Book of Common Prayer
Kazi ya Paulo Thesalonike
2 Ndugu zangu, mnafahamu kuwa safari yetu kuja kwenu ilikuwa yenye nguvu. 2 Lakini kabla ya kuja kwenu, watu wa Filipi walitutenda vibaya kwa kututukana matusi mengi na kutusababishia mateso. Mnafahamu yote kuhusu hilo. Na kisha tulipokuja kwenu, watu wengi huko walitupinga. Tuliwaeleza ninyi Habari Njema za Mungu lakini ni kwa sababu Mungu alitupa ujasiri tulio hitaji. 3 Hatukuwa na kitu cha kupata faida kwa kuwaomba ninyi muiamini Habari Njema. Hatukuwa tunataka kuwafanya wajinga wala kuwadanganya. 4 Hapana, tulifanya hivyo kwa sababu Mungu ndiye aliyetuagiza kazi hii. Na hii ilikuwa baada ya yeye kutupima na kuona ya kuwa tunaweza kuaminiwa kuifanya. Hivyo tunapoongea, tunajaribu tu kumpendeza Mungu, na sio wanadamu. Yeye tu ndiye awezaye kuona kilichomo ndani yetu.
5 Mnafahamu kuwa hatukujaribu kuwarubuni kwa kusema mambo mazuri juu yenu. Hatukuwa tunatafuta jinsi ya kuzichukua pesa zenu. Hatukutumia maneno ama matendo kuficha tamaa yetu. Mungu anajua ya kuwa huu ni ukweli. 6 Hatukuwa tukitafuta sifa toka kwa watu ama kutoka kwenu au kwa mtu yeyote.
7 Tulipokuwa pamoja nanyi, kama mitume wa Kristo tulikuwa na uwezo wa kutumia mamlaka yetu kuleta madai ya nguvu kwenu. Lakini tulikuwa wapole kwenu.[a] Tulikuwa kama vile mkunga anavyowahudumia watoto wake wadogo. 8 Ilikuwa ni upendo wetu mkuu sana kwenu uliotufanya tuwashirikishe Habari Njema za Mungu. Zaidi ya hayo yote tulifurahi kuwashirikisha ninyi nafsi zetu wenyewe. Hiyo inadhihirisha ni kwa kiwango gani tuliwapenda. 9 Ndugu zangu, ninajua kuwa mnakumbuka jinsi tulivyofanya kazi kwa bidii. Tulifanya kazi usiku na mchana ili tujitegemee, pasipo kumwelemea mtu yeyote wakati tukifanya kazi ya kuhubiri Habari Njema za Mungu.
10 Tulipokuwa pamoja nanyi enyi mnaoamimi, tulikuwa safi, wa kweli, na wasio na kosa lolote kwa namna tulivyoishi maisha matakatifu. Mnafahamu, kama vile Mungu anavyotenda, kuwa jambo hili ni la kweli. 11 Mnafahamu jinsi tulivyo mtendea kila mmoja wenu kama vile baba anavyowatendea wanaye. 12 Tuliwatia moyo, tuliwafariji, na tuliwaambia kuishi maisha mema kwa Mungu. Yeye anawaita muwe sehemu ya maisha mema mbele za Mungu.
Yesu Afundisha Kuhusu Sheria ya Musa
17 Msifikiri kwamba nimekuja kuiharibu Sheria ya Musa au mafundisho ya manabii. Sikuja kuyaharibu mafundisho yao bali kuyakamilisha. 18 Ninawahakikishia kuwa hakuna jambo litakaloondolewa katika sheria mpaka mbingu na nchi zitakapopita. Hakuna hata herufi ndogo ama nukta katika Sheria ya Musa itakayotoweka mpaka hapo itakapotimizwa.
19 Kila mtu anapaswa kutii kila amri iliyo katika sheria, hata ile isiyoonekana kuwa ya muhimu. Kila atakayevunja mojawapo ya amri hizi ndogo na kuwafundisha wengine kuzivunja atahesabiwa kuwa ni mdogo sana katika ufalme wa Mungu. Lakini kila anayeitii na kuwafundisha wengine kuitii sheria atakuwa mkuu katika ufalme wa Mungu. 20 Ninawambia, ni lazima muitii sheria ya Mungu kwa kiwango bora kuliko kile cha walimu wa sheria na Mafarisayo. La sivyo, hamtaweza kuingia katika ufalme wa Mungu.
© 2017 Bible League International