni wengine kama Kristo alivyotupenda sisi. Alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu na kuwa sadaka ya harufu ya manukato mazuri na dhabihu kwa Mungu.
3 Lakini hakupaswi kuwepo dhambi ya zinaa kati yenu. Hakupaswi kuwepo aina yoyote ya uasherati au matamanio ya zinaa, kwa sababu mambo kama hayo hayastahili kwa watakatifu wa Mungu. 4 Vivyo hivyo, pasiwepo na mazungumzo maovu miongoni mwenu. Msizungumze mambo ya kipuuzi au ya uchafu. Hayo siyo kwa ajili yenu. Bali mnatakiwa kutoa shukrani kwa Mungu. 5 Mnaweza kuwa na uhakika wa hili: Hakuna atakayepata sehemu katika ufalme wa Kristo na wa Mungu kama mtu huyo atakuwa anafanya dhambi ya uzinzi, au akitenda mambo maovu, au kama atakuwa mtu wa kutamani vitu zaidi na zaidi. Mtu mwenye choyo kama huyo atakuwa anamtumikia mungu wa uongo.
6 Msimruhusu mtu yeyote awadanganye kwa maneno yasiyo ya kweli. Mungu huwakasirikia sana watu wasipomtii kama hivyo. 7 Hivyo msiwe na jambo lolote pamoja nao. 8 Hapo zamani mlijaa giza, lakini sasa mmejaa nuru katika Bwana. Hivyo ishini kama watoto wa nuru. 9 Nuru hii huleta kila aina ya wema, maisha ya haki, na kweli. 10 Jaribuni kutafuta yale yanayompendeza Bwana. 11 Msishiriki katika mambo yanayotendwa na watu wa giza, yasiyosababisha jambo lolote zuri. Badala yake, mwambieni kila mtu jinsi mambo hayo yasivyokuwa sahihi. 12 Hakika, ni aibu hata kuyazungumzia mambo haya wanayoyatenda sirini. 13 Lakini nuru inaonesha wazi jinsi mambo hayo yasivyokuwa sahihi. 14 Ndiyo, kila kitu kinawekwa wazi na nuru. Ndiyo maana tunasema,
“Amka, wewe unayelala!
Fufuka kutoka kwa wafu,
na Kristo atakuangazia nuru yake.”
15 Hivyo, muwe makini sana jinsi mnavyoishi. Ishini kwa busara, si kama wajinga. 16 Nasema kwamba jitahidini kutumia kila fursa mliyo nayo katika kutenda mema, kwa sababu nyakati hizi ni za uovu. 17 Hivyo msiwe kama wajinga katika maisha yenu, bali mfahamu yale ambayo Bwana anapenda ninyi mfanye. 18 Msilewe kwa mvinyo, ambao utaharibu maisha yenu, bali mjazwe Roho. 19 Mhimizane ninyi kwa ninyi katika zaburi, nyimbo za sifa, na nyimbo zinazoongozwa na Roho. Imbeni na msifuni Bwana katika mioyo yenu. 20 Siku zote mshukuruni Mungu Baba kwa mambo yote katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo.
Mathayo Amfuata Yesu
(Mk 2:13-17; Lk 5:27-32)
9 Yesu alipokuwa anaondoka, alimwona mtu aliyeitwa Mathayo amekaa mahali pa kukusanyia ushuru. Yesu akamwambia, “Nifuate.” Hivyo Mathayo akasimama na kumfuata Yesu.
10 Baadaye Yesu alikula chakula nyumbani kwa Mathayo. Watoza ushuru wengi na watu wenye sifa mbaya walikuja na kula chakula pamoja na Yesu pamoja na wafuasi wake. 11 Mafarisayo walipoona kuwa Yesu anakula pamoja na watu hao, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi wengine?”
12 Yesu alipowasikia wakisema hili, akawaambia, “Wagonjwa ndiyo wanaohitaji daktari si wenye afya. 13 Nendeni mkajifunze andiko hili linamaanisha nini: ‘Sihitaji dhabihu ya mnyama; Ninataka ninyi mwoneshe wema kwa watu.’(A) Sikuja kuwaalika wema kujiunga nami, bali wenye dhambi.”
Swali Kuhusu Kufunga
(Mk 2:18-22; Lk 5:33-39)
14 Kisha wafuasi wa Yohana wakamjia Yesu na kusema, “Sisi na Mafarisayo tunafunga mara kwa mara, lakini wafuasi wako hawafungi. Kwa nini?”
15 Yesu akajibu, “Kwenye harusi marafiki wa bwana harusi hawana huzuni anapokuwa pamoja nao, hivyo hawawezi kufunga. Lakini wakati unakuja ambao bwana harusi ataondolewa kwao. Ndipo watakuwa na huzuni kisha watafunga.
16 Mtu anaposhona kiraka kwenye vazi la zamani, atatumia kiraka chakavu. Akitumia kiraka kipya vazi lake litachanika kwa sababu ya kusinyaa kwa kiraka hicho kipya. Kisha tundu litakuwa baya zaidi. 17 Pia, watu hawawaweki divai mpya kwenye viriba[a] vya zamani. Wakifanya hivyo viriba vitapasuka, na divai itamwagika na viriba vitaharibika. Daima watu huweka divai mpya katika viriba vipya, ambavyo haviwezi kupasuka, na divai huwa salama.”
© 2017 Bible League International